Mthamini Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha akiangalia moja ya nyumba iliyofanyiwa uthamini kwa ajili ya kulipwa fidia katika kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara kupisha upanuzi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la taka sumu jana. Kulia ni Mthamini kutoka wilaya ya Serengeti Bariki Ileta.
Mthamini Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha (Nyuma) akiwa na wataalamu wa Uthamini kutoka Serengeti Bariki Ileta (Mbele) na Bisare Charles kutoka Tarime wakati wa zoezi la Uthamini linaloendelea katika kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara ili kulipwa fidia kupisha upanuzi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la taka sumu jana.
Mthamini Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha (kushoto) akitoa maelekezo kwa wataalamu wa Uthamini wakati wa zoezi la Uthamini katika kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara ili kulipwa fidia kupisha upanuzi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la taka sumu jana.
Mkazi wa kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara Marwa Mangora Mube akiwaoongoza wataalamu wa Uthamini kukagua eneo lake kwa ajili ya kufanyiwa tathmini ili kulipwa fidia kupisha upanuzi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la taka sumu jana.
Wataalamu wa Upimaji kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakiandaa vifaa tayari kwa upimaji wakati wa zoezi uthamini katika kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara ili kulipa fidia kwa wananchi kupisha upanuzi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la taka sumu jana. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

************************************ 


Na Munir Shemweta, WANMM NYAMONGO

Serikali imeanza kusikiliza kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Nyamongo katika wilaya ya Tarime mkoani Mara kwa kuanza kufanya tathmini ya fidia ya kutwaa eneo la ardhi kwa ajili ya kupanua Mgodi wa Dhahabu wa ACACIA North Mara ili kujenga Bwawa la Maji Taka.

Tayari timu ya wataalamu 25 kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inayojumisha Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali pamoja na idara ya Upimaji na Ramani iko eneo la Nyamongo kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoani Mara kutathmini mali za wananchi ili kulipwa fidia na kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Maji Taka.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo jana katika kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara Mthamini Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha alisema, zoezi la uthamini linalofanyika ni kwa ajili ya kutwaa eneo la ujenzi wa Bwawa la Maji Taka katika eneo la Nyamongo lenye ukubwa wa hekta 237 ambalo linahusisha vitongoji vitatu vya Kigonga A, Kwinyunywi na Kigonga B ambapo uthamini wake ulishaanza toka mwezi julai mwaka huu.

Mugasha alisema, uthamini huo unaangalia mali inayohamishika na ile isiyohamishika na kufuata sheria ya ardhi na ile ya kijiji na kusisitiza uthamini huo umekuwa ukifanyika kwa uwazi na hauna lengo la kumnufaisha au kumpunja mtu yeyote.

‘’ Eneo la Nyamongo tunalichukulia kama eneo la mfano hasa baada ya kufanyika tathmni maeneo mbalimbali ya mgodi miaka ya nyuma na kubaini udanganyifu wa baadhi ya wananchi na Wathamni wasiowaaminifu kutumia zoezi kama hili kujinufaisha’’ alisema Mugasha.

Kwa mujibu wa Mthamini Mkuu wa Serikali, udanganyifu wowote utakaofanyika kwa nia ya mmiliki wa nyumba ama eneo kujinufaisha Ofisi yake haitamvumilia kwa kuwa baada ya uthamini wanafanya uhakiki kujiridhisha usahihi wa taarifa na mali za wananchi.

Mthamini kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu Lazaro Mayumba anayeshiriki zoezi hilo alisema, zoezi hilo linafanyika kwa kasi kwa kuwa serikali ina jukumu la kulinda mali na afya za wananchi waliokuwa wakilalamikia kwa muda mrefu kuhusu kutiririka maji yenye sumu katika Mgodi wa Dhahabu wa ACACIA North Mara.

Alieleza kuwa, katika kuhakikisha wananchi wanaozunguka mgodi huo hawaathiriki na wakati huo mgodi haufungwi kutokana na madhara yanayopatikana dhidi ya taka sumu, serikali iliona iko haja kutwaa eneo litakalosaidia mgodi kupata eneo kwa ajili ya ujenzi bwawa kubwa na lenye ubora ambalo halitaleta madhara yanayodaiwa na wananchi.

”Mbali na madai ya wananchi wanaozunguka mgodi wa North Mara lakini pia athari za taka sumu zinaweza kufika mto Mara ambao uko umbali wa takriban kilometa tatu kutoka katika Mgodi na kama hatua za haraka hazitachukuliwa unaweza kuharibu uoto wa asili pamoja na mbuga za wanyama”’ alisema Mayumba.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Matongo linakofanyika zoezi la Uthamini wameonesha kufurahishwa na hatua ya serikali kuamua kutafuta eneo kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa jipya la taka sumu za Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa madai kuwa wamekuwa wakiathirika sana na maji yanayotiririka katika mgodi huo.

Gaga Sita Kishashila mmoja wa wakazi wa kijiji cha Matonga alisema pamoja na zoezi la uthamini linaloendelea sasa lakini shauku kubwa ya wakazi hao ni kutaka kujua wanalipwa lini ili waweze kuondoka maeneo hayo mapema na hofu yao ni kukwama kwa zoezi hilo kama ilivyotokea huko nyuma.

Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Simion Kirario aliomba uthamini unaofanyika kuangalia na hali za wananchi hao kwa kuwa baadhi yao wana hofu ya kulipwa kiasi kidogo kutokana na aina ya nyumba wanazomiliki za Msonge huku wakihitaji kuwa na fedha nzuri itakayowawezesha kununua eneo lingine na kufanya maendelezo.

Mwenyekiti wa Kitongoni cha Kigonga A Kibwabwa Mwita Kibwabwa alisema kazi ya uthamni katika kitongoji chake imeenda vizuri kwa kuwa zoezi hilo linafanyika kwa kasi na wananchi wake wanataka kujua wanalipwa lini. Hata hivyo alisema baadhi ya wananchi wamelalamikia kiasi watakacholipwa na kukiona kidogo ukilinganisha na matarajio yao.

Kwa muda mrefu wananchi wa Nyamongo wilaya ya Tarime mkoa wa mara hasa wale wanaoishi vitongoji vinavozunguka Mgodi wa Dhahabu wa ACACIA North Mara wamekuwa wakilalamikia uchafuzi wa mazingira hasa maji yanayovuja kutoka Mgodi huo kuwa yana sumu inayoathiri afya zao jambo lililomlazimu Rais John Pombe Magufuli wakati wa ziara yake katika eneo hilo kuagiza kufanyika utafiti ili kubaini ukweli huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...