Charles James, Michuzi TV

WATANZANIA wameaswa kupiga vita mambo matatu ambayo ni rushwa, ubaguzi pamoja na unyanyapaa wa namna yoyote ile katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Elirehema Kaaya baada ya kutoka kujiandikisha katika daftari la orodha ya wapiga kura katika kituo cha Site One mtaa wa Mlimwa jijini Dodoma leo.

Kaaya amesema anawahamasisha wananchi wa Dodoma na watanzania kwa ujumla kujitokeza katika zoezi hilo la uandikishaji ili waweze kuchagua kiongozi bora atakaewatumikia kwa miaka mitano.

Amesema ALAT ni wadau wakubwa wa Tawala za Mikoa hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi ili kuweza kutimiza haki yao ya msingi.

" Katika wakati huu ambao wananchi wanajiandikisha nipende kuwakumbusha kutokubali kutumika kama daraja la kuwapandisha watu wanaotaka uongozi kwa namna ambayo siyo ya kikatiba na kidemokrasia.

Niwasihi sana watanzania kutoruhusu vitendo vya rushwa kuchukua nafasi, tupige vita unyanyapaaji wa namna yoyote ile iwe ya kijinsia, kidini na kikabila," Amesema Kaaya.

Amewataka watanzania kuchagua viongozi waadilifu wenye uzalendo kwa Nchi yao ambao wataweza kurahisisha maendeleo katika Mitaa yao wakishirikiana na viongozi wa ngazi ya Kitaifa.

" Katika kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere basi tumuenzi katika kuchagua viongozi wenye uchungu na rasimali zao, viongozi watakaochukia rushwa kama Rais Magufuli anavyoichukia," Amesema Kaaya.

Ametoa wito kwa vijana na wanawake sambamba na watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu ili waweze kuomba ridhaa ya uongozi katika Mitaa wanayoishi.

Akitolea ufafanuzi suala la uandikishaji, Kaaya amesema kumekua na upotoshaji wa namna ya uandikishaji huku akisema Mwananchi atakayeruhusiwa kupiga kura ni yule ambaye yupo kwenye daftari la orodha na siyo kuwa na kitambulisho cha mpiga kura kama wengi wanavyosema.

" Kumekua na upotoshaji kwamba mtu ambaye ana kadi ya mpiga kura anaweza kupiga kura bila kujiandikisha. Huo ni upotoshaji wote wenye sifa wanapaswa kujiandikisha katika daftari hili la orodha," Amesema Kaaya.
 Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT), Elirehema Kaaya akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma baada ya kutoka kujiandikisha katika daftari la orodha ya wapiga kura
 Katibu Mkuu wa ALAT, Bw Elirehema Kaaya akijiandikisha katika daftari la orodha ya wapiga kura katika kituo cha Site One mtaa wa Mlimwa jijini Dodoma leo
 Katibu Mkuu wa ALAT akizungumza na wanadishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma baada ya kutoka kujiandikisha katika daftari la orodha ya wapiga kura.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...