Na Said Mwishehe,Michuzi Globu ya jamii

WAZIRI wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola amesema siku za mtu anayejiita Kigogo anayetumia mtandao wa kijamii na hasa Twitter kutukana,kukejeli na kuikashfu Serikali ya Awamu ya Tano anatakiwa kufahamu siku zake zinahesabika.

Kwa muda sasa mtu anayejiita Kigogo2014 amekuwa akitumia mtandao wa kijamii kutoa taarifa mbalimbali ambazo nyingi zimekuwa zikilalamikiwa na nyingine zimekuwa  zikisababisha mjadala mtaani na mitandaoni kiasi cha baadhi ya Watanzania kuhoji huyo Kigogo ndio nani,maana haijafahamika kwa jina zaidi ya kutumia sura kama  ya mwanamuziki maarufu wa Marekani Jay Z ingawa alichokifanya ni kuuurefusha mdomo.

Waziri Lugola ameyasema hayo leo Novemba 2,mwaka 2019 jijini Dar es Salaam  wakati anazungumzia utendaji kazi wa Jeshi la Polisi nchini ambapo ameeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa jeshi hilo chini ya uongozi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi ,IGP Simon Sirro.

Hata hivyo waandishi walitaka kufahamu hatua ambazo zinachukuliwa kukabiliana na baadhi ya watu wenye kutumia mitandao ya kijamii kutoa lugha za kukejeli,kashfa,kuzusha na dhihaka dhidi ya wengine na hasa Kigogo2014, ambapo Waziri Ligola amesema kila mtu anafahamu kalenda inavyohesabiwa ,hivyo Kigogo atambue siku zake zinahesabika na siku si nyingi atpatikana.

" Huyo anayejiita Kigogo afahamu kwamba siku zake zinahesabika , ni kama vile kuhesabu kalenda unaanza moja hadi 31 ,hivyo tutampata tu, "amesema Waziri wakati akijibu swali kuhusu mtu huyo na kuongeza Watanzania wanatakiwa kutumia mitandao vizuri na sio kuitumia kwa ajili ya kupotosha, kuchonganisha au kutukana wengine kwani sheria itachukua mkondo wake.

Mbali ya kuzumzungumzia Kigogo, Waziri Lugola ameeleza kutokana na utendaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi chini ya Serikali  ya Awamu ya Tano ya Rais Dk.John Magufuli, usalama wa raia na mali zao umeimarika na hata matukio ya ujambazi yamepungua kwa asilimia kubwa .

Amesema kuwa Jeshi la Polisi liko imara wakati wote,hivyo amesema wenye tabia ya kujihusisha na uhalifu watambue kuwa hawako salama na wasithubutu kutenda uhalifu kwani watakamatwa na watakaokuwa wabishi kwa Kupambana na Polisi watashughulikiwa.

Pia amesema kuna majambazi ambao wamekuwa wakifanya ujambazi na kisha kukimbilia Mkoa wa Kigoma na Kagera, hata hivyo ameeleza Polisi wameizingira Mikoa hiyo na hivyo majambazi walioko huko muda wowote watakuwa mikononi mwa jeshi hilo.

Kuhusu vitendo vya rushwa, Waziri huyo amesema kwa sehemu kubwa rushwa imepungua lakini ametoa rai kwa kila Mtanzania kuchukia rushwa kwani hakuna rushwa kama hakuna anaetoa,hivyo mtoa rushwa na mpokea rushwa wote ni wakosefu mbele ya sheria.

Pia amezungumzia wa watu kutoa malalamika iwapo watakuwa nayo dhidi ya Jeshi la Polisi lakini ni vema wakafuata utaratibu kwa kuonana na wakuu wa vituo vya Polisi na wakaona hawajaridhika wanakwenda kwa wakubwa zaidi na hata kwa IGP au Wizara ya Mambo ya Ndani.

Amesema kwa kufanya hivyo anaamini malalamiko dhidi ya Polisi kama yapo badi yatapata ufumbuzi kwani kuendelea kulalamika bila kufuata utaratibu huo inaweza kuonekana kama majungu.
 Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhe. Kangi Lugola akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo Novemba 2,2019 jijini Dar  es Salaam,kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo suala la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,Uhalifu na matumizi mabaya ya silaha na  mitandao ya kijamii.
Waziri wa Mambo ya Ndani,Mhe. Kangi Lugola akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo suala la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,Uhalifu na matumizi mabaya ya silaha na mitandao ya kijamii.Pichani kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,Meja Jenerali Jacob Kingu na kushoto ni Mkuu wa Jeshi la Polisi ,IGP Simon Sirro.Picha na Michuzi JR.(MMG).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...