*Asema chini ya Rais Magufuli mambo yanakwenda vuziri
*Awatumia salamu wananchi wanaozunguka Ziwa Victoria


Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Kagera

WAZIRI wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Issack Kamwele amesema amekuwa katika ziara ya siku mbili mkoani Kagera kwa ajili ya kukagua maendeleo ya miradi ya ujenzi wa miundombinu katika bandari ya Kemondo na bandari ya Bukoba huku akitumia nafasi hiyo kuelezea mikakati inayochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano kuboresha sekta ya usafiri nchini.

Katika bandari za Kanda ya Ziwa, Waziri Kamwelwe amesema kupitia maelekezo yaliyotolewa na Rais Dk.John Magufuli baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani kuhusu uboreshwaji wa bandari za maziwa makuu kumekuwa na jitihada zinazoendelea.

Huku akieleza kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera ule usafiri wa meli ambao ni wa raha mustarehe utarejea kutokana na ujenzi wa meli mpya unaoendelea pamoja na kufanyiwa matengenezo kwa meli za zamani ikiwemo MV.Bukoba. 

Akizungumza na waandishi wa habari walioko kwenye ziara ya kutembelea miradi inayotekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania(TPA) katika bandari za Ziwa Victoria, Waziri Kamwelwe amesema ziara yake inalenga kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa na Serikali.

Kuhusu bandari ya Bukoba amesema ilianza kujengwa mwaka 1943 na kukamilika mwaka 1945 na wakati huo ilianza kutumia kwa vyombo mbalimbali vya majini lakini baadaye nchi ikawa na meli kama Mv Bukoba, Mv Victoria, Mv Butiama.

"Mv Victoria kwa bahati mbaya ilizama lakini pia tulikuwa na meli nyingine Mv Clarias ambayo nayo iliharibika.Baada ya kuanza Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk.John Magufuli ambaye amekuwa na dhamira thabiti ya kusubutu na ametoa maelekezo, ndio mnaona haya maendeleo sasa bandari hii inakarabatiwa ili iwe mpya.

"Kinachofanyika ni pamoja na kukarabati magati kwa ajili ya meli ili ziweze kufika sehemu na kuegesha, pia maghala kwa ajili ya mizigo, chumba cha abiria ambao wanasubiri kusafiri, ofisi za wafanyakazi wa TPA, Kampuni ya Meli Tanzania pamoja na TASAC ambaye ni dhibiti ili sasa Bandari hii ianze kufanyakazi rasmi,"amesema Waziri Kamwelwe.

Amesema kuwa wanashukuru katika ukarabati unaoendelea tayari wamekarabati meli ya Mv Umoja ambayo yenyewe inaingia behewa 19 na tayari meli hiyo imeanza kufanya kazi. Amefafanua kuwa meli hiyo ya Umoja inabeba behewa ya shehena ya mizigo na kuipeleka pia nchini Uganda katika Bandari ya Port Bell Uganda lakini ikiwa huko inachukua mizigo ikiwemo ya kahawa na mabati inaleta nchini Tanzania.

"Kwa sasa tumekarabati bandari hii na sasa hivi pia tunakarabati Bandari ya Kemondo sasa, juhudi ambazo zimefanywa na Rais wetu Dk. John Magufuli, anakarabati meli ya Mv Victoria, Mv Butiama na ukarabati unavyoendelea unakwenda kwa kasi kubwa.Zile meli zinabadilika zinakuwa mpya kwa sababu vifaa vyote vinavyofungwa ikiwamo injini, majenereta vyote mpaka viti ni vipya,"amesema.

Kuhusu matarajio yake, na Serikali kwa ujumla, amesema kuanzia Machi mwaka 2020 ukarabati wa meli mbili utakuwa umekamilika na hivyo kuanzia Aprili mwakani MV.Victoria itaanza kubeba abiria kutoka Mwanza na kuzunguka kwenye magati mengine kama Nyamirembe na kwenda Musoma kuja Kemondo pamoja na Bukoba. Amesisitiza kazi ya maboresho inaendelea vizuri, hivyo wana Bukoba ule usafiri wao wa raha uliosimama kwa muda mrefu karibu utaanza tena.

"Kama ambavyo tumerudisha usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam, treni kutoka Tanga ambayo sasa inakwenda Kilimanjaro inaendelea na safari kwa kubeba saruji na sasa wanabeba abiria. Kwa kipindi hiki cha kueleka mwaka mpya na Krismasi hawalanguliwi tena pale Ubungo kwani treni ipo na ipeleka abiria Moshi.

"Hivyo tukifika Aprili mwakani tutakuwa tunatembeza meli za Mv Victoria ili sasa kurudisha na kurahisisha usafiri ndani ya maji usafiri ambao ni wa raha na pia nauli yake ni nafuu zaidi. Nipongeze TPA, wananchi na sekta binafsi walioamua kutoa huduma za boti za kubeba mizigo na abiria.Ndio maana TPA wamejenga gati dogo hapa Bukoba pamoja na jengo dogo la mizigo,"amesema.

Akielezea maboresho yanayofanyika bandari ya Bukoba,Waziri Kamwelwe amesema kuwa mwaka 1945 Bukoba haikuwa na nyumba nyingi lakini leo hii zipo nyingi na watu ni wengi, hivyo shughuli za uchumi zimeongezeka."Ndio maana Serikali ya CCM iliyochaguliwa na wananchi inaendelea kutekeleza yote ambayo iliahidi."

Akizungumzia bandari ambazo zina usafiri wa reli wa ajili ya kubeba mabehewa ya mizigo, Waziri Kamwelwe amesema tayari TPA wameshaagiza injini sita za treni ambazo zitakuwa katika Bandari ya Kemondo, Musoma kwa ajili ya kumvuta behewa za mizigo.

"Baada ya Rais kumuagiza Waziri Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina kuzuia uvuvi haramu hivi sasa tunazalisha samaki wengi na wakubwa ikiwamo minofu ya samaki tani za kutosha, ndio maana tuko kwenye hatua za mwisho ili Air Cargo ije Mwanza ibebe minofu ya samaki na kupelekwa moja kwa moja Ulaya pamoja na maeneo mengine yote ambayo wanaohitaji kula samaki.Watanzania nao watakula samaki si kwamba tutasafirisha wote,"amesema.

Hata hivyo amesema kazi inaendelea vizuri ambapo ametumia nafasi hiyo kuipongeza TPA kwa kusimamia vema shughuli zote hizo na kazi ambayo imebaki itakuwa kutoa huduma tu kwa wananchi.
 Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Issack Kamwelwe akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 13 akiwa katika Bandari ya Bukoba mkoani Kagera ambako amefanya ziara ya kukagua uboreshaji wa miundombinu.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Issack Kamwele akifafanua jambo akiwa katika bandari ya Bukoba mkoani Kagera.
 :Waziri Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano akiwa katika gati ya Bandari ya Kemondo Bay iliyopo mkoani Kagera ambapo amefika kuangalia kasi ya uboreshaji wa gari hiyo ya reli ambayo ni maalum kubeba mahewa ya mizigo.
 Meneja wa Bandari za Kanda ya Ziwa Morris Mchindiuza akizungumza mbele ya Waziri wa Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Issack Kamwelwe (aliyekaa kushoto)kuhusu hatua mbalimbali za uboreshaji wa miundombinu katika bandari ya Bukoba na Bandari ya Kemondo baada ya Waziri huyo kufanya ziara jana na leo.
 Mwakilishi wa Kiwanda cha Simba Cement (pembeni ya Waziri kushoto) akizungumza kuhusu umuhimu wa bandari ya Kemondo na Bandari ya Bukoba katika usafirishaji wa saraji kwa mkoa wa Kagera.
 Mfanyabiashara mkubwa mkoani Kagera akizungumza na Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Issack Kamwelwe(hayupo pichani) kuhusu huduma za usafirishaji wa mizigo katika bandari ya Bukoba na ile ya Kemondo.
 Meneja wa Bandari za Kanda ya Ziwa Morris Mchindiuza(kulia) akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Issack Kamwelwe.
 Gari ya kubeba mizigo ikiwa katika bandari ya Bukoba ikiwa imeegeshwa baada ya mizigo kupakiwa katika meli ya mizigo katika eneo hilo.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...