Jeshi la Polisi mkoa
wa Mbeya limeendelea kukabiliana na vitendo vya uhalifu na ajali za barabarani
ili kuhakikisha kuwa wageni na wakazi wa mkoa huu wanaendelea kuwa salama na mali
zao. Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kushirikiana na wananchi
na wadau wengine wa usalama hali inayopelekea kupata mafanikio makubwa ikiwa ni
pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu, ajali za barabarani na
kukamatwa kwa watuhumiwa mbalimbali wa uhalifu.
Baadhi
ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na misako na doria ni kama ifuatavyo:-
i.
KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI.
Jeshi la Polisi Mkoa
wa Mbeya linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kupatikana na Nyara za
Serikali vipande kumi na moja [11] vya
meno ya Tembo vyenye uzito wa kilo 21.5 sawa
na Tembo 4 wenye thamani ya Tshs 137,970,000/=. Watuhumiwa hao ni:-
1. ABDULMARIK UPETE [41] mkazi wa Uyole
2. MOHAMED OMARY [50] mkazi wa Kilosa
Mkoani Morogoro na
3. AYOUB KIDUMBA [49] mkazi wa Ilembula
Mkoani Njombe.
4. LAWI KALONGA [50] mkazi wa Mkoani
Dodoma.
Watuhumiwa
walikamatwa Disemba 21, 2019 majira ya saa 18:30 jioni huko eneo la Soweto
lililopo Kata ya Ruanda, Tarafa ya Iyunga Jijini Mbeya baada ya Jeshi la Polisi
kuweka mtego. Nyara hizo zilisafirishwa kutoka Mkoani Njombe kwa lengo la
kutafuta wateja na zilikuwa zimehifadhiwa kwenye duka la kuuza vipuri vya
magari mali ya ABDULMARIK UPETE.
Taratibu za kisheria zinafanywa ili watuhumiwa wafikishwe Mahakamani.
ii.
KUINGIZA BIDHAA NCHINI BILA KULIPIA USHURU.
Jeshi la Polisi Mkoa
wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili [02] kwa tuhuma za kuingiza nchini
bidhaa aina ya vitenge belo 24 kila
belo moja likiwa na doti 50 za
vitenge sawa na doti 1,200 kutoka nchini Zambia bila kulipia ushuru. Mzigo
huo ulikuwa unasafirishwa kwenye gari T.471
BJJ aina ya Toyota Hiace. Watuhumiwa
waliokamatwa ni:-
1.ELIA MWAKAGILE [30] mkazi wa
Mwakibete na
2.FURAHA LUTENGANO MWAKALENGELA [35] mkazi wa Mwakibete.
Watuhumiwa
wamekamatwa Disemba 22, 2019 majira ya saa 03:00 usiku huko eneo la Ituta
lililopo Kata na Tarafa ya Iyunga Jijini Mbeya katika barabara kuu ya Mbeya –
Tunduma.
Taratibu zinafanywa
ili watuhumiwa pamoja na mzigo huo kukabidhiwa Mamlaka ya Mapato [TRA] kwa
hatua za kiforodha.
iii. KUINGIZA BIDHAA NCHINI BILA KULIPIA USHURU.
Jeshi la Polisi Mkoa
wa Mbeya linamshikilia mtuhumiwa mmoja [01] MARIAM JAPHET [35] Mkazi wa Ilembo – Mbeya kwa tuhuma za kuingiza
nchini bidhaa aina ya vitenge doti 42
kutoka nchini Malawi bila kulipia ushuru.
Mtuhumiwa amekamatwa
Disemba 22, 2019 majira ya saa 06:30 alfajiri huko eneo la stendi ya mabasi
Kyela, iliyopo Kata ya Kyela – Kati, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa
wa Mbeya.
Taratibu zinafanywa
ili mtuhumiwa pamoja na mzigo huo kukabidhiwa Mamlaka ya Mapato [TRA] kwa hatua
za kiforodha.
iv. KUKAMATWA WATUHUMIWA WANAOJIHUSISHA NA
MTANDAO WA WIZI WA PIKIPIKI NA MATUKIO MENGINE
YA UHALIFU.
MTANDAO WA WIZI WA PIKIPIKI NA MATUKIO MENGINE
YA UHALIFU.
Katika kipindi hiki
cha kuelekea mwishoni mwa mwaka - 2019 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanya
msako maeneo mbalimbali Mkoani Mbeya dhidi
ya wahalifu wa matukio mbalimbali ikiwemo mtandao wa wizi wa Pikipiki.
Katika misako
iliyofanyika jumla ya watuhumiwa wanne
[04] wamekamatwa, wamehojiwa na wamekiri kufanya matukio kadhaa ya uporaji
wa Pikipiki na kuziuza nchi jirani ya Malawi na Zambia.
Watuhumiwa waliokamatwa
katika misako ya hivi karibuni ni pamoja:-
1. ADAM BRAYSON SANGA [27] Bodaboda, mkazi
wa Iyunga
2. OSCAR ELIAS MWAKABIKI [25] mkazi wa
Utengule – Mbalizi na
3. BENJAMIN SILVESTER MWANDATA [26]
Bodaboda na mkazi wa Utengule – Mbalizi.
4: RAMADHAN BAKARI [25] mkazi wa Lupa –
Chunya.
V.
KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA WIZI KWENYE MAGARI.
Jeshi la Polisi Mkoa
wa Mbeya litaendelea kufanya misako na doria katika maeneo yote ili kuhakikisha
linasambaratisha mtandao wa wizi wa Pikipiki na wahalifu wengine kwa
kushirikiana na wananchi na wadau wengine vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama
ndani ya Mkoa wa Mbeya.
Kutokana na kuibuka
kwa wizi wa vifaa vya magari katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya, Jeshi
la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanya misako na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa
wanne [04] kuhusiana na matukio ya wizi kwenye magari, kuvunja vioo vya magari
na kuiba betri za magari, kufungua milango ya magari na kuiba vitu vya thamani.
Watuhumiwa
waliokamatwa kuhusiana na matukio hayo ni:-
1.
JOSEPH
SIMON @ MBOGOLO @ WHITE [40] Mkazi wa Mwananyamala
D’Salaam.
2.
FAIDHA
NSAJIGWA @ MWASEBA [44] Mkazi wa Isanga.
3.
GABRIEL
MWANDWANGA [48] Mkazi wa Manga – VETA.
4.
AYOUB
EMANUEL KISUNGA [22] Mkazi wa Iyela
Watuhumiwa hao
walikutwa na vifaa vya kuvunjia magari na baada ya kuhojiwa wamekiri kuhusika
na matukio kadhaa ya wizi kwenye magari katika maeneo ya Forest, Kabwe, Isanga,
Uyole, Sokomatola na Mwanjelwa Jijini Mbeya. Pia wamekiri kufanya matukio kama
hao katika mikoa ya Arusha na Tanga.
Misako na ufuatiliaji
wa taarifa mbalimbali za kuzuia na kupambana na uhalifu Mkoani Mbeya inaendelea
vizuri.
vi.
MAUAJI
Jeshi la Polisi Mkoa
wa Mbeya linawashikilia watu wawili mke na mume ambao ni ALLY MBAVU [23] na SABINA
ALEX [19], wakazi wa Pambogo kufuatia kifo cha mtoto wao ISMAIL ALLY MBAVU [mwaka 1 na miezi 11]
Tukio hilo limetokea
Disemba 22, 2019 majira ya saa 06:30 alfajiri huko mtaa wa Pambogo, Kata ya
Iyela, Tarafa ya Iyunga Jijini Mbeya. Marehemu alitoweka nyumbani kwao tangu Disemba
21, 2019 jioni na hakuonekana mpaka alipokutwa amefariki dunia.
Uchunguzi wa shauri
hili unaendelea na mara baada ya kukamilika, watuhumiwa watafikishwa
Mahakamani.
vii. KUELEKEA SIKUKUU ZA KRISMAS NA MWAKA MPYA.
Katika kuelekea
sikukuu za Mwisho wa Mwaka [Krismas] na Mwanzo wa Mwaka [Mwaka Mpya] Jeshi la
Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga kikamilifu kuhakikisha wakazi wa Mkoa wa
Mbeya, wageni na wakazi wa mikoa jirani wanasherehekea sikukuu hizo kwa amani
na utulivu.
Kwa kutambua kuwa
Mkoa wetu unapakana na nchi jirani ya Malawi pia barabara kuu inayounganisha
nchi yetu na nchi jirani pamoja na mikoa jirani imepita hapa, tumejipanga
vizuri kuhakikisha usalama kwa watumiaji wa barabara wakiwemo madereva na
watembea kwa miguu. Wito wangu kwa watumiaji wote wa barabara kuzingatia
sheria, alama na michoro ya usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza
kuepukika.
Kuelekea kipindi hiki
cha sikukuu, waumini wa madhehebu mbalimbali ushiriki katika ibada/misa kwa
nyakati tofauti kulingana na ratiba zao, Jeshi la Polisi limejipanga
kuhakikisha ulinzi na usalama katika makanisa pamoja na misikiti hasa katika
misa au ibada za mkesha. Aidha ninatoa wito kwa viongozi katika makanisa na
misikiti kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri hasa katika suala la ulinzi kwa
kuunda kamati za ulinzi na usalama ili kuhakikisha ulinzi unakuwepo maeneo ya
ndani na nje ya Makanisa na Misikiti.
Pia rai kwa wamiliki
wa Kumbi za starehe kufuata sheria hasa kuzingatia Leseni zao za biashara zinavyowaelekeza
ikiwa ni pamoja na kuzingatia muda wa kufungua na kufunga sehemu zao za
biashara, wenye kumbi za muziki kuhakikisha kambi zao zinaingiza idadi ya watu
inayohitajika [capacity] pamoja na kuweka walinzi katika maeneo
yanayowazunguka.
Kuelekea msimu huu wa
sikukuu, ni wito wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa wazazi, walezi na jamii
kwa ujumla kuzingatia ulinzi wa mtoto, na pia kuwasaidia watoto hasa kuwavusha
katika maeneo tete kama vile barabarani au maeneo yenye mito ili kuepuka
madhara yanayoweza kuwapata. Pia ili kuepuka watoto kupotea katika kipindi cha
sikukuu, wazazi na walezi wanapaswa kuongeza umakini, uangalizi wa watoto wao
kila mahali wanapokwenda iwe ni makanisani, misikitini au katika maeneo yenye
michezo ya watoto ikiwemo fukwe za ziwa nyasa Matema na Ngonga Wilayani Kyela.
Mwisho, nitumie
fursa hii kuwatakia wananchi wote wa mkoa wa Mbeya na Watanzania kwa ujumla Kheri
ya Krismas na Mwaka Mpya 2020 tukumbuke kufanya vitu kwa kiasi,
tusivuke viwango/mipaka.
Ahsanteni.
Imetolewa
na:
[ULRICH O. MATEI - SACP]
KAMANDA
WA POLISI MKOA WA MBEYA.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...