Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
akifafanuliwa jambo na Mkurugenzi wa Uendeshaji (MIUKI) NHC, Haikamen
Mlekio, wakati alipokagua Mradi wa Ujenzi wa Hospital ya Rufaa Kanda ya
Ziwa, iliyopo katika Manispaa ya Musoma Mjini, mkoani Mara, Desemba 7,
2019.



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua Mradi wa Ujenzi wa Hospital ya Rufaa Kanda ya Ziwa, iliyopo katika Manispaa ya Musoma Mjini, mkoani Mara, Desemba 7, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
SERIKALI KUFUNGUA TIBA ZA MIFUPA NA MISULI HOSPITALI
YA MKOA WA MARA - MAJALIWA
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali
inatarajia kufungua kitengo cha tiba za mifupa na misuli katika hospitali ya
rufaa ya mkoa wa Mara Kwangwa mara hospitali hiyo itakapokamilika kujengwa.
Akizungumza mara
baada ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo iliyopo Manispaa ya Musoma mkoani
Mara, leo mchana (Jumamosi, Desemba 7, 2019), Waziri Mkuu amesema kitengo hicho
kitakuwa cha pili kwa ukubwa kikifuatia cha MOI Muhimbili.
“Lengo la
kufungua kitengo hiki kwenye hospitali hii ni kusogeza huduma karibu na
wananchi hususan wa Kanda ya Ziwa ambao kwa sasa wanategemea huduma hizo kutoka
hospitali ya Bugando, jijini Mwanza ambayo pia imezidiwa kutokana na udogo
wa kitengo hicho kwenye hospitali hiyo,” amesema.
Amesema kuwa
ujenzi wa hospitali ya Kwangwa ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa
na Serikali ya awamu ya tano ambapo mbali na kutoa huduma za afya lakini pia
hospitali hiyo itafungua fursa zaidi za kiuchumi kwa mkoa wa Mara.
Waziri Mkuu amesema
Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliagiza kutolewa kwa shilingi bilioni 15 kwa ajili
ya ujenzi wa hospitali hiyo uliokwama kwa zaidi ya miaka 40 na ameridhishwa na
ujenzi wake unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Bw. Adam Malima alisema hospitali
hiyo inatarajiwa kuanza kutoa huduma ya mama na mtoto ifikapo Februari, mwakani
baada ya kukamilika kwa jengo A (wing A) mapema mwakani.
Bw. Malima alisema
kuwa huduma za rufaa za hospitali ya mkoa wa Mara zinatarajiwa kuanza kutolewa Mei,
mwakani huku huduma za kibingwa zikitarajiwa kuanza kutolewa kabla ya mwisho wa
mwaka 2020.
Mkuu huyo wa
Mkoa amesema kuwa baada ya Rais Magufuli kupokea ombi kutoka mkoa wa Mara
kuhusu kusaidia mkwamo wa ujenzi huo, Serikali ilitoa fedha zote (sh. bilioni 15)
kwa mara moja ili kukamilisha ujenzi huo.
Katika ziara
hiyo, Waziri Mkuu akiwa ameambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa, ameiwakilisha
Serikali kwenye mazishi ya kaka wa mke wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania,
Mama Maria Nyerere katika kijiji cha Kinesi kilichopo wilayani Rorya, mkoani
Mara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...