Na Dkt. Ramadhani K Dau
Ilikuwa siku ya ijumaa tarehe 21 Februari
2020 kiasi cha saa 4 usiku kwa saa za Malaysia wakati Mhe Balozi AshaRose
Shaaban Mtengeti-Migiro aliponipigia simu kutaka kuzungumza na mimi kuhusu mambo
mawili.
La kwanza lilikuwa la kiofisi lakini la pili ilikuwa kunipa taarifa
kuwa Bi Sharifa Hussein Kalala anaumwa na hali yake ni mbaya sana. Kwa maneno
yake Balozi Migiro, “kilichobaki ni Rehma ya Mwenyezi Mungu”.
Kwa hakika nilihuzunika na kushituka sana.
Nilihuzunika kwa sababu namfahamu Bi Sharifa kwa zaidi ya robo karne. Lakini
nilishituka kwa sababu siku ya Alhamisi tarehe 13 Februari 2020, nilimtumia Mzee
Yusuf Kalala (mume wa marehemu Bi Sharifa) ujumbe mfupi wa simu (sms) kumuarifu
kuwa Mzee Iddi Simba amefariki dunia.
Mzee Kalala alinijibu kwa ufupi kusema “Innallillah
Wainnaillahi Raajiuun” kisha akaongeza kwa kuniarifu kuwa yupo kiwanja cha
ndege cha Zurich akielekea Marekani kwa sababu Bi Sharifa anaumwa. Haikunijia
kabisa kuwa hali ya Bi Sharifa ilikuwa mbaya hadi aliponipigia simu Mhe Balozi
Migiro siku moja tu kabla ya Bi Sharifa kufikwa na umauti. Kwa huzuni kubwa,
nilipoamka asubuhi ya Jumamosi tarehe 22 Februari nikakuta ujumbe wa simu
uliotumwa kiasi ya masaa 3 yaliyopita kuniarifu kuwa Bi Sharifa Hussien Kalala
amefariki dunia!
Nimewahi kusema mara kadhaa kuwa kuandika taazia
ni jambo zito sana na haswa inapohusu mtu ambaye unaemfahamu sana. Mara zote
niandikapo taazia hutamani sana kuwa hiyo iwe ndio ya mwisho.
Kila niandikapo
taazia (hii ni ya 7), hujikuta nabakiwa na majonzi kwa muda wa siku kadhaa
baada ya kuichapisha kwa sababu kila inaposomwa, baadhi ya wasomaji hunipigia
simu au kunitumia ujumbe kueleza hisia zao. Jambo hili huwa linavuta hisia zangu
(emotions) na inakuwa kana kwamba msiba ule ndio kwanza umetokea; ni sawa na
kutonesha kidonda.
Hivyo basi, kwa kila
taazia nilizoandika, msiba kwangu huwa haumaliziki mapema. Kutokana na sababu
hii, mara hii niliamua nisiandike chochote kuhusu Bi Sharifa. Hata hivyo, nafsi
yangu inanisuta kuacha kuandika kuhusu Bi Sharifa kutokana na ukaribu wangu na
familia yote ya Mzee Yusuf Kalala. Ndipo leo ikiwa ni siku ya 5 tokea afariki
Bi Sharifa, nilipoamua nibadili uwamuzi wangu kwa sababu ningekuwa sikumtendea
haki Bi Sharifa na familia ya Mzee Kalala. Katika mazingira haya, ni bora
kwangu mimi kuendelea kuwa na majonzi kwa siku kadhaa baada ya kusomwa taazia
hii, kuliko kuacha kuandika machache kati ya mema yake mengi aliyowafanyia
binaadamu wenziwe.
Nimemfahamu Bi Sharifa tokea miaka ya 1990s
wakati nilipokuwa Mkurugenzi wa Masoko katika Mamlaka ya Bandari Tanzania
(THA). Kipindi hicho nilikuwa nasafiri mara kwa mara kwenda Marekani kikazi na
wakati huo Bi Sharifa na mumewe Mzee Yusuf Kalala walikuwa wanafanyakazi
Washington DC.
Katika kumbukumbu zangu, mara zote nilipokwenda Washington DC ziara
yangu inakuwa haijakamilika iwapo sijaenda nyumbani kwa Mzee Kalala ambapo mara
kadhaa Mzee Kalala mwenyewe alikuwa ananifuata Baltimore Washington International (BWI) au International Airport Dulles (IAD) ambavyo ni viwanja vya ndege
vinavyotumiwa sana na abiria wa Washington.
Marehemu Bi Sharifa pamoja na mumewe Mzee
Yusuf Mtingwa Kalala ni watu wenye ukarimu usio na mfano. Nyumba yao ilikuwa
nyumba ya Watanzania ambayo milango yake ilikuwa wazi muda wote kwa watu wa
aina zote. Kama zilivyo familia nyingi za Marekani, familia ya Mzee Kalala haikuwa
na mtumishi wa ndani.
Mkewe Bi Sharifa alikuwa anafanyakazi Benki ya Dunia na
akirudi nyumbani jioni anakuta kundi la wageni nyumbani kwake. Bila kujali
uchovu, Bi Sharifa huwapokea kwa bashasha na kuingia jikoni kuanza kupikia
wageni. Wakati mwingine, mara tu baada ya kumaliza kula, kundi lingine la
wageni huwa linaingia na Bi Sharifa anaingia tena jikoni. Hayo yalikuwa ni
maisha yao ya kila siku. Bi Sharifa alikuwa akiyafanya hayo kwa furaha ambayo
ilidhihiri kwa watu wote kiasi cha kuwafanya wajione wapo nyumbani.
Yapo mengi sana mazuri ambayo Bi Sharifa na
mumewe Mzee Kalala wameyafanya katika kusaidia jamii ya Watanzania. Nakumbuka katikati
ya miaka ya 1990s Bi Sharifa na Mzee Kalala walianzisha utaratibu wa kuwasaidia
vijana wa Kitanzania kwenda kusoma Marekani. Chini ya mpango huo, vijana hao
walikuwa wanakwenda kuanza masomo kwenye
Community Colleges kwa sababu ada ya masomo zilikuwa chini sana
ukilinganisha na ada za vyuo vikuu.
Walipofika Marekani, vijana hao walikuwa
wanafikia kwenye nyumba ya Bi Sharifa na Mzee Kalala hadi watakapoweza kujikimu
na kupata makazi yao ya kudumu. Vijana wengi sana wamenufaika na mpango huu na
wamesoma hadi kupata shahada za Chuo Kikuu huko Marekani. Baadhi yao wamerudi
nyumbani na wengine hadi leo wanaishi Marekani na wanafanyakazi kwenye
makampuni makubwa kwenye fani mbalimbali kama vile Wahasibu, Wahandisi,
Wanasheria nk. Baadhi yao leo wanamiliki kampuni zao binafsi Marekani na
zinafanya vizuri sana. Msingi wa yote haya ni mapenzi na ukarimu mkubwa uliooneshwa
na marehemu Bi Sharifa na mumewe Mzee Yusuf Kalala.
Miongoni mwa sifa zake kubwa Bi Sharifa ni
kutokuwa na kinyongo na mtu hata pale ambapo utamkosea. Nakumbuka vyema mwezi
Januari 2001 kuna kijana mmoja alikwenda Marekani na kama ilivyokuwa kwa wengi
waliotangulia kabla yake, nae alifikia nyumbani kwa Bi Sharifa. Baada ya miezi
minne tu yule kijana akapata marafiki Uingereza ambao walimshawishi aende huko
kwa kuambiwa kuwa kuna fursa nyingi zaidi kuliko Marekani. Kwa bahati mbaya
sana yule kijana aliondoka bila kuwaaga wenyeji wake ambao walipata taharuiki
sana waliporudi nyumbani na kuona kijana ameondoka bila kuacha taarifa yoyote.
Siku ya pili tu baada ya kuondoka Marekani,
nilipata taarifa kuwa yule kijana amehamia Uingereza na ameondoka bila kuaga.
Bila kusita nilimpigia simu Bi Sharifa na kumtaka radhi sana kwa yaliyotokea.
Jibu lake lilinituliza sana moyo wangu na kuona kuwa Bi Sharifa alikuwa na moyo
wa pekee kabisa. Kwa kifupi tu aliniambia “Bwana Dau (kama alivyozoea kuniita),
fulani (kamtaja jina) ni kijana mdogo sana. Amefanya makosa na katika maisha
yake ataendelea kufanya makosa. Wajibu wetu sisi kama wazazi ni kumsamehe na
kumuongoza, haifai kabisa kumkasirikia”. Huyo ndio Bi Sharifa!
Binafsi nimeumizwa sana na msiba huu kwa sababu
Bi Sharifa alikuwa mzungumzaji wangu sana. Kila niendapo Marekani lazima nifike
nyumbani kwao kuwatembelea na mara nyingi hulala hapo hapo. Mke wangu ameshakwenda
Marekani mara kadhaa na mara zote amefikia nyumbani kwa Bi Sharifa. Walipoamua
kurudi Tanzania zaidi ya miaka 10 iliyopita, mara nyingi tumekuwa
tukitembeleana.
Pamoja na ukarimu wake mkubwa, Bi Sharifa atakumbukwa kwa
ucheshi wake usio kifani. Katika mazungumzo yetu, mara kwa mara nimekuwa
nikimtania kuwa amruhusu mumewe aoe mke wa pili ili bi mdogo amsaidie kazi ya
kumlea Mzee Kalala. Kwa kusisitisa suala hili, nimekuwa namkumbusha ule wimbo maarufu
wa taarabu kuhusu ukewenza ulioimbwa na Sami
Haji Dau na Bi Mwapombe na haswa pale Sami Haji Dau aliposema “ukewenza ndio wenye maliwaza, kazi na
mwenzio atakupokeza”. Siku zote jibu
la Bi Sharifa lilikuwa “jambo zuri kama hili bora uanze wewe Bwana Dau”. Baada
ya jibu hilo tunaishia kucheka!
Kifo ni siri kubwa sana ambayo Mwenyezi
Mungu Ameiweka. Aidha maisha baada ya kufa ni siri kubwa zaidi ambayo hakuna
mwanadamu anaejua. Hata hivyo katika mafunzo Yake, Bwana Mtume (SAW) Anatumbia
kuwa binaadamu wenyewe ndio mashahidi wakubwa wa hatma ya mtu anapokwenda baada
kifo.
Iwapo mtu ameishi vizuri na binaadamu wenziwe, hao binaadamu wenziwe ndio
mashahidi wa wema aliyoyafanya. Kwa wale waliotenda mabaya wakati wa uhai wao,
binaadamu kuwa mashahidi wa hayo. Kwa sisi tuliomfahamu Bi Sharifa, tunashuhudia
kuwa wakati wote wa uhai wake aliwafanyia wema watu wengi ambao kwa kupitia
wema wake, leo wamepata msingi mzuri wa maisha. Pamoja ya kuwa hakuna binaadamu
mwenye haki ya kuhukumu hatma ya binaadamu mwenziwe baada ya kufa, lakini sisi
ambao tumeamiliana na Bi Sharifa, tuna dhana
njema kuwa amepata mapokezi mema huko Barzaq.
Dhana hii
inathibitishwa na kauli ya Bwana Nassor Basalama ambaye alimuuguza Bi
Sharifa kwa kuwa nae muda wote mpaka alipoaga dunia. Kwa maneno ya Bwana
Nassor, siku za mwisho za uhai wake, Bi Sharifa alikuwa katika hali mbaya sana
kiasi ambacho muda wote alikuwa amefumba macho. Kwa muda wote huo Bwana Nassor
alikuwa hospitali na kumsomea visomo mbalimbali ikiwemo Sura Yassin na Swalat Naria
huku akiwa amemshika mkono. Hata hivyo muda mchache kabla hajaaga dunia kwa
mara ya kwanza Bi Sharifa alikunjua mkono wake na akawa anaupigapiga (tap)
mkono wa Bwana Nassor kumpa ishara kuwa amtazame.
Alipomtazama usoni, akamuona
Bi Sharifa akiwa na tabasamu kubwa sana kisha akamwambia kwa sauti ya chini
kuwa “nimefurahi sana kukuona”. Muda mchache baadae alifariki dunia saa 8
dakika 32 mchana akiwa amezunguukwa na mumewe wa zaidi ya miaka 40 Mzee Yusuf
Kalala, binti zake wawili Bi Farida na Bi Rahima, wadogo zake wawili Bi Zahra
na Bi Shekha wote wakiwa na waume zao. Kwa mujibu wa Bwana Nassor, Bi Sharifa
ameiaga dunia huku akiwa na utulivu na tabasamu kubwa usoni mwake. Alifariki akiwa
hana hofu wala huzuni. Na hizo ndizo sifa za watu wema wakati wanakata roho kama
Alivyosema Mwenyezi Mungu kwenye Quran
Sura ya 41 Aya 30:
Hakika
waliosema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu, Kisha wakadumu katika waliloliamini,
hao huwateremkia Malaika (wakati wa kukata roho) wakawaambia: msiogope, wala
msihuzunike; furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Azithibitishe
amali za Bi Sharifa, Ampe Makaazi Mema Peponi na Amuongezee Ucheshi wake
aliokuwa nao hapa duniani awe nao katika Barzaq na siku ya Hesabu. Tunamwomba
Mwenyezi Mungu Atupe sisi wafiwa subira njema.
Aaaamin, Yaa Rab!
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...