Na Mwandishi Wetu, Michuzi Globu ya jami
SPIKA wa Bunge Job Ndugai ameziomba  taasisi za dini pamoja na viongozi wakuu wa dini zote kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI huku akitoa rai ya kuondoa unyanyapaa kwa wanaoishi na virusi vya UKIMWI.

Ametoa ombi hilo jijini Arusha wakati akifungua mkutano maalum ulioandaliwa na ofisi yake kupitia NACOPHA chini ya mradi wa Hebu Tuyajenge unaofadhiliwa na USAID kutoka kwa watu wa Marekani. Mutano huo ulihusisha Taasisi na viongozi wakuu wa dini nchini, TACAIDS pamoja na wadau mbalimbali wanaoshughulikia maswala ya VVU,  kwa lengo la kuweka mkakati wa pamoja wa kujadili na kuona njia sahihi  zinazoweza kutumika kukabiliana na maambukizi ya ya Virusi vya UKIMWI.

Akizungumza zaidi wakati wa mkutano huo Spika Ndugai amewaambia viongozi wa dini na wadau wengine kuwa  zipo sababu nyingi   zinazorudisha nyuma mwitikio wa juhudi za kutokomeza maambuki ya VVU ikiwemo ya  unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya wanaoishi na virusi vya ugonjwa huo nchini.

Hivyo ametoa mwito kwa viongozi wa dini nchini kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na changamoto hizo huku akieleza kuwa wao Bunge nalo chini ya  ushauri wa wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya masuala ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Dawa za Kulevya inayoongozwa na Oscar Mukasa(Mb) na kwa kushirikiana na wadau mbali itahakikisha inafikia malengo ya 95-95-95.

Ndugai amefafanua asilimia 95 ya watu wawe wanatambua hali zao za maambukizi na asilimia 95 wawe wanatumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI na asilimia 95 ya walio katika dawa wawe na kiwango cha chini cha Virusi vya UKIMWI ifikapo mwaka 2030 na kwamba moja ya mambo makubwa kabisa yanayokwaza ni unyanyapaa kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI lakini pia hiyo inasababisha wapimaji kupungua sana. 

"Tumeona tushirikiane nanyi viongozi wa dini ili kuondokana na tatizo hili kubwa la unyanyapaa,Katika ushirikiano wetu, Bunge tutatekeleza wajibu wetu wa kutunga sheria dhidi ya unyanyapaa, tutaishauri Serikali hatua madhubuti za kuchukua dhidi ya unyanyapaa na pia tutakuwa tukiomba kutoka Serikalini taarifa za utekelezaji ili zitusaidie wote kujua tulipo na tunapoelekea katika kufanikiwa kutokomeza unyanyapaa na hili linawezekana tukifanya kazi kwa pamoja,"amesema Ndugai

Ameongeza mkutano huo kwa kiasi kikubwa ni wa kujiandaa na mkutano mkubwa utakaofanya Dodoma Machi ambao utashirikisha wabunge wote, viongozi wa dini na kwa upande mwingine uwakilishi wa juu kabisa wa Serikali ili kuwakabidhi yale ambayo utatoa maazimio yao na kisha yafanyiwe kazi.

 Amesema siku hiyo itakuwa ni mjumuiko mkubwa utakaoshirikisha viongozi wengine kutoka nje ya nchi ambao watatoa ushuhuda wa kadhia hii ya unyanyapaa, tutakuwa na Wabunge, Majaji na Viongozi wa Dini.

Amesisitiza kwamba vingozi wa dini wana nafasi kubwa katika kuvunja ukimya,kuonesha na kuamsha huruma; kuwafariji waliokata tamaa na kufungua fursa ya msamaha na kutoa matumaini mapya.Pia viongozi wa dini wana uwezo wa kubadili mawazo na mitazamo hasi na kujenga jamii yenye mtazamo mpya na kwambaTaasisi za dini zina uzoefu wa kutoa huduma bora, rafiki na zenye kufikika na wengi.

Hivyo amesema  taasisi za dini zina vyombo na mifumo imara ya kupashana habari zinazoaminika kwa urahisi na jamii,na Viongozi wa dini wanasikilizwa, wanaaminika na wanaheshimika sana na kwamba zaidi ya asilimia 90 ya watanzania ni waumini wa dini na wanashiriki kwa hiari bila kushurutishwa na hivyo ni rahisi kufikisha ujumbe ukafanyiwa kazi.

"Kimsingi sisi kama wawakilishi wa wananchi tunaguswa sana changamoto za mwitikio wa jamii katika maambukizi ya virusi vya UKIMWI, ni miaka 37 sasa tunaendelea na kasi ndogo ya mwitikio. Ziko sababu nyingi ambazo zinarudishanyuma mwitikio wa juhudi za kutokomeza maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Awali Afisa Mtendaji Mkuu wa NACOPHA, Deogratius Rutatwa amesema viongozi wakuu wa dini ambao wameshiriki mkutano huo wapo tayari kupokea na kuyafanyia kazi yote ambayo yameelezwa mkutanoni huo.
 Rutatwa ameeleza wazi wao kwa nafasi yao kama wadau katika mapambano dhidi ya UKIMWI wamekuwa wakikutana kwa kufanya mikutano mbalimbali yenye lengo la kuona jamii ya Watanzania inakuwa salama na hakuna maambukizi mapya ya ugonjwa huo na kwa wale ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI wanaishi bila kunyanyapaliwa na yoyote.
  Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo(kulia) akisalimiana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NACOPHA wakati wa mkutano wa wadau wakiwamo viongozi wakuu wa dini nchini waliokutana kujadili na kuweka mkakati wa kupambana na maambukizi mapya ya UKIMWI na kukomesha unyanyapaa. Kati kati ni Spika wa Bunge Job Ndugai.
Spika Job  Ndugai akiwa na baadhi ya viongozi wa dini wakijadiliana jambo wakati wa mkutano wa kujadili namna ya kukomesha unyanyapaa kwa watu wanaoshi na VVU.
 Spika wa Bunge Job Ndugai( wa tatu kushoto) akiwa na viongozi wakuu wa dini wakati wa mkutano wa kujadili namna bora ya kukabiliana na maambukizi ya UKIMWI na kukomesha unyanyapaa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...