Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani
Manya akisafisha mikono kwa kutumia kitakasa
mikono Makao Makuu ya Tume ya Madini jijini
Dodoma tarehe 20 Machi, 2020
|
Na Greyson Mwase, Dodoma
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya amesema kuwa Tume ya
Madini Makao Makuu pamoja na Ofisi zilizopo chini yake zimejipanga katika kukabiliana
na maambukizi ya virusi vya korona.
Akizungumza jijini Dodoma leo tarehe 20 Machi, 2020 amesema kuwa hatua hiyo ni
sehemu utekelezaji wa wito wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu na Miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) wa kuchukua hatua mbalimbali
za tahadhari ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya COVID 19 vinavyosababisha homa
ya korona.
Alisema tayari Ofisi ya Tume ya Madini imeweka vitakasa mikono pamoja na maji tiririka
kwenye ofisi zake lengo likiwa ni kuwakinga watumishi wake na wadau wa madini
wanaotembelea ofisi hizo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali na maambukizi ya
korona.
Aliongeza kuwa, Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa zimeweka vitakasa mikono na
maji tiririka na kuwataka wadau wa madini wanaotembelea ofisi hizo kuanza kuvitumia
ili kujikinga na maambukizi hayo.
Alisema hatua zilizochukuliwa na Tume Makao Makuu na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi
wa Mikoa katika kuzuia kusambaa kwa virusi vya COVID 19 vinavyosababisha homa ya
Korona ni pamoja na kuepuka msongamano, kunawa mikono vizuri kwa maji safi titirika
na sabuni, au maji yenye dawa, kutumia vitakasa mikono, kutumia vikinga pua na
mdomo (masks), kuepuka kugusana, kukaa mbali na mtu mwenye dalili za mafua na
mwenye historia ya kusafiri katika nchi zenye mlipuko wa ugonjwa huo.
Katika hatua nyingine Profesa Manya aliwataka wachimbaji wa madini kuepuka
mikutano isiyo ya lazima na kuepuka misongamano ikiwa ni pamoja na kufuata
maelekezo mengine yanayotolewa na Serikali.
“Ikumbukwe kuwa hadi sasa hakuna tiba au chanjo dhidi ya virusi vya korona lakini kwa
sababu virusi hivyo vinaleta dalili mfano wa zile za mafua makali, mchanganyiko wa tiba
unatumika kupunguza athari za virusi vya korona, hivyo wachimbaji wa madini
wanatakiwa kuchukua tahadhari kubwa kwenye shughuli zao cha utafutaji na uchimbaji
wa madini.” alisema Profesa Manya
Aidha katika hatua nyingine, Profesa Manya amewataka Maafisa Madini Wakazi wa
Mikoa kuhakikisha wanapunguza msongamano wa watu pamoja na kuweka maji tiririka
na vitakasa mikono kwenye masoko yote ya madini na vituo vya ununuzi wa madini
nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...