Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akitoa taarifa ya miaka minne ya uzalishaji wa zao la Korosho nchini ambapo amebainisha kuwa uzalishaji umeongezeka maradufu. 
(Picha Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo
WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga (Mb) ametoa taarifa ya uzalishaji wa zao la Korosho katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli ambapo amebainisha kuwa uzalishaji wa korosho umefikia Tani 1,036,698

Waziri Hasunga amesema kuwa kiasi hicho kimepelekea serikali kuingiza zaidi ya Trilioni 3.3 na fedha za kigeni zaidi ya Dola Milioni 1139 za Marekani kwa kipindi cha miaka mitatu (2017-2019) hivyo zao hilo kuongoza kwa uzalishaji kuliko mazao yote nchini.

Katika kutekeleza sera ya Viwanda ya serikali ya awamu ya tano Waziri Hasunga amesema kuwa viwanda vya kubangua korosho vimeongezeka kufikia 30 kutoka viwanda 21.

Kadhalika katika taarifa hiyo ameeleza kuwa uzalishaji wa korosho nchini umeongezeka kwani mpaka sasa jumla ya mikoa 20 inazalisha korosho ukilinganisha na mikoa mitano pekee kabla ya serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani.

Watanzania wengi wamehamasika na kilimo hicho ambapo mikoa hiyo imeamua kujishughulisha na zao hilo kutokana na umuhimu wake katika mapato ya wakulima na watanzania kwa ujumla wake.

Kwa mujibu wa Waziri Hasunga amesema kuwa Takribani watanzania wanaokadiriwa kuwa 1,200,000 mpaka 1,600,000 wameajiriwa katika zao hilo jambo ambalo limewanufaisha na kuweza kujipatia kipato chao.

Hata hivyo amesema kuwa Mafanikio hayo yametokana na namna ambavyo serikali imetoa elimu kwa kina kuhusu namna bora ya kutumia viuatilifu, kuongeza uzalishaji na Tija, kadhalika uwekezaji katika eneo la utafiti kupitia kituo cha Taasisi ya Utafiti wa kilimo cha Korosho cha Naliendele kilichopo Mkoani Mtwara.

Amesema kuwa kituo hicho kimefanya kazi kubwa na nzuri ya kuhakikisha kuwa wakulima wanapata miche bora ya mikorosho, yenye uwezo wa kuongeza uzalishaji, zenye uwezo wa kustahimili ukame, na zenye uwezo wa kukinzana na magonjwa mbalimbali hivyo kuwa kitovu cha uzalishaji wa miche ya mikorosho nchini.

Waziri Hasunga amesema kuwa katika kipindi hicho ubora wa korosho umeimrika hivyo kupelekea Korosho ya Tanzania kupendwa na kuvutia wanunuzi wengi Duniani.

Kuhusu sekta ya Ushirika, Waziri Hasunga amesema kuwa sekta hiyo imekuwa muhimu kwa watanzania kwani manufaa ya zao la korosho yanatokana na uwepo wa ushirika hivyo ushirika huo utaendelea kuimarishwa ili kuwa na mafanikio makubwa zaidi katika sekta hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...