Na Said Mwishehe,Michuzi TV
KAMISHNA wa Uhifadhi wa Misitu Tanzania kutoka Wakala wa Huduma za Misitu nchini(TFS) Profesa Dos Santos Silayo amewakumbusha Watanzania wote kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kutunza mazingira ili yaweze kuendelea kutoa huduma zake kama ambavyo tunatarajia ikiwemo ya hewa safi na kuifanya Dunia kusa mahali salama pa kuishi.
Pro.Silayo ameyasema hayo leo wakati akizungumzia Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo hufanyika kila Juni 5 ya kila mwaka ambapo amefafanua kuwa lengo la siku hiyo ni sehemu ya kukumbusha wajibu wetu kama wanadamu kuwa mazingira tunayoishi lazima tuyatunze na Taifa letu linaowajibu wa kuhakikisha mazingira yetu tunayatunza.
"Sisi kama Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) tunawajibu wa kuhifadhi rasilimali za misitu na nyuki na katika kuhifadhi rasilimali hizi tuna amini kabisa ni rasilimali muhimu kwasababu sekta nyingine nyingi zinaitegemea sana sekta ya misitu ili ziweze kuendelea,"amesema Profesa Silayo.
Ametoa mfano kuwa iwe sekta ya nishati, maji , mifugo , kilimo, uvuvi,viwanda pamoja na sekta nyingine nyingi zinategemea kwenye sekta ya misitu ili ziweze kuendelea vema na shughuli zake."Hivyo kupitia maadhimisho ya siku ya mazingira ni nafasi nzuri kuwakumbusha watanzania na wadau wa sekta ya misitu kuendelea kulinda na kutunza misitu, hifadhi pamona na rasilimali zake zote."
Amesisitiza kwa kuwaomba wadau wote wanaojihusisha na sekta ya misitu kuitumia siku ya leo kukumbusha wajibu wao katika misitu ambayo wanaisimamia inaendelea kuwa salama."Misitu yetu lazima endelee kutoa huduma zake za ikolojia kama hewa safi kwa ajili ya afya zetu pamoja na maji lakini zaidi kuwa makazi ya viumbe hai wengine wa porini.
"Na hiyo peke yake inaonesha kwamba mtawanyiko wa baianuai ya mimea yenyewe katika misitu lakini na wanyama kuanzia wale wadogo na wakubwa wanaendelea kupata makazi, kwa hiyo tukiweza kufikia lengo kama taifa tuaamini mchango wetu sasa kama sekta ya misitu kwenye hifadhi na usimamizi wa mazingira kwenye misitu yetu itakuwa imekwenda vizuri,"amefafanua Profesa Silayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...