Na Karama Kenyunko Michuzi TV.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaeleza mawakili katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya kilo 268.50  na utakatishaji wa zaidi ya Sh. Milioni 27 kuwa hivi karibuni shughuli za Mahakama zitarudi kama kawaida,hivyo watakuwa wanapata wasaa wa kuzungumza na wateja wao.

Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi, amesema hayo leo Juni 29, 2020 wakati kesi hiyo inayomkabili Kigogo wa biashara ya dawa za kulevya raia wa Nigeria David Ochuku (38) mkazi wa Masaki na watanzania wawili Isso Lupembe (49) mkazi wa Mbezi Luis na Allistair Mbele (38) mkazi wa Mbezi Kibanda cha Mkaa ilipoitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

Imeelezwa kuwa hivi karibuni Mahakama zitarudi katika utaratibu wake wa kawaida na hivyo mtapata wasaa wa kuwa mnaongea na wateja wenu.

Mapema Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika hivyo ameomba tarehe nyingine ya kutwa.

Hata hivyo mawakili wa utetezi wakiongozwa na Wakili Jeremiah Mtobesya alidai ni zaidi ya miezi miwili sasa upelelezi bado haujakamilika na washtakiwa wote wako gerezani."Tunaomba mahakama iwaeleze waharakishe upelelezi kwani haki inayocheleweshwa na haki inayonyimwa."

Aidha mawakili hao waliomba wapatiwe nafasi ya kuongea na wateja wao kwani tokea walipokamatwa hajawahi kuongea nao.

Akijibu hoja kuhusu upelelezi Wankyo amesema, kiasi cha dawa kinachodaiwa kisafirishwa ni kingi na upelelezi unahusisha ndani na nje ya nchi hivyo hauwezi kukamilika kwa haraka ila muda utakapofika wataeleza juu ya hali ya upelelezi.

Awali ilidaiwa Aprili 15, mwaka huu maeneo ya Mbezi Kibanda cha Mkaa eneo ambalo lipo katika wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao kwa pamoja walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa Kilogramu 286.50.

Pia inadaiwa, kati ya Januari Mosi, 2016 na Aprili 15,2020 katika maeneo tofauti ndani ya Jiji la Dar es Salaam washitakiwa hao walijihusisha na miamala ya fedha kiasi cha Dola za Marekani 61,500 na Shilingi za kitanzania 17,835,000, huku wakifahamu kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la usafirishaji wa dawa za kulevya.Washtakiwa wote wamerudishwa rumande.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...