Na Karama Kenyunko Michuzi TV,  
ALIYEKUWA Rais wa Kampuni ya Acacia, Deodatus Mwanyika na wenzake wamehukumiwa kulipa fidia ya Sh bilioni 1.5 baada ya kukiri mashitaka ya kukwepa kulipa kodi.

Pia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kulipa faini ya Sh milioni 1.5 1 ama kutumikia kifungo cha miezi minne gerezani iwapo watashindwa kulipa faini hiyo.


Mbali na Mwanyika washitakiwa wengine ni Meneja Uhusiano wa Mgodi wa Bulyanhulu, Alex Lugendo,  Mkurugenzi mtendaji wa mgodi wa Pongea, North Mara na Bulyanhulu, Assa Mwaipopo ambao tayari wameshalipa fidia hiyo.


Akisoma hukumu hiyo, hakimu mkazi Mwandamizi, Mfawidhi, Godfrey Isaya amesema mahakama imezingatia kwamba washitakiwa wamekiri wenyewe makosa yao ni wakosaji wa mara ya kwanza na wameingia makubaliano hivyo, hakuna sababu ya kuwapa adhabu kali.

Mapema, Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi akisaidiana na wakili wa serikali Mkuu Shadrack Kimaro na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai Juni 16, mwaka huu washitakiwa pamoja na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) waliingia makubaliano ambapo katika mashtaka 39 waliyokuwa wanakabiliawa yameondolewa na wamebakisha shitaka moja.

Katika shtaka hilo wanadaiwa,  kati ya Mei 16,2008 na Desemba 31,2008 katika sehemu tofauti za Jiji la Dar es Salaam, Kahama mkoani Shinyanga na Biharamulo Kagera na maeneo ambayo yapo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  washtakiwa waliwasilisha taarifa ya uongo  kwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa nia ya kukwepa kulipa kodi ya Dola za Marekani 9,309,600 ambayo  iliyopaswa kulipwa kwa TRA.

Washitakiwa wamekiri kutenda makosa hayo na mahakama imewatia hatiani.

Kabla ya kusomwa kwa adhabu, Wakili Kadushi aliieleza mahakama kuwa, hawana kumbukumbu za makosa ya nyuma ya washitakiwa hivyo, ameiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria huku ikizingatia hatua ya makubaliano waliyofikia.

Hata hivyo, wakili wa Utetezi, Alex Mgongolwa akisaidiana na Hudson Ndusyepo alidai mashitaka yanayowakabili washitakiwa yana faini hivyo, aliomba mahakama kutoa adhabu ya faini kuliko kifungo.

Mgongolwa alidai washitakiwa wana wazazi ambao ni wazee na wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali na kwamba wanafamilia changa kwani watoto wao bado wako mashuleni.

Pia alidai washitakiwa tayari wameshalipa fidia ya Sh bilioni 1.5 hivyo, ione huo ni mzigo kwao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...