Mkurugenzi Mkuu wa mashtaka nchini Bw. Biswalo Mganga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Julai 10, 2020 mjini Bariadi katika Ofisi ya Katibu Tawala wa mkoa wa Simiyu, juu ya hatua alizochukua kwa mawakili wawili wa serikali mkoani Simiyu ambao wanatuhumiwa kuwafutia kesi watuhumiwa wa kesi ya mauaji bila kuzingatia taratibu, (kushoto ) ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga.Mkurugenzi Mkuu wa mashtaka nchini Bw. Biswalo Mganga(kulia) akisikiliza maswali kutoka kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) Julai 10, 2020 mjini Bariadi katika Ofisi ya Katibu Tawala wa mkoa wa Simiyu, mara baada ya kuzungumza nao juu ya hatua alizochukua kwa mawakili wawili wa serikali mkoani Simiyu ambao wanatuhumiwa kuwafutia kesi watuhumiwa wa kesi ya mauaji bila kuzingatia taratibu, (kushoto) ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga.

*********************************

Na Stella Kalinga, Simiyu RS

Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka nchini (DPP), Bw. Biswalo Mganga amewasimamisha kufanya kazi za mashtaka mawakili wa Serikali mkoani Simiyu, Amani Kirua na Twahab Yahaya kwa tuhuma za kuwaachia huru watuhumiwa saba wa mauaji ya bibi kikongwe Nchambi Sing’hini mkazi wa kijiji cha Kinamwigulu wilayani Maswa kinyume na taratibu.

DPP ameyasema hayo Julai 10, 2020 mjini Bariadi wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo pia amemuagiza naibu mkurugenzi wa mashitaka kuwachukulia hatua za kinidhamu haraka; huku akibainisha kuwa mawakili hao hawataenda mahakamani wala kupewa majalada ya mashtaka wakati taratibu za kinidhamu zikiendelea.

“Kuanzia leo mawakili hawa nimewasimamisha kufanya kazi za mashtaka yaani hawataenda mahakamani wala hawatapewa jalada lolote,wakati taratibu za kinidhamu zikiendelea, wakati huo huo jeshi la polisi liendelee kuchunguza kujua ukweli juu ya ‘involvement’ (ushiriki) yao, nkama kuna rushwa na mambo mengine yoyote yamefanyika,” alisema DPP Mganga.

Aidha, DPP Mganga amesema yapo maelekezo yanayopaswa kufuatwa na mawakili kabla ya kufuta kesi ambayo ni pamoja na kuandika kwenye jalada sababu zilizofanya kesi ifutwe na mkuu wa mashtaka katika eneo husika kutoa kibali cha kesi kufutwa, ambayo yote yalionekana kutozingatiwa katika ufutaji wa kesi hiyo.

Katika hatua nyingine DPP Mganga amelitaka jeshi la polisi liendelee kuwatafuta watuhumiwa wa mauaji walioachiwa kinyume na taratibu na liwarejeshe mahakamani huku akibainisha kuwa jeshi hilo limeshawakamata watuhumiwa wawili ambao hakuwataja majina kwa sababu za kiupelelezi na watapelekwa mahakamani Julai 13, 2020.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga amesema serikali haitawavumilia watumishi wa umma wanaokiuka taratibu kwa maslahi yao binafsi hivyo itaendelea kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Mmbaga ametoa wito kwa wananchi kuwa na imani na serikali yao na vyombo vyake kwa kuwa mifumo ya serikali ipo na inafanya kazi huku akiwataka kuwa huru kutoa taarifa wakati wowote kupitia vyombo vya ulinzi na usalama.

Mawakili wawili wa Serikali waliosimamishwa kufanya kazi za mashtaka mkoani Simiyu wanatuhumiwa kuwafutia watuhumiwa saba kesi ya mauaji namba moja ya mwaka 2019 ya mauaji ya bibi kikongwe Nchambi Sing’hini, ambapo alibainika kuwa watuhumiwa wawili walifutiwa kesi hiyo Desemba 31, 2019 na wakili Twahab Yahaya na watano walifutiwa kesi hiyo Juni 17 mwaka huu na wakili Amani Kirua kinyume cha taratibu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...