Charles James, Globu ya Jamii
IMEANZA kuboa! Inakera sasa, ni kama imekua kitu rahisi kwa kila mtu kufanya, zamani ilipewa heshima yake ila kwa mwendo huu ni kama imekua danguro, kila mtu anaingia.

Nazungumzia 'Siasa' na hasa Ubunge ambao hivi sasa zoezi la uchukuaji fomu ya kuomba nafasi ya kugombea kwenye vyama mbalimbali linaendelea.

Kila kona ya Nchi hii zoezi la uchukuaji wa fomu linaendelea, hasa kwenye Chama cha Mapinduzi ambapo kunaonekana kumenoga zaidi. Upinzani upepo siyo kama wa mwaka 2015.

Idadi ya wachukuaji fomu imekua kama utitiri, magazeti mengi ya leo yameandika kuwa ni Maafuriko. Ni kusema kwamba wagombea wamekua wengi kuliko wapiga kura.

Tazama hadi muda huu Jimbo la Dodoma Mjini ambalo tena lina Naibu Waziri wa Kazi Ajira na Vijana, Anthony Mavunde mpaka watia nia wamefika 33.

Huko Kawe nasikia wamezidi 30, Bunda, Tarime, Arusha, Moshi Vijijini kote huko kumewaka moto, kila mtu anataka jimbo kila mmoja anatangaza nia, sijui wote tukiwa waheshimiwa nani atakua mwananchi.

Siyo Wanasiasa wenyewe, Wachungaji, Maaskofu, Mashehe, Wasanii, Wanahabari, Wanamitindo wote hao wamejivika mabomu wanataka siasa iwalipukie. 

Swali la kujiuliza ni je kwanini mwaka huu wagombea wamekua wengi kiasi hiki? Na hapa tunapozungumz ni siku ya pili ya uchukuaji fomu, bado siku nyingine mbili. 

Maana yake kuna majimbo wagombea wanaweza kufika hadi 100 na zaidi. Swali ni je siasa imekua nyepesi sana, ajira hakuna mtaani, siasa inalipa ama watu wanatafuta kiki? Ukipata jibu wee kaa nalo tu moyoni mwako.

Wapo watu nawafahamu kabisa uelewa wao wa  siasa ni sifuri, wapo tunaowafahamu uwezo wao wa kuongoza ni zero lakini wote wamekazana kutafuta Ubunge.

Rapa GNako ana rekodi yake inayotamba hivi sasa inaitwa 'Trend Yake' ni kusema kwamba Siasa kwa sasa ndio trend yake. Yaani kila mtu anaona fursa ipo kwenye siasa.

Kuna makundi yanaamini kwamba yanaweza kuongoza wananchi na kuwaletea maendeleo na ndio sababu ya wao kuchukua fomu kwenye vyama vyao kuomba ridhaa ya kugombea.

Wapo waliosoma upepo mwaka 2015 kwamba ukigombea ukatikisa na jina lako kuonekana basi hata ukikosa unaweza kuteuliwa kwenye nafasi za u-RC, u-DC, Ukurugenzi, u-DAS na nafasi zingine za kiteuzi.

Hili ni kundi kubwa sana na ukilitazama kwa kina ni kundi ambalo halina ajira mtaani, wanafunzi na kama wapo wenye ajira ni wachache na wengine wakiwa na ajira zisizoeleweka.

Lipo kundi lingine ambalo lenyewe linatafuta kiki tu kuonekana ni CCM ili waweze kufanya biashara zao kwa amani, kupata tenda mbalimbali serikali kwa sababu walionekana ni wanachama wa chama tawala na waligombea.

Ukweli ni kwamba ukiwatazama wagombea wengi waliotia nia sura zao zinaonesha dhahiri wanayawaza matumbo yao kuliko maisha ya wananchi wa chini waliopo Ngarenanyuki, Butihama na Rungwe.

Wengi wanakimbilia fomu ili wapige picha na kupost kwenye mitandao ya kijamii wakiwa na fomu zao ili tuone fulani aligombea Ubunge.

Kuna watu unawatazama unasema hawa wakienda bungeni ataweza kweli kuisimamia serikali juu ya mikataba mibovu? Ataweza kushauri serikali kuhusu miradi ya maendeleo? Au anataka kwenda kusaini posho tu na kupiga selfie mjengoni?

Nafikiri ni wakati pia wa kutungwa kwa Sheria mpya ya Ubunge. Kile kipengele cha kujua na kusoma peke yake hakitoshi. Lasivyo ipo siku tutajikuta tuna nusu ya wabunge ambao wameenda bungeni kupiga selfie.

Swali la kumalizia mbona upande wa pili kumelala? Au ndo Trendy yake iko Kijani?
0683 015145

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...