TAKUKURU MANYARA YAWAPA ONYO VIONGOZI WA CCM WANAOKATA MAJINA

Na Mwandishi Wetu, Babati

MKUU wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara Holle Joseph Makungu amewaonya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wanaondoa majina ya wapiga kura halali wa kura za maoni na kubandika majina ambayo wanaamini watawapigia kura wagombea ambao wanawataka.

Makungu ameyasema hayo mjini Babati Julai 16 baada ya kupata taarifa kwamba baadhi ya viongozi wa chama hicho tawala ngazi ya kata wamekuwa na mtindo huo jambo ambalo ni kinyume na taratibu.

Amesema wamesambaza makachero wa TAKUKURU kufanya uhakiki wa majina halali kwenye maeneo yanayolalamikiwa.

Amewaambia viongozi wa CCM wanaofanya mabadiliko hayo, wafahamu kuwa hawako juu ya sheria na kwamba kitendo hicho cha kubadilisha majina ya wapiga kura ni kosa la kughushi ambalo likithibitishwa adhabu yake kwa mujibu wa Kifungu cha 337 kanuni ya adhabu  ni miaka saba jela.

"Makosa ya rushwa katika kipindi cha uchaguzi yameanishwa katika vifungu vya 21, 22 na 23 vya sheria ya Gharama za uchaguzi namba 6/2010 ambavyo ni pamoja na hongo ya fedha kwa wapiga kura ili kuwashawishi kupiga au kutopiga kura , ahadi za ajira kwa wapiga kura kwamba nitakuajiri kwenye ofisi fulani, kutoa zawadi, mikopo isiyo na riba au riba iliyo kinyume cha sheria," amesema Makungu.

Amesema makosa hayo pia yanamhusu mpiga kura anayekubali kupokea fedha,zawadi, mikopo, ahadi ya ajira au kitu chochote cha thamani ili ampigie kura au asipige kura kwa mgombea.

Ameongeza kuwa ni kosa pia kutoa vyakula, vinywaji kwa nia ya kushawishi wapiga kura, sheria ambayo inaanza kufanya kazi kuanzia wakati wa mchakato wa wagombea ndani ya vyama vyote vya siasa hadi wakati wa uchaguzi mkuu hapo Oktoba 2020.

Ametoa onyo kwa Viongozi hao wa kata warejeshe majina ya wapiga kura za maoni ambao ni halali mara moja na kuwataka makatibu wa wilaya wa chama cha Mapinduzi kutoa ushirikiano kwa makachero wao wanaoshugulikia uchunguzi huo kubaini wachache wanaotaka kurejesha demokrasia nyuma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...