Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Mkutano wa
Viongozi wa Dini Kuelekea Uchaguzi Mkuu na Kuunga Mkono Juhudi za Rais
Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake katika Ustawi wa Amani,
Uzalendo na Kumtanguliza Mungu uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Agosti 17, 2020.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amesema Tanzania imeshika nafasi ya kwanza barani Afrika kwa kufanikiwa
kusambaza umeme nchini kote kwa asilimia 80.
“Leo hii
Tanzania ni ya kwanza barani Afrika kwa kusambaza umeme kote nchini hadi
vijijini na kufikisha asilimia 80. Kuna nchi ngapi barani Afrika, lakini Tanzania
imefanikiwa kuwa ya kwanza. Tumeweza kufikia vijiji 9,112 Tanzania na hadi
Aprili 2020 na tumetumia shilingi trilioni 2.27,” amesema.
Ametoa kauli hiyo
leo mchana (Jumatatu, Agosti 17, 2020) wakati akielezea mafanikio ya Serikali
ya Awamu ya Tano kwenye mkutano wa viongozi wa dini kutoka kamati za amani za
mikoa mbalimbali Tanzania bara na Zanzibar, uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano
cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na
viongozi waliohudhuria mkutano huo uliandaliwa ili kuunga mkono juhudi za Rais
Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake katika ustawi wa amani, uzalendo na
kumtanguliza Mungu, Waziri Mkuu amesema ushirikiano mkubwa wanauonesha kwa
Serikali, umewezesha kufanya mambo mengi ikiwemo kuimarisha huduma za
upatikanaji wa nishati kwa ajili ya ustawi wa Watanzania.
Mbali ya upatikanaji
wa umeme nchini, Waziri Mkuu ameelezea mambo mengine 15 yaliyofanyika kwa ufanisi
mkubwa chini ya uongozi wa Dkt. Magufuli ikiwemo kurejesha nidhamu na uwajibikaji
katika utumishi wa umma; mapambano dhidi ya dawa za kulevya; ulinzi wa
raslimali za Taifa; kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato na kukua kwa uchumi.
Mengine ni
mapambano dhidi ya umaskini na ukosefu wa ajira; ukarabati na ujenzi wa miundombinu
ya afya; maboresho ya elimu; huduma za maji; ujenzi wa bwawa la kufua umeme la
Nyerere, ujenzi wa mradi wa reli kwa kiwango cha kimataifa (SGR); usafiri wa
anga; ujenzi wa meli na bandari na ujenzi wa barabara na madaraja.
Akielezea kuhusu
kuondoa umaskini na ukosefu wa ajira, Waziri Mkuu amesema kupitia sekta kuu za viwanda,
kilimo, biashara, madini, utalii, miundombinu ya kimkakati pamoja na mifumo ya
mikopo nafuu, Serikali imezalisha ajira za kutosha kwa Watanzania.
“Kupitia ujenzi wa viwanda vipya, tumetengeneza jumla ya ajira
zipatazo 482,601 na kupitia
utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya SGR, Stieglers’ Gorge, ujenzi wa shule,
hospitali na ufufuaji wa mashirika yetu tumefanikiwa kutengeneza ajira zipatazo
6,032,299.”
“Tunao
uwezo wa kuhimili ujenzi wa viwanda vipya na nipende kuwahakikishia wenye
mitaji kwamba Tanzania ni mahali salama pa kuwekeza. Tulianza na mazao matano
ya kimkakati lakini sasa tumeyaongeza. Kupitia kilimo tunazalisha mazao ambayo
ni malighafi kwa viwanda vyetu,” amesema.
“Suala
la ajira ni kilio cha wote lakini kila nchi inatumia njia yake kukabliana nayo.
Je tusingekuwa na miradi ya kimkakati kama SGR na Stieglers’ Gorge, hawa watu
milioni sita na zaidi wangekuwa wapi kwa sasa?”
Mapema, akitoa wasilisho la viongozi wa dini, Katibu
wa Kamati ya Amani, Askofu Jackson Sosthenes alisema lengo la mkutano wao ni
kumpongeza Rais Magufuli kwa hatua iliyofikiwa ambayo Tanzania imefikia kabla
ya mwaka 2025, kina miatno kabla ya muda uliopangwa.
“Viongozi
wa Serikali ya awamu ya tano wameweza kufikia matarajio ya wengi na wamekuwa siyo
watu wa maneno mengi. Siri ya yote hayo ni kumtanguliza Mwenyezi Mungu kama
ilivyosemwa kwwenye maandiko matakatifu kwamba mtafuteni kwanza Mungu na
mengine yote mtazidishiwa,” amesema.
Akitoa
tamko la viongozi wa dini, Mwenyekiti wa Kamati ya Amani, Sheikh Alhad Mussa
alisema ujasiri wa Rais Magufuli wa kutozuia ibada na kukata kufungia watu ndani
(lockdown), ulimpendeza Mwenyezi Mungu na akaamua kuifanya Tanzania kuwa nyota
inayong’ara ulimwenguni.
Kuhusu
uchaguzi mkuu ujao, Sheikh Alhad alisema: “Viongozi wa dini hatuko tayari
kushuhudia uvunjifu wa amani ukitendeka nchini. Tunawaomba viongozi wa saisa
wahakikishe wanalinda amani yetu na mshikamano wetu.”
Mufti
na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeiry ambaye alikuwa wa kwanza kutoa
salamu za viongozi wakuu wa dini, alisema mtu mwenye akili anahitaji pointi
ndogo tu kuona kinachofanywa na Rais Magufuli. “Mambo aliyoyafanya Mheshimiwa
Rais kwa nchi yetu hayahitaji kufikiri sana kwa sababu yako dhahiri. Amefanya kazi
kubwa ndani ya miaka mitano, ambayo yangeweza kufanyika kwa miaka 25.”
Naye
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki
na Pwani, Dkt. Alex Malasusa alisema amani ndiyo msingi wa maendeleo yote. “Amani
ni mtaji wa maendeleo. Ukiwa na fedha lakini kama hakuna amani, haziwezi
kukusaidia chochote.”
“Viashiria
vya ukosefu wa amani hatuvipendi, na tunaviombea vitoweke katika jina la Mungu,”
alisema na kuongeza kuwa viongozi wa siasa watambue kuwa yako maisha wakati wa
uchaguzi na baada ya uchaguzi.
“Sisi
viongozi wa dini tutaendelea kuiombea nchi yetu. Mungu anaipenda sana Tanzania,
na hata tulipopita kwenye bonde la uvuli wa mauti la COVID 19, bado alituvusha.
Tuendelee kumheshimu Mungu, kumtii na tuendelee kumwabudu Mungu,” alisisitiza.
Akizungumza
kwa niaba ya Mufti wa Zanzibar, Sheikh Nooman Jongo alisema zamani Tanzania iliathiriwa
sana mambo matatu ya udini, ukabila na uchama lakini kwa sasa hayapo. “Ukiwa Mkristo
au Muislamu unapaswa utambue kuwa sisi sote ni ndugu wa baba mmoja, ambaye ni
Ibrahimu. Tuangalie amani na upendo na yaliyofanywa na Rais John Pombe Magufuli
hayahitaji tochi ili uyaone,” alisema.
Naye
Askofu Michael Hafidhi wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Zanzibar aliwataka
viongozi wa vyama vya siasa waache kuwasema wenzao vibaya na kutumia majina ya
maaskofu na sheikh kwa manufaa yao binafsi.
“Zamani
tulikuwa na siasa chafu, siasa za majitaka. Je sasa hivi zinatoka wapi? Tafadhali
tusirudi tena kule nyuma. Wako baadhi ya viongozi wa siasa, wakipanda majukwani
wanawasema wenzao, waache mara moja.”
“Tena
kuna wanatumia majina ya Masheikh na Maaskofu vibaya. Msitufanyie reference katika
majukwaa yenu kwa sababu sisi tunafanyiwa reference na Mwenyezi Mungu. Wakiendele
kututumia, wajue tunahesabu zao siku,” alisema.
Naye
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Amani, Mchg. George Fupe alisema wanatoa tamko
kwa wagombea wote watakaoenda kujinadi kwenye kampeni ili kutunza amani ya nchi
ya Tanzania.
“Tamko
letu kwa wagombea wote, lina mambo matatu: Tunawataka wamtangulize Mungu katika
utendaji wao, pili watumie busara na hekima wawapo na tatu wazingatie utu wema.”



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...