Karama Kenyunko, Michuzi TV     

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeridhia Mkurugenzi wa Kampuni ya Jandu Constructions and Plumber Ltd, Khairoon Jandu kutoka gerezani na kwenda kuhojiwa katika kituo cha polisi kwa siku tano.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu Casian Matembele leo Septemba 23, 2020 baada ya upande wa Jamuhuri kuomba kwenda kumuhoji mshtakiwa huyo 

Mapema leo asubuhi wakili wa serikali Mwandamizi Wankyo Simon aliomba mahakama, mshtakiwa Khairoon arejeshwe polisi kwa mahojiano kwenye kesi zingine ambazo bado zinapelelezwa.

"Mheshimwa tunaomba mshtakiwa arejeshwe polisi akahojiwe kwenye kesi zingine mbali na hii, na atahojiwa kwa siku tano na kukabidhiwa tena mahakamani hapa Jumatatu Septemba 28,2020," amesema Wankyo.

Mbali na Khairoon ambaye ni mke wa marehemu Jandu, washtakiwa wengine ni, Zainabu Tharia binti yake, Wakili Mohamed Majaliwa na Meneja wa benki ya Stanbic Ibrahim Sangawe.

Katika kesi ya msingi inadaiwa, katika muda tofauti kati ya Januari na Juni, 2020 katika jiji na Mkoa wa Dar es Salaam washtakiwa wote kwa pamoja kwa kudhamilia waliunda genge la uhalifu,  kwa lengo la kughushi na kuiba fedha.

Katika shtaka la pili  imedaiwa, Januari 16, 2017 katika jiji na Mkoa wa Dar es Salaam washtakiwa khairoon Jandu, Majaliwa na Sangawe walighushi saini ya Inderjit Jandu katika nyaraka zilizoonesha kuwa ni nyaraka halali za kikao cha Kampuni ya Jandu huku wakijua si kweli. 

Aliendelea kudai katika kosa la tatu washtakiwa hao kasoro Zainabu walighushi saini ya Inderjit Jandu katika nyaraka za kampuni zinazoonesha amechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo akionesha ni nyaraka halali huku akijua si kweli.

Washtakiwa hao pia wanadaiwa Mei 25, 2019 katika jiji na Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa na nia ya udanganyifu walighushi saini ya Inderjit Jandu wakionesha kuwa amehamishia hisa za kampuni kwa Khairoon huku wakijua si kweli.

Shtaka jingine la kughushi linalomkabili Khairoon ni la nyaraka za wosia ulioandikwa na Inderjit akionesha ni wosia halali huku akijua si kweli.

Ngukah aliendelea kudai kuwa katika shtaka la sita, saba na nane Khairoon alitoa nyaraka za uongo kwa BRELA zilizoonesha kuwa ni nyaraka halali za vikao vya kampuni ya Jandu zilizoonesha kuwa amechaguliwa kuwa Mkurugezi wa kampuni hiyo na pia amehamishiwa hisa za kampuni huku akijua kuwa nyaraka hizo si za kweli.

Aidha katika shtaka la tisa washtakiwa wote wanadaiwa  katika tarehe tofauti mwaka 2020 waliiba Sh 1,033,860,100 mali ya Kampuni ya Jandu Constructions and Plumber. 

Mshtakiwa Sangawe pia anadaiwa kati ya mwaka 2019 na 2020 akiwa ameajiriwa kama meneja wa benki ya Stanbic alishindwa kutumia mbinu zote kuzuia wizi wa kiasi hicho cha fedha kilichokuwa kimehifadhiwa katika benki hiyo.

Katika kosa la mwisho la utakatishaji inadaiwa katika ya Januari  2019 na Juni 2020 jijini Dar es Salaam washtakiwa wote kwa pamoja walijipatia  kiasi cha Sh 1,033,860,100 mali ya Kampuni ya Jandu Construction huku wakijua kuwa fedha ni zao la kosa tangulizi la wizi.

Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa shauri hilo bado haujakamili hivyo aliomba tarehe nyingine ha kutajwa.

Hakimu Matembele ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 28,2020.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...