*Aanika mipango yake ya kuwatumikia wananchi wa Ubungo kwa miaka mitano ijayo
*Asisitiza umoja na mshikamano, awataka watanzania kujiepusha na vurugu
Na Said Mwishehe,Michuzi TV
RAIS
wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania ambaye pia ni Mgombea urais kwa
tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu,
Dk.John Magufuli ameagiza kuanzia leo Soko la Ndizi Mabibo maarufu
Mahakama ya ndizi lililopo jijini Dar es Salaam liwe chini ya wananchi
na kwamba wasisumbuliwe na mtu yoyote.
Dk.Magufuli
ametoa maagizo hayo leo mbele ya maelfu ya wananchi wa Wilaya hiyo
Ubungo waliofika kumsikiliza licha mvua kubwa kunyesha na kusababisha
kuwaambia kwa jinsi ambavyo wamejitokeza kwa wingi huo yuko tayari
kuwasikiliza kero inayowasumbua.
"Niko
tayari kusikiliza kero mojawapo ya hapa, nasikia pale Mahakama ya ndizi
kuna kero ambayo inawasumbua.Mahakama ya ndizi mnataka nifanye nini?
Wana mateso gani?
"Kwa
heshima ambayo mmenionesha nataka kuwaeleza wananchi kwa mamlaka
niliyonayo soko hili sasa litabakii chini ya wananchi wa hapo ambao
waendelee kufanya biashara, kama kutakuwa na sheria nyingine za Wizara
ya Ardhi na Sheria zote ambazo ziko chini ya Rais kuanzia hapo patakuwa
chini yao na hawatalipa ushuru bali watalipia kitambulisho mabacho cha
20,000 na asitokee mtu wa kuwasumbua,"amesema Dk.Magufuli.
Kabla
ya kutoa maagizo hayo Rais Magufuli alimuita mgombea ubunge jimbo la
Ubungo Profesa Kitila Mkumbo ili kuelezea kero iliyopo katika soko hilo
la Mahakama ya ndizi ambapo alifafanua soko hilo linashindwa kuendelezwa
kwani kuna mgogoro wa umiliki kati ya wananchi na kiwanda cha Urafiki.
Baada
ya maelezo hayo ndipo Dk.Magufuli akatangaza rasmi soko hilo limerudi
kwa wananchi kuanzia leo hii Oktoba 13 mwaka huu, na mambo ya kiseria
yashughulikiwe haraka.
Pamoja
na maagizo hayo,Dk.Magufuli ametumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi hao
mikakati aliyonayo katika kuwatumikia kwa kipindi cha miaka mitano
ijayo.
Ambapo amesema
kwamba mwaka 2915 alifika mbele ya wananchi hao kuomba kura."Nilikuka
kuomba kura, mimi mnilinipa lakini kwa wabunge mkaninyima,hivyo nilikuwa
na wakati mgumu wa kuleta maendeleo.Maendeleo ambayo tumefanya ni kwa
tabu sana.Nafahamu hata hapa Mburahati kuna barabara za lami.
"Na
miradi hii ambayo tunaifanua ni ya kitaifa, lakini hapa imekwama
kwasababu ya kuwa na wapinzani, na ndio maana hata safari hii aliyekuwa
mbunge wa Kibamba na Ubungo wameshindwa hata kugombea tena maana wanajua
waliwakosea wananchi
"Naomba
mchague wagombea wa CCM , na nasema hivyo sio kwasababu nawachukia
wapinzani, hapana .Siwachukii na maendeleo hayana vyama lakini
maendeleo ya kweli yataletwa na CCM,"amesema Dk.Magufuli.
Ameeleza
jinsi ambavyo Wilaya ya Ubungo imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika
sekta mbalimbali."Tumefanya mambo makubwa ya maendeleo na niwahakikishie
tutaendelea kufanya maendeleo makubwa zaidi kwa wananchi hawa wa Ubungo
na Kibamba."
Kuhusu maji
Dk.Magufuli amesema katika Jiji la Dar es Salaam, Serikali katika miaka
mitano imeweka mkazo katika kutatua changamoto ya uhaba wa maji na sasa
maji yanapatikana maeneo mengi ya jiji hilo.
"Leo
hii hata mikokoteni ya kuuza maj imepungua mtaani, magari ya kubeba
maji leo hii yanatangatanga hayana pakwenda.Nilimchagua Profesa Kitila
Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na amefanya kazi kubwa sana
katika kutatua changamoto ya maji Ubungo,Kibamba na maeneo mengine ya
Jiji la Dar es Slaam.
"Nasikia
kuna watu wanasema kuhusu ukabila wanasema Kitila Mkumbo ni wa
Singida.Tuache mambo ya ukabila ambao Mwalimu Nyerere aliumaliza ,
tuache kuleta ukabila. Hapa katika mkutano wapo wa makabila yote na dini
zote, na ndio Tanzania yetu ilivyo,"amesema Dk.Magufuli.
Ametumia
nafasi hiyo kufafanua Wilaya ya Ubungo na Kibamba pamoja na kuwepo kwa
barabara za lami,bado kunachangamoto ya barabara za lami katika mitaa
kwa kutokuwa na lami, ameomba apelekewe wagombea hao wa wa majimbo hayo
ili afanye kazi ya kujenga barabara hizo na wabunge wa Chama hicho
watapendekeza barabara ambazo wanataka ziwekewe lami na yeye
atatekeleza.
Wakati huo
huo, Dk.Magufuli amesema Wilaya ya Ubungo haina majengo ya halmashauri
na hivyo akichaguliwa tena kuongoza nchi atasimamia kuhakikisha Ubungo
wanakuwa na jeng lao kama ilivyo Wilaya mpya ya Kigamboni ambayo yenyewe
ilishajenga jengo lake.
"Wilaya
ya Kigamboni ni mpya lakini tayari ina majengo yake ya halmashauri ,
wamepata haraka kwasababu walikuwa na wabunge wa CCM na hivyo ilikuwa
rahisi kufanikisha mipango yao ya maendeleo,"amesema Dk.Magufuli.
Kuhusu
ujenzi wa miundombinu, Dk.Magufuli amesema kwamba wapinzani wamekuwa
wakisema daraja la Ubungo waliomba wao, jambo ambalo sio kweli na ni
uongo wa mchana kweupe kwani daraja hilo na mengine yamejengwa na
Serikali ya CCM kwa kutambua umuhimu wake na hasa ya kuondoa foleni
katika majimbo ya Ubungo na Kibamba na maeneo mengine ya Dar es Salaam
na wamefanya hivyo kwa faida ya watanzania wote .
Dk.Magufuli
amesema ili kuleta maendeleo katika jimbo la Ubungo na Kibamba
amewaomba wananchi kuhakikisha wanamchagua Profesa Mkumbo na Jumanne
Mtemvu wa jimbo la Kibamba ili walete maendeleo ya wananchi."Naomba
mniletee hawa vijana wawili, nileteeni wagombea udiwani wa majimbo ya
Ubungo na Kibamba ,tulete maendeleo.
"Nchi
yetu imeibiwa vya kutosha, tumewabana na wakubwa wamenuna,wamekasirika
,hivyo wameamua kutumia vibaraka ili watutoe madarakani,"amesema
Dk.Magufuli na kuwataka Watanzania kuungana katika kuleta maendeleo bila
kujali vyama vyao.
Pamoja
na hayo,Dk.Magufuli amesema siasa isitumike kama kichaka cha
kuwagombanisha Watanzania, kwani wanaotaka kuvuruga nchi wao mambo
yakiharibika watakimbia,hawatakaa hapa."Watakachokifanya ni kuchocheaa
weee halafu wao watakimbia.Msikubali kuiharibu nchi yetu,msiwape kura.
"Nchi
yetu ikisambaratika maadui watatumia nafasi hiyo kuiba rasilimali zetu
.Watanzania naomba niwaambie nchi yetu Tanzania, tumezaliwa Tanzania,
tunaishi Tanzania na tutazikwa Tanzania,hatuna nchi nyingine ya kwenda
zaidi ya hii.Tuitunze na hao ambao wanataka kutugawa na kuharibu amani
ya nchi msiwachague katika uchaguzi mkuu mwaka huu,"amesema Dk.Magufuli.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...