


ZIARA UKAGUZI Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu, Emmy Hudson hii leo ametembelea katika Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa, Wilaya ya Mpanda na Tanganyika Mkoani Katavi kwa lengo la kukagua maendeleo ya utoaji wa huduma za usajili wa vizazi na vifo kama unazingatia na kufuata sheria na taratibu za usajili hususani katika maeneo hayo ya mipakani ambako kuna mwingiliano mkubwa wa wageni kutoka nchi jirani pamoja na utekelezaji wa utoaji huduma hizo kwa njia ya kielekroniki iliyoanzishwa mapema mwaka huu kama sehemu ya maboresho na kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo karibu na wananchi.
Akiwa katika ziara hiyo amefanikiwa kujionea utoaji wa huduma na kuzungumza na watumishi kuhusu kutanguliza uzalendo na uadirifu kwa ustawi na usalama wa Taifa letu huku baadhi ya Wananchi waliojitokeza kupatiwa huduma hizo wakisisitizwa kuhakikisha kila mmoja ndani ya familia au ukoo anasajiliwa na kupatiwa cheti cha kuzaliwa kutokana na umuhimu na uhitaji wakati wa kupatiwa baadhi ya huduma za msingi kama vile Vitambulisho vya Taifa, hati za kusafiria, Matibabu ya bima ya afya, elimu ya msingi na sekondari na mikopo kwa wanafunzi wanaoomba kujiunga na elimu ya juu.
Wakati huo huo wananchi Mkoani Katavi wametakiwa kutumia huduma za usajili wa vizazi na vifo kwa njia ya kielekroniki iliyoanzishwa kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma hizo kwa wakati.
Bi Hudson amesisitiza kuwa lengo la kuanzisha kutoa huduma kwa njia ya kielekroniki ni kumpatia fursa mwananchi wakati akiendelea na shughuli nyingine za ujenzi wa Taifa huku akipatiwa huduma kule kule anakoishi ili kurahisisha muda na gharama za usafiri wakati wa kufuatilia huduma hizo
"Kwa sasa mwananchi anaweza kuomba cheti cha kuzaliwa au kifo akiwa nyumbani kwake na kuonesha sehemu ambayo angependa kuchukulia cheti hicho" alisema Bi Hudson.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Ndugu Sostenes Mayoka amesema kwa sasa wamejipanga kuwahudumia wananchi licha ya changamoto iliyopo ya wahamiaji haram huku akisisitiza watu wasisubiri matukio au vyeti vihitajike ndiyo wafuatilie vyeti vya kuzaliwa.
Kwa sasa umuhimu wa vyeti vya kuzaliwa umeongezeka ambapo watoto wanaojiunga na elimu ya msingi au sekondari wanatakiwa kuwa na vyeti vya kuzaliwa, hati ya kusafiria, vitambulisho vya Taifa pamoja na bima ya afya.
Ziara hiyo inayoendelea inajumuisha mikoa ya nyanda za juu kusini ambapo ni Mikoa ya Mbeya,Rukwa na Katavi lengo likiwa kukagua utekelezaji wa maboresho yanayoendelea katika utoajibwa huduma za wakala pamoja na uzingatiaji wa sheria na taratibu za usajili hasa katika Mikoa hiyo inayopakana na nchi jirani za Zambia, Malawi, Burundi, Congo na Rwanda.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...