Na Mwandishi wetu, Mbulu
MKUU wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Dk Chelestino Mofuga, amezindua shughuli ya usajili na kugawa bila gharama vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.
Dk Mofuga akizungumza wakati wa uzinduzi wa tukio hilo amewataka wananchi wenye watoto wa umri wa chini ya miaka mitano kutumia fursa hiyo ya kupatiwa cheti cha kuzaliwa cha bure.
Amesema shughuli ya utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika wilaya ya Mbulu, zitafanyika kwa ndani ya
siku 12 kwenye vituo husika.
Amesema wananchi wanapaswa kutambua umuhimu wa vyeti vya kuzaliwa kwa kila mtoto
anayezaliwa na kwa kila mtanzania kwani ni kitambulisho cha awali.“Tunamshukuru Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan kwa kusogeza huduma hii karibu na wananchi ambao awali walikuwa wanafuata mjini Mbulu kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya,” amesema Dk Mofuga.
Amesema kwa takribani wiki mbili wananchi wa Mbulu watapatiwa huduma hiyo bure bila kuchangia chochote kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kupatiwa cheti cha kuzaliwa.Amesema baada ya kupata cheti cha kuzaliwa inakuwa rahisi mtoto kujiunga na shule kwa ngazi zote, ajira, elimu ya juu na kitambulisho cha Taifa na cha mpiga kura hivyo ni nyaraka muhimu.Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa wilaya ya Mbulu, wamepongeza hatua hiyo kwani kwa namna moja au nyingine itawarahisishia upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa.
Mkazi wa kijiji cha Murkuchida, Johanes Matle amesema awali iliwalazimu kufuata huduma hiyo zaidi ya kilomita 80 hadi Mbulu mjini ilipo ofisi ya Mkuu wa wilaya ila hivi sasa huduma imewasogelea.
“Tunaishukuru Serikali kwa kweli kwani huduma tunapata bila kuchangia gharama ikiwemo usafiri, yaani unafika na vyeti vya kliniki na kujaziwa taarifa za mtoto kisha unapata cheti,” amesema Matle.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...