WATU watano wanaoishi mkoani Sumbawanga na Katavi wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka matatu ya kukutwa na vipande vinne vya meno ya tembo vyenye thamani ya USD 15,000 ambazo ni sawa na Sh. Milioni 34.6.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon imewataja washtakiwa hao kuwa ni, Craft Kileo (43) mfanyabiashara, mkazi wa Kizwite, Shinyanga, Godfrey Kashuli (42) mkulima, mkazi wa Namanyere, Katavi, Richard Kafwa (43), mkulima mkazi wa Kabunde, Katavi, Moses Zakaria (33) mkulima, mkazi wa Mawiti, Katavi na Benjamin Lushina (33) mkulima, Mkazi wa Mawiti Katavi.
Imedaiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kassian Matembele kuwa Mei 5,2021 huko Ukonga, Wilaya ya Ilala ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam washtakiwa walikutwa na vipande vinne vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 15,000 sawa na Sh. 34,649,250 mali ya Jamhuri wa Muungano Tanzania bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Katika shtaka la pili, linawakabili washtakiwa wote, inadaiwa kati ya Aprili Mosi, 2021 na Mei 5,2021 wakiwa eneo la Katavi na Dar es Salaam walisafirisha vipande vinne vya meno hayo mali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania bila kibali cha Mkurugenzi huyo.
Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka yao, Hakimu Matembele aliwaeleza kuwa hawatatakiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.
Katika suala la dhamana, Hakimu Matembele aliwaeleza kuwa Mahakama hiyo haiwezi kuwapa dhamana kwa sababu sheria inaeleza kuwa thamani ya mali ikizidi Sh.Milioni 10, dhamana inatolewa na Mahakama Kuu, kwa hiyo kama wanataka dhamana wakaombe katika Mahakama hiyo.
Upande wa mashtaka, ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa. Hakimu Matembele ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 8,2021 , washtakiwa wamerudishwa rumande.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...