MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imemaliza mgogoro wa muda mrefu wa Kanisa la Siloam, linalojulikana kama Siloam Ministry International, dhidi ya aliyekuwa mmoja wa Makuhani wa Kanisa hilo, Elisha Eliya Miaka1000 aliyewahi kujulikana kwa jina la Nathaniel Zabulon Rusumo. Kuhani huyu alikuwa amepora mamlaka ya Uongozi wa Kanisa hilo kinyume cha taratibu.

Mgogoro huo ulianza baada ya kifo cha Mwanzilishi na Kiongozi mkuu wa Huduma hiyo, Mtume na Nabii Nduminfoo Zebedayo Munuo, aliyefahamika kwa jina la Eliya Ad2 MunguwaMajeshi ambaye alitwaliwa na Mungu Novemba 16, 2014, ndipo Elisha Eliya Miaka1000 alijipa madaraka ya kumrithi kiongozi huyo bila kufuata utaratibu wa Katiba ya Huduma ya Siloam.

Kutokana na hatua hiyo ya kujipa madaraka hayo, Elisha Eliya Miaka 1000, alisababisha mgawanyiko wa waumini akashawishi baadhi wamuunge mkono ili wapore mali mbalimbali za huduma yakiwemo majengo ya ibada na kuondoka na sadaka kupeleka nyumbani kwake.

Serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Msajili wa Vyama vya Jamii walijaribu kutatua mgogoro huo lakini E.E. Miaka1000 alikataa utengamano.

Kutokana na matukio hayo Bodi ya wa Wadhamini ililazimika kumshtaki Mahakama Kuu ya Tanzania, kupitia kesi ya madai namba 24 ya mwaka 2017.

Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyosomwa na Jaji Leila Mgonya Julai 23, 2021, baada ya kusikiliza kesi hiyo upande mmoja kwani mdaiwa hakufika mahakamani, ilikubaliana na maelezo ya wadai na ikatoa amri walizokuwa wakiziomba. 

Katika hukumu hiyo, Mahakama Kuu ilitoa amri za zuio la kudumu dhidi yake yeye Elisha Eliya Miaka1000, mawakala wake, watumishi wake na mtu yeyote atumikae kwa niaba yake kutokutumia na kutokusajili jina la The Pool of Siloam Church au Kanisa la Siloam mahali popote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia mahakama hiyo iliamuru kuwa Elisha Eliya Miaka1000 kwa kuwa hakuwa kiongozi wa Kikatiba ndani ya Siloam Ministry InternationaI haruhusiwi kufanya shughuli za kiutawala zikiwemo kuwateua au kuajiri makuhani au waumini na kuwahamisha kwa jina la The Pool of Siloam Church.

Vilevile mahakama hiyo ilimwamuru Elisha Eliya Miaka1000 au yeyote anayetumika kwa niaba yake kukabidhi mara  moja, maeneo, viwanja, majengo na mali zote za Siloam Ministry InternationaI walizokuwa wanazitumia kwa jina la Siloam Ministry InternationaI au The Pool of Siloam Church na kulipa gharama zote za kesi hiyo.

Kwa mujibu wa maelezo ya wadai,  Siloam Ministry International (SMI)   ilianzishwa mwaka 2003 na kuongozwa na Mtume na Nabii N.Z Munuo, aliyefahamika pia kwa jina la Eliya Ad2 MunguwaMajeshi.

Huduma hiyo ilisajiliwa na Serikali ya Tanzania, Wizara ya Mambo ya Ndani kwa hati namba SO.12880 iliyotolewa Agosti 9, 2005, ambapo ilieneza Injili ya Yesu Kristo na kujenga makanisa maeneo mbalimbali nchini.

Tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo mwaka 2003 hadi mwanzilishi huyo alipotwaliwa na Mungu Novemba 16, 2014, huduma hiyo ilikuwa imeshakubalika ndani na nje ya nchi, ambapo kazi ilipanuka na kujenga vituo vya huduma katika mikoa mbalimbali nchini.

Kwa muda wote huo kabla ya kutwaliwa kwa mwanzilishi wake, kulikuwa na mshikamano, amani na heshima miongoni mwa waumini na viongozi na hapakuwepo na dalili zozote za uvunjifu amani katika kanda zote Saba za huduma hiyo zilizokuwa zimeanzishwa.

Mwaka 2007 aliingia katika huduma hiyo muumini aitwaye Nathaniel Zabuloni Rusomo ambaye baadae alijulikana kwa jina la Elisha Eliya Miaka1000 akiwa na matatizo mbalimbali ambapo aliombewa na kufunguliwa kisha akajiunga na huduma ya Siloam Bible School ambapo alifundishwa utumishi.

Wakati tayari akiwa kuhani wa kanda ya Dar es Salaam Miaka 1000 alisaliti kiapo cha utumishi, kwani baada ya kiongozi mkuu wa huduma hiyo kutwaliwa na kabla ya mchakato wa kumpata kiongozi mwingine, yeye alijivua safu ya ukuhani na akajipa cheo cha Mzeituni, Mpaka Mafuta, Mzee wa Siku, Wakili wa Mungu, mungu aliyetuma wote, baba wa uzao, baba halisi nk.

Mpaka aliacha kabisa imani aliyoikuta Siloam na aliazimia kupora thamani, uzuri na kibali cha kusanyiko la Siloam akiwa kwenye majengo ya Siloam.

Aliwapindua waumini kwa kuingiza mafundisho yaliyoacha maswali na hadithi za Kanisa Halisi la Mungu baba. E. E. Miaka1000 alitumia mbinu mbalimbali za kuvuruga safu za makuhani mikoani ambapo aliwashawishi waungane naye kusaliti maono ya mwanzilishi wa Huduma.

Ili kuhalalisha mapinduzi  hayo alitunga Katiba yake akitaka kusajili The Pool of Siloam Church lakini haikupitishwa na Serikali kwa kuwa hakuwa mmoja wa viongozi wa Kikatiba. Hivyo, alizalisha mzozo ili Serikali ifute usajili halali wa Siloam Ministry InternationaI.

Hata hivyo hilo nalo halikufanikiwa.

Hivyo yeye na kundi lake la waumini aliofanikiwa kuwashaiwishi katika vituo mbalimbali waliendelea kutumia mali na majengo ya SMI kufanyia ibada na kuondoka na sadaka.

Serikali, viongozi na makuhani waaminifu walijitahidi kunusuru mgogoro huo lakini Miaka 1000 alikataa utengamano kwa madai kuwa yeye ni mungu na hawezi kujadiliwa, kuhojiwa wala kushauriwa.


 

Nathanael Zabron Rusomo, maarufu kama Elisha Eliya Miaka 100 (mdaiwa) aliyeshtakiwa na bodi ya wadhamini ya Siloam Ministry International.









 

 


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...