Na Muhidin Amri,Mbinga
WAZIRI wa madini Dotto Biteko, ametembelea mgodi wa dhahabu wa Lukalasi
katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma unaomilikiwa na mzawa Jonson
Nchimbi na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na mwekezaji huyo.
Waziri Biteko amesema, wizara ya madini itaendelea kumuunga mkono
mwekezaji huyo mzawa katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa
madini.
Kwa mujibu wa Waziri Biteko, katika kipindi kifupi mwekezaji huyo
amechimba dhahabu yenye thamani ya zaidi ya Sh Bilioni 3 na amelipa
zaidi ya Sh milioni 200 kama kodi kwa Serikali.
Amewaomba wananchi wanaofanya kazi katika mgodi huo kufanya kazi kwa
uaminifu na kujiepusha na vitendo vya wizi vinavyoweza kumvunja moyo
mwekezaji huyo mzaliwa wa mkoa wa Ruvuma.
Amesema, haya madini ni nyenzo pekee ambaye Watanzania tumepewa na Mungu
ili tuondoa umaskini wetu,kwa hiyo ni lazima tuchimbe kwa haki,kulipa
kodi na kufuata sheria na taratibu za nchi badala ya kutugombanisha.
Waziri Biteko amesema,kwa kutambua uwekezaji huo, Serikali itaendelea
kumsaidia kwa kumpatia wataalam ili aweze kuchimba dhahabu kisasa na
kumkutanisha na taasisi mbalimbali za fedha ili kupata mikopo.
Amesema, lengo ni kumwezesha kupata vifaa vya kisasa kwa ajili ya
shughuli za uchimbaji wa madini kwa sababu bado ana vifaa vya kizamani.
Amesema, serikali inatambua leseni zote na baadhi bado hazijafanyiwa
kazi na nyingine zimeisha muda wake, hivyo wizara ya madini itazifuta
ili kupewa watu wengine watakaokuwa tayari kuchimba na kuachana na watu
wenye tabia ya kushikilia maeneo bila ya kuyafanyia kazi.
Amesema,uchimbaji wa madini ni safari ndefu na serikali inawahitaji
sana wachimbaji wakubwa na wadogo na kamwe wizara haitaruhusu kuwepo
kwa wachimbaji wakubwa pekee yake kwani inahitaji watu wengi kufanya
utafiti ili kufahamu kiasi cha madini kilichopo katika nchi yetu.
Ameiagiza,ofisi ya Mkuu wa Ruvuma na mkuu wa wilaya Mbinga kuhakikisha
inapitia upya maeneo na leseni zote ambazo hazijaendelezwa ili maeneo
hayo yaweze kupewa vikundi vidogo kwa ajili ya uchimbaji.
Mmiliki wa mgodi huo Jonson Nchimbi amesema,tangu mgodi ulipoanzishwa
wameweza kuzalisha dhahabu yenye thamani ya Sh.bilioni 3,038,167,518.24
na kulipa mrabaha wa Sh.182,290,051.09,ada ya ukaguzi Sh. Milioni
30,381,675.18 pamoja na ushuru wa Halmashauri jumla ya Sh.9,114502.55.
Aidha amesema,mgodi unashiriki shughuli mbalimbali za kijamii na za
maendeleo katika kijiji cha Lukalasi na umetoa ajira kwa wananchi
wasiopungua 300 wanaofanya kazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchimbaji
wa dhahabu juu ya ardhi.
Hata hivyo amesema, kwa kuwa eneo hilo limeanza kujulikana kuwa na
uzalishaji mzuri wa dhahabu kumeanza kutokea migogoro michache ya
kuingiliana katika leseni za uchimbaji na kuishukuru wizara ya madini
kumaliza moja kati ya migogoro hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge amesema,serikali inatambua
uwezo wa mgodi huo katika kuongeza ajira na mapato ya serikali na mapato
binafsi.
Balozi Ibuge,amewataka wananchi wanaishi kuzunguka mgodi huo kutambua
juhudi za uwekezaji na kazi inayofanyika katika mgodi huo ambao tangu
ulipoanzishwa umeshaleta manufaa makubwa.
Hata hivyo,ametaka kufanyiwa kazi tatizo la kushuka kwa uzalishaji wa
dhahabu katika mkoa huo ambapo kwa Mwezi Julai dhahabu iliyopatikana ni
kilo 2,wakati mwezi Juni ilikuwa kilo 4, na Mwezi Mei kilo 5.
Amesema, serikali ya mkoa itaendelea kuunda vikundi vingi na kuwataka
viongozi wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Ruvuma kuhamasisha
wanachama wake kwa kuwa lengo la Serikali ya mkoa ni kutoa ajira na
kuongeza mapato yatokanayo na madini.
Waziri wa Madini Dotto Biteko kushoto na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge kulia,wakimsikiliza jana mmiliki wa mgodi wa dhahabu Lukalasi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Jonson Nchimbi katikati wakati wa ziara ya Waziri wa madini alipotembelea mgodi huo ili kujionea kazi zinafanywa na mwekezaji huyo.,Mmiliki wa mgodi wa dhahabu Lukalasi katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Jonson Nchimbi kulia,akitoa taarifa ya hali ya uzalishaji wa dhahabu kwa Waziri wa Madini Dotto Biteko katikati, aliyetembelea mgodi huo akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma,kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge.
Picha na Muhidin Amri,
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...