CHAMA  Cha  Mapinduzi  (CCM) kimewapongeza Umoja wa Machifu na Watemi kwa kumsimika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaue amesimikwa Uchifu Mkuu wa machifu wote nchini .

Kimemesema kwamba CCM itaendelea kupiga vita  sera za udini, ukanda  na  ukabila lakini kitaendelea kuwatambua,kuwaheshimu ba kuwathamini machifu wote na kubwa zaidi wanawapongeza kwa kumsimika Rais Samia kuwa Chifu Mkuu.

Pia Chama hicho  kimesema pamoja na sera za TANU na baadae CCM kutoruhusu tawala za kichifu na kitemi  hiyo  haina maana koo za kichifu na mchango wao kwa nchi yetu zisitambuliwe.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Shaka Hamdu Shaka ametoa ufafanuzi huo baada ya kuona kuna haja ya kutoa maelezo iwapo Rais Samia kusimikwa uchifu mkuu ni kushabikia ukabila na kueleza wanaokosoa kitendo  hicho wanatakiwa wafanye rejea ya historia kabla ya kusema hayo.

"Hata Rais wa Kwanza Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye ndiye aliyekuwa  mstari wa mbele kupiga vita himaya za kichifu na kukomesha ukabila ili kujenga misingi imara ya umoja wa kitaifa alikuwa akivikwa mavazi ya kimila na kupewa hadhi za uchifu kwenye makabila yote alipokuwa Rais wa nchi yetu.

"Wanaodai kitendo cha Rais Samia kupewa hadhi ya uchifu mkuu wa machifu  wote nchini ni kushabikia ukabila waelewe kuwa hiyo ni hadhi inayotolewa kwa watu muhimu na waliotoa mchango mkubwa kwenye jamii zao kama ile itolewayo na vyuo vikuu duniani kote ikiwemo udaktari wa heshima,"amesema Shaka.

Pia amesema hawatashabikia ukabila, udini wala ukanda lakini muhimu ikafahamika CCM hakitabeza utamaduni, mila na desturi ambazo ni chanya ikiwemo kuutambua utemi, uchifu na viongozi wa mila kwani kufanya hivyo sio kuendeleza ukabila.

Ameongeza  hata baada ya mwalimu Nyerere kukomesha ukabila alionekana akivikwa mavazi  ya kitamaduni na kiasili katika makabila mbalimbali,  mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati mzee Benjamin Mkapa, Dkt Jakaya Kikwete na hayatI Dkt John Magufuli  wote walitunukiwa heshima hizo.

Amesema wapo washindani wao  wa kisiasa na wamekosa hoja basi watakosoa kila kitu ambacho CCM na viongozi wake itafanya." Hata mwanasiasa Theresa Ntare wa kabila la Waha huko Kigoma alitambuliwa kwa heshima yake na akaitwa Mwami Ntare hata baada ya uhuru."

Amesisitiza CCM wakati wote itatambua, itathamini na itaenzi mchango wa machifu na watemi kama vile kina Mangi Meli, Chifu Kimweri wa Usambara, Mtemi Mirambo wa unyanyembe, Makunganya, Kinjikitile Ngwake na  kina chifu Songea, Nkossy na Mkwawa ambao walikuwa mstari wa mbele kupigania uhuru na ukombozi wa Mwafrika dhidi ya wakoloni.

Amesema machifu na watemi wameshiriki juhudi za mapambano kupinga tawala za kijerumani na kiingereza kwa kuwaeleza kinagaubaga waondoke ili wajitawale wenyewe.

"Hatuwezi kuzungumzia uhuru wa Tanganyika au mapinduzi ya  Zanzibar bila kutambua na kuthamini mchango wa machifu, watemi, viongozi wa kijadi na kimila.Ndiyo maana katika kuenzi mchango wao yapo maeneo mengi ya umma yaliyopewa majina yao kama vile kuna mitaa imeitwa Kimweri, Makunganya; shule zinazoitwa Mkwawa, Mirambo" ameeleza Shaka

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...