Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHRC Anna Henga akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu Afrika.


KITUO Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC,) katika kuadhimisha siku ya Haki za Binadamu Afrika imetoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia upya uamuzi wao wa kujiotoa katika katika ibara ya 34 (6) ya mkataba wa nyongeza wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu ambayo ilikuwa inaruhusu mtu au taasisi yoyote  kuifikia Mahakama ya Afrika wanapokuwa na uhitaji wa kudai haki katika Mahakama hiyo ya haki na za binadamu na watu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya maadhimisho ya siku ya Haki za Binadamu Afrika inayoadhimishwa kila Oktoba 21, Mkurugenzi wa kituo hicho Bi. Anna Henga amesema, siku hiyo ni muhimu kwa wapenda haki wote katika nchi za Afrika kwa kuwa Afrika inasherehekea kuanzishwa kwa mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu wa mwaka 1981.

''LHRC inapenda kutumia maadhimisho haya kutoa mwito kwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia upya uamuzi wake wa kujitoa katika mkataba huo kwani itarudisha na kuimarisha heshima ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uwanda wa kikanda.'' Amesema.

Aidha amesema, Tanzania imekuwa nchi ya pili baada ya Rwanda kujitoa katika mkataba huo unaoruhusu mtu au taasisi kufungua kesi dhidi ya Serikali pale ambapo kuna malalamiko ya kuvunjiwa haki yake.

''Kumekuwa na dhana pamoja na tafsiri isiyo sahihi kwamba, Watu kufungua kesi katika mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu sio nia nzuri kwa Serikali na ni kwa lengo la kuichafua, LHRC inapenda kusahihisha dhana na tafsiri hiyo ya kuwa hiyo ni ishara ya kuimarika kwa demokrasia, ufikiaji wa haki, uvumilivu na uongozi bora unaooneshwa na Serikali kwa kuruhusu watu au taasisi kufungua kesi dhidi ya Serikali.'' Amesema.

Aidha amesema, Tanzania bado inaweza kurudi katika mkataba huo na kuruhusu wananchi kuifikia Mahakama hiyo kwa lengo la kuifikia Mahakama na kupata mustakabali wa haki zao na LHRC inaamini muundo wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu iliyopo Arusha hapa nchini inafahamu misingi ya kiafrika, tamaduni, taratibu, sheria pamoja na mazingira hivyo maamuzi yanayotolewa na Mahakama hiyo ni maamuzi ya haki na usawa.

Pia ameishauri Serikali kuendeleza utamaduni wa kuripito hali ya haki za binadamu kwa umoja wa Afrika kupitia mfumo wa Mapitio ya Haki za Binadamu Afrika yaani 'African Peer Review  Mechanism (APRM,)

''Mara ya mwisho ripoti ya mapitio ya hali ya haki za binadamu ilitolewa mwaka 2013 ambapo utekelezaji wake ulianza rasmi 2014, hivyo ni vyema Serikali ikaendeleza utamaduni huo kwa kuwa unaimarisha na kukuza misingi ya haki za binadamu nchini.'' Amesema.

Bi. Anna amesema pamoja na ushauri na mwito kwa Serikali kituo hicho kinatoa mwito kwa taasisi za Serikali hususani jeshi la Polisi na vyombo vya usalama na wananchi kuzingatia haki za binadamu kwa kukuza na kulinda haki za binadamu kwa ngazi zote.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...