Na John Mapepele, WUSM

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe Innocent Bashungwa amesema mwigizaji maarufu duniani kutoka nchini India Sanjay Dutt amekubali kuwasaidia Wasanii wa Tanzania katika maeneo ya kuandaa filamu, vifaa na utaalam ili kutangaza utalii wa Tanzania duniani.

Akizungumza kwenye Mkutano wa kumtambulisha Dutt kwa Waandishi wa Habari na wadau mbalimbali wa Sanaa na Filamu nchini leo Novemba 11, 2021 jijini Dar es Salaam. Mhe, Bashungwa amefafanua kuwa Msanii Dutt amekubali kuleta wataalam ambao watashirikikiana na Bodi ya Filamu, Taasisi ya Chuo cha Sanaa Bagamoyo na Kampuni ya Africable katika kuwasaidia wasanii wa Tanzania katika maeneo mbalimbali.

“Ujio wake ni fursa kwa nchi yetu na kunatusaidia kuendeleza safari ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuitangaza Tanzania kupitia filamu, safari ambayo Mhe. Rais aliianza kupitia maandalizi ya filamu ya Royal Tour” Ameongeza Mhe. Bashungwa

Amesema ujio huu unaashiria kuwa tasnia ya filamu nchini Tanzania, inapitia mabadiliko chanya na makubwa, kiasi kwamba waigizaji wakubwa wa filamu kama Dutt, wanasikia furaha na kutenga muda kutembelea Tanzania na kuwa uwepo wake hapa utakuwa ni fursa kubwa kwa tasnia ya filamu na wadau wote wa filamu nchini.

Aidha, Mhe. Bashungwa ametumia muda huo kumwomba Msanii Sanjay Dutt kutoa vifaa vya kuandaa filamu za kisasa kwa wasanii wasio na uwezo wa kuwa na vifaa hivyo na kwamba vitakuwa vikitunzwa na kusimamiwa na Bodi ya Filamu nchini na Msanii huyo amekubaliana na ombi hilo.

Pia, Mhe. Bashungwa amefafanua kuwa Sanjay Dutt amesema anakusudia kuandaa filamu kubwa ambayo itaisambaza duniani kwa ajili ya kuitangaza Tanzania.

Akizungumza kwenye mkutano huo Msanii Sanjay Dutt amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu kwa ukaribisho ambapo ameahidi kuisaidia Tanzania kuwa katika sura ya dunia kwenye tasnia ya filamu.

Pia ametoa wito kwa Serikali kuwa “film academy” ambayo itasaidia kuandaa fani mbalimbali kama uigizaji na muziki ambapo amekubali kuwaleta wataalam kutoka India kuja kufundisha.

Mhe. Bashungwa amesema Serikali itaendelea kufanya jitihada za kufungua milango ya ushirikiano kwenye tasnia ya filamu kati yake na India.

Ameyataja baadhi ya maeneo muhimu ya ushirikiano kuwa ni pamoja na utayarishaji wa filamu ambapo amefafanua kuwa kuna nafasi kwa wasanii wa filamu kutoka India na Tanzania kushirikiana na kutayarisha filamu kwa pamoja (co-production) kwa kutumia mandhari zinazopatikana nchini.

Amesema sasa ni wakati mwafaka wa kuuonesha ulimwengu mandhari nzuri za Tanzania, ambazo zinaweza kutumika kwa ajili ya kurekodia filamu na kusisitiza kwamba Tanzania imebarikiwa kuwa na maeneo mengi mazuri ya kurekodia filamu, ambayo baadhi yake hadi sasa tayari yamevutia kampuni mbalimbali za filamu, kutoka nje ya nchi kutengeneza filamu kwa kutumia maeneo hayo.

Ametaja baadhi ya filamu na makala za filamu zilizotengenezwa nchini Tanzania, na makampuni za kigeni kuwa ni pamoja na Amazing Race, Criminal Mind, Serengeti, Forces of Nature, the Mating Game, On the Steps of Kuwait Sailor, Tanzania Beyond the Wild, Extreme Treks, Pechino Express, Big Cat, Ben Fogless, the Great African Migration, na Night of the Lotus.

Amelitaja eneo la pili la ushirikiano kuwa ni usambazaji (Uuzaji) wa filamu za kitanzania na amesema kuna haja ya kusambaza filamu zinazozalishwa hapa nchini ili kufikia hadhira kubwa zaidi ambapo ameeleza kuwa kwa sasa Tanzania inazalisha takriban filamu 1,400 kila mwaka, ambazo hutayarishwa kwa lugha ya Kiswahili.

Amesema Kiswahili kinazungumzwa na takriban watu milioni 150 duniani, wakiwemo Diaspora wanaoishi katika nchi mbalimbali za Magharibi, na Mashariki ya mbali ambapo amesisitiza kuwa Filamu za Kiswahili zina uwezo wa kupata soko kubwa, na ameomba ushirikiano wa Kampuni ya Africab katika kutafuta masoko ya filamu za Tanzania duniani.

Pia amesema eneo jingine ni Jumba Changamani la Filamu ambapo amefafanua kuwa kuna fursa ya kuwekeza kwenye kitovu cha shughuli mbalimbali za filamu, ambacho kitakuwa na miundombinu ya kisasa ya utayarishaji wa filamu kama vile studio za utayarishaji, sehemu za kurekodia filamu, na kumbi za sinema ambapo ameongeza kuwa hiyo inaweza kuwa hatua moja kuelekea kuwa tasnia kubwa ya filamu nchini Tanzania, kama Nigeria (Nollywood), India (Bollywood) na USA (Hollywood).

Kupitia mkutano huo Mhe. Bashungwa ametoa wito kwa wasanii wote nchini kujitokeza kwa wingi kesho Novemba 11, 2021 kwenye uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam kwenda kuishangilia timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars) itakayocheza na Timu ya Kongo kwenye mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia 2022.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa nchini, Dkt. Emmanuel Ishengoma amesema Mhe. Rais alipoanzisha mkakati wa kuitangaza Tanzania kupitia filamu ya Royal Tour aliyoiandaa hivi karibuni alikuwa ametoa fursa ya kutafsiri maono hayo ambapo amesema Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Idara ya Sanaa sasa inaunga mkono kwa njia hii ya kushirikiana na wasanii wakubwa duniani kama Sanjay Dutt kwenye eneo la kuandaa filamu zenye kutangaza Tanzania kimataifa.

Naye Msanii Mboto amemshukuru Mhe. Rais kwa kuendelea kumwamini Waziri Bashungwa kusimamia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na kusisitiza kuwa anafanyan kazi nzuri ya kuboresha sekta ya filamu nchini.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Filamu nchini Dkt. Kiagho Kilonzo amemshukuru mwigizaji Dutt kwa kukubali kuigiza na kutokea kwenye filamu za kitanzania ambapo amesema tayari taasisi yake imeshaandaa orodha ya filamu zilizoainishwa ili aweze kuchagua na maeneo kwa ajili ya kuandaa ili kazi iendelee.

Rais wa Shirikisho la Filamu nchini Eliya Mjata amesema Shirikisho linamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa katika tasnia ya filamu nchini

Mkutano huo ulipambwa na kikundi cha wasanii wa ngoma za asili cha kutoka mkoani Mtwara ambacho kiliwavutia wadau mbalimbali waliohudhuria mkutano huo ikiwa ni pamoja na Sanjay Dutt.

“Kwa kweli niseme ukweli ndugu zangu kikundi hiki cha wasanii wa ngoma za asili kimenivutia sana japokuwa sikuwa naelewa maana ya wimbo wao.” Ameshuhudia Sanjay Dutt wakati alipokuwa akitoa hotuba yake kwa waandishi

Picha ya pamoja  baina  ya Mhe. Innocent Bashungwa na Sanjay Dutt  Viongozi mbalimbali  kwenye Sekta Sanaa   na wasanii (waliosimama nyuma)

Mhe. Innocent Bashungwa(kushoto) akimkabidhi zawadi ya Kamusi ya Kiswahili Sanjay Dutt

Mhe. Innocent Bashungwa akizungumza na Waandishi wa Habari

  Wasanii mbalimbali  waliohudhuria  Mkutano wa Sanjay Dutt


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...