Tarehe 30 Novemba, 2021, Mbeya.
Ndugu Wananchi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto imekuwa ikitoa taarifa kwa wananchi kuhusiana na mwenendo wa magonjwa
mbalimbali yakiwemo yale ya milipuko. Taarifa hii imekuwa ikienda sambamba na
taarifa ya hatua zinazostahili kuchukuliwa kwa ajili ya kudhibiti magonjwa hayo. Aidha, wote
tumeshuhudia Dunia ikipambana na mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19 ambapo, nchi
mbalimbali zimeendelea kuchukua hatua za kukabiliana. Hata hivyo, kumekuwa na wimbi la pili na la tatu la mlipuko
wa ugonjwa huo, ambapo nchi nyingi zimeathiriwa ikiwemo Tanzania. Aidha, hivi karibuni kumekuwa na tishio la
wimbi la nne baada ya taarifa kutoka nchi mbalimbali Duniani.
Ndugu Wananchi, hadi kufikia tarehe 29 Novemba, 2021 jumla ya waliothibitika kuwa na
maambukizi Duniani ni 260,867,011 na
vifo 5,200,267 vimetolewa taarifa.
Aidha, tangu kuripotiwa kwa ugonjwa huu hapa nchini Tanzania mnamo tarehe 16
Machi, 2020 hadi 28 Novemba 2021 jumla ya waliothibitika kuwa na maambukizi ni 26,273 na vifo 731 vimetolewa taarifa. Kwa
ujumla baadhi ya nchi Duniani zikiwemo za Afrika zimeanza kuripoti ongezeko la
visa vipya vya UVIKO 19 na hivyo kuleta tishio la kukumbwa na wimbi la nne la
maambukizi ya ugonjwa huo.
Kwa upande mwingine, hivi
karibuni baadhi ya nchi zimeripoti ugunduzi wa anuwai mpya ya kirusi
anayetambulika kwa jina la Omicron (B.1.1.529).
Kama nchi hatuna budi kuendelea kuchukua hatua sahihi za kujikinga. Kwa msingi huu, tunahitaji kuongeza kasi
zaidi ya kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO-19.
Ndugu Wananchi, jukumu la kinga dhidi ya magonjwa yote ni la kila
mmoja wetu. Serikali kupitia Wizara ya Afya na wadau wake imekuwa ikisimamia
utekelezaji wa afua mbalimbali za kuwezesha jamii kujikinga na UVIKO-19. Aidha,
Serikali imeendelea kuwezesha upatikanaji wa chanjo nchini ambapo hadi sasa
imeshapokea jumla ya dozi za chanjo 4,305,750 ambazo zinatosha kuchanja
wananchi 2,766,575.
Aina ya chanjo zilizopokelewa
mpaka sasa ni Jansen (J&J) dozi 1,227,400 ambapo mtu mmoja anachoma dozi
moja, Sinopharm dozi 2,578,400 zitakazochanja watu 1,289,200 ambapo mtu mmoja anachoma dozi 2, na chanjo aina ya Pfizer dozi 499.950
zitakazochanja watu 249,975 ambapo mtu mmoja anachoma dozi 2.
Ndugu Wananchi, Mpaka kufikia tarehe 28 Novemba 2021, jumla ya
Wananchi waliopata chanjo ni 1,520,275 sawa na 2.7% ya watanzania wote. Kati ya
hao, watanzania waliomaliza chanjo ni 1,027,818. Lengo la Serikali ni kufikia
60% ya watanzania wote waliopata chanjo dhidi ya UVIKO 19 hivyo wizara na wadau
wake wote wataendelea kuelimisha na kutoa huduma ya chanjo. Aidha, natoa wito
kwa kila aliyechanja amwelimishwe mwingine aone umuhimu wa kuchanja.
Ndugu Wananchi, pamoja na juhudi hizi za uchanjaji, Serikali
imeendelea na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ugonjwa huu nchini kwa
kuendelea kuimarisha huduma za tiba. Mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza wigo
wa upimaji wa UVIKO-19 nchini ambapo kwa sasa jumla ya Maabara 5 zilizopo Mikoa
ya Dar es Salaam (Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii), Hospitali ya Rufaa ya
Kanda Mbeya, Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Arusha na Dodoma pamoja na maabara
katika Hospitali ya Bugando - Mwanza zinafanya upimaji wa virusi vya ugonjwa
huu. Aidha, upimaji katika maeneo mengine utafuata ambapo kwa sasa mpango ni
kuwezesha upimaji katika Hospitali zote za Rufaa za Mikoa.
Ndugu Wananchi, pamoja na jitihada hizi, hatuna budi kuchukua
tahadhari juu ya wimbi la nne la ugonjwa wa UVIKO-19. Serikali kwa kushirikiana
na wadau mbalimbali inaimarisha mikakakati ya kukabiliana na tishio hili
ikiwemo kuwakumbusha wananchi kuzingatia miongozo ya kukabiliana na UVIKO-19
ambayo ni pamoja uvaaji wa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni
au vipukusi, kuzingatia kufanya mazoezi, mlo kamili na kutumia tiba asili kama
inavyoelimishwa na wataalamu wa baraza la tiba asili.
Vilevile, kuendelea kuishirikisha
jamii katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa huu nchini kwa kuendelea kutoa
taarifa za ugonjwa huu kutoka maeneo mbalimbali duniani na ndani ya nchi, kutoa
taarifa za viashiria vya mwenendo wa ugonjwa nchini na taarifa zingine zote
ambazo zinaweza kuwa na msaada kwenye kupambana na ugonjwa huu. Kwa upande
mwingine, kuimarisha uchunguzi katika viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya
nchi kavu na kufanya ufuatiliaji wa nchi zenye ongezeko la wagonjwa na kuchukua
hatua stahiki.
Ndugu Wananchi, napenda kutoa rai kwenu kuwa twendeni tukachanje
chanjo ya UVIKO-19. Chanjo hizi zinatolewa bure na kwa hiari na pia
zimethibitishwa kuwa ni bora na salama na tayari nchini Tanzania watu wengi
wameshapata chanjo hizi na wanaendelea na shughuli zao kwa kujiamini. Nichukue
fursa hii kuwapongeza watanzania wanaoendelea kujitokeza kupata chanjo hizi
katika vituo vyetu vya huduma za afya na vituo maalumu vya huduma za mkoba
karibu na jamii.
Kipekee nitambue mikoa 10 ambayo
ilifanya kazi nzuri sana kipindi cha utoaji wa chanjo ya J & J ambayo ni
Mtwara, Ruvuma, Kilimanjaro, Lindi, Mbeya, Dar es Salaam, Arusha, Pwani, Dodoma
na Kigoma. Aidha, nipongeze pia Mikoa inayoenda kwa kasi zaidi sasa katika
kutoa chanjo ya Sinopharm, ambayo ni Mwanza, Dodoma, Ruvuma, Kagera, Mara,
Morogoro, Mbeya, Arusha, Lindi na Dar es Salaam. Nitoe wito kwa Viongozi ngazi ya Mikoa na
Halmashauri kuendelea kusimamia utoaji wa chanjo katika maeneo yao ili
kuwafikia wananchi wengi zaidi. Niwakumbushe
wale waliopata chanjo moja ya Sinopharm kurudi kuchanja dose ya pili ili wapate
kinga kamili.
Ndugu Wananchi, nawaelekeza
Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Waganga Wafawidhi wa Hospitali zote nchini
pamoja na Timu zote za Usimamizi wa Afya za Mikoa na Halmashauri, kuendelea kufanya ufuatiliaji na
kutuma taarifa za wagonjwa kwa miongozo na maelekezo waliyopewa na Wizara. Na kwa watoa huduma za Afya wote
nchini nasisitiza yafuatayo:
1. Kuimarisha
upokeaji wa taarifa kutoka kwenye jamii kupitia Madawati ya kufuatilia Tetesi
“Alert Desk”.
2. Wahisiwa
wote wa ugonjwa wa UVIKO-19 watolewe sampuli kuongeza wigo wa upimaji, ili
kujua mwenendo wa ugonjwa katika maeneo yetu.
3. Hospitali
zote za Taifa, Kanda, Mikoa na Wilaya, na vituo vya kutolea huduma za afya,
ziimarishe mfumo wa kubaini wagonjwa mapema.
4. Watoa
huduma kwenye vituo vya kutolea huduma waendelee kuzingatia Miongozo ya
Matibabu na Miongozo ya Kuzuia maambukizi.
Ndugu Wananchi, Nipende kuwasihi kutokuwa na hofu bali tuendelee kuwa watulivu na kutekeleza shughuli za maendeleo huku tukichukua tahadhari zote. Aidha, Wizara inaendelea kupokea taarifa na viashiria vya magonjwa yote ya milipuko kutoka kwa wananchi zikiwemo za UVIKO-19 kupitia namba ya simu 199 bila malipo yoyote. Wizara itaendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa magonjwa ya milipuko nchini kila baada ya siku kumi hivyo mara tatu kwa mwezi. Mwisho, wananchi zingatieni matamko na taarifa kutoka vyanzo rasmi, epukeni vyanzo visivyo rasmi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...