Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 22
Desemba, 2021 ameshiriki Mkutano Maalum wa 18 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika kwa njia ya mtandao.
Mkutano
huo Maalum umejadili ajenda kuu mbili ambazo ni kupokea ripoti ya Baraza la
Mawaziri la Jumuiya hiyo ya uhakiki wa utayari wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki na ajenda ya pili ilihusu pendekezo
la mabadiliko ya Kanuni ya 11(1) inayohusu akidi ya Mikutano ya Wakuu wa Nchi na
Wanachama wa Jumuiya hiyo.
Wakuu
wa Nchi wa Jumuiya hiyo wamepokea taarifa ya uhakiki na kuagiza Baraza la
Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuharakisha mchakato wa majadiliano ya
Mkataba (accession treaty) yatayowezesha DRC kuwa mwanachama na kuwasilisha
taarifa hiyo katika mkutano wa kawaida utakaofanyika mapema mwaka 2022.
Aidha,
kuhusu ajenda ya pili iliyohusu Kanuni ya 11(1), Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo
wameagiza Baraza la Mawaziri la kisekta la Sheria na Mahakama kukutana ili
kujadili kuhusu pendekezo la mabadiliko ya Kanuni ya 11 (1) ya uendeshaji wa
Mikutano ya Wakuu wa
Nchi Wanachama na kuwasilisha ripoti hiyo katika Mkutano ujao wa kawaida wa
Wakuu wa Nchi Wanachama kwa lengo la kujadili na kukamilisha suala hilo.
Katika
kikao hicho kilichofanyika kwa njia ya mtandao, Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki wamemkaribisha na kumpongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa
utendaji wake tangu ashike wadhifa huo.
Akihutubia
kwa mara ya kwanza katika Mkutano huo, Mhe. Rais Samia amewashukuru Viongozi wa
Jumuiya hiyo kwa ushirikiano mkubwa na kuahidi kuwa Tanzania itashiriki
kikamilifu katika kuhakikisha kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki inatimiza
malengo yake.
Aidha,
Mhe. Rais Samia amesema Tanzania ikiwa kama mwenyeji wa Makao Makuu ya EAC, itahakikisha
kuwa inatoa ushirikiano ili kuwezesha Taasisi hizo za Jumuiya kutekeleza
majukumu yake kwa ufanisi.
Katika
Mkutano huo wa EAC, Viongozi wa Jumuiya hiyo walisimama kwa dakika moja kumkumbuka
Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa mchango wake alioutoa katika Jumuiya hiyo
ya Afrika Mashariki.
Jaffar Haniu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya
Rais, Ikulu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akishiriki Mkutano Maluum wa 18 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika kwa njia ya mtandao leo tarehe 22 Desemba, 2021, Ikulu Jijini Dar es Salaam.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...