TPSF yaahidi ushirikiano na Serikali
Na Chalila Kibuda,Michuzi TV
Serikali imesema kuwa itaendelea kuweka mazingira ya sekta binafsi ikiwemo kushiriki miradi ya kimkakati ili iweze kuinua wafanyabiashara nchini.
Hayo ameyasema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akifungua mkutano Mkuu wa 21 wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) uliofanyika Jijini Dar es Salaam,amesema kuwa sekta binafsi inatakiwa kufanya kazi kwa kujituma ikiwa ni pamoja na kuweka fedha katika benki na sio kuzifungia ndani.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa kwa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Benki Kuu kuangalia namna ya kupunguza riba ili kufanya biashara ziweze kukua pamoja na kubaki na fedha za kuendesha biashara hiyo.
Amesema kuwa vitu vilivyokuwa vikwanzo wameweza kuondoa tozo ikiwa ni nia ya serikali kuhakikisha sekta binafsi inakua kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Aidha amesema kuwa katika kufanya biashara kwa sekta binafsi waende kuwekeza hadi maeneo ya vijijini kutokana na serikali kuweka huduma ambazo ni wezeshi kwa kufanya biashara.
Hata hivyo Waziri Mkuu ameziagiza Wizara ya Nishati na Wizara ya Maji kuhakikisha wanapeleka huduma za maji na nishati kwa maeneo yanayowekeza ili isiwe kikwazo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka Taasisi za Udhibiti TBS,TMDA ,Ardhi kuwa na dirisha la pamoja katika ofisi za mikoa katika kurahisisha kuondoa usumbufu kwa wawekezaji pindi wanapotaka kuwekeza.
Nae Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Angelina Ngalula amesema kuwa serikali isaidie kuwashika mkono wafanyabiashara kuweza kufanya biashara ndani na nje ya nchi kama ambavyo nchi zingine zinavyofanya.
Mwenyekiti Ngalula amesema kuwa katika miaka 21 ya TPSF serikali imeweza kuondoa vikwazo zaidi ya 40 hali ambayo imefanya sekta binafsi kuendelea na kutoa mchango kwa nchi pamoja wananchi.
Ngalula amesema sekta binafsi inaendelea katika kujiimarisha na kuongeza wanachama ambapo ni kutaka kuendelea kukua zaidi kwa kutanua uwigo wa biashara.
Amesema wanamshukuru Rais Samia Hassan Suluhu kwa kufungua milango na mataifa mbalimbali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...