Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa na utu katika maamuzi ya mashauri mbalimbali wanayoyasikiliza na kuyatolea maamuzi.
Rais Samia ameyasema hayo leo Februari 2, 2022 wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yakienda sanjari na uzinduzi wa mwaka wa kazi wa Kimahakama wa 2022.
Rais Samia amesema anafahamu changamoto ya upungufu wa Watendaji wa Mahakama kwa sasa nchini kote pamoja na vitendea kazi na vyombo vya usafiri.
“Naomba Majaji wa Mahakama Kuu mkatumie utu katika kuamua mashauri mbalimbali katika Kanda zote nchini, lakini nafahamu kwa sasa kuna upungufu wa watendaji wa Mahakama, kwa mfano, Mahakama ya Rufani kuna Majaji 26 wakati wanatakiwa Majaji 28”, amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amekemea suala la Rushwa katika Mahakama, huku akiwataka watendaji wa Mahakama hizo kupiga vita suala hilo, ambalo ni adui wa haki. Pia ameahidi kama kiongozi wa Mhimili wa Serikali kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta hiyo ya Mahakama.
“Sisi kama Serikali tutahakikisha, tunafanyia kazi changamoto zote na kuziondoa kabisa, ikiwa katika Uwekezaji katika TEHAMA kwenye Sekta ya Mahakama, kuhakikisha umeme unapatikana vijijini katika sehemu zote zenye Mahakama, tutahakikisha ushirikiano kati ya Mahakama na Taasisi za Serikali, kukamilisha Anuani za Mahakama kabla ya Sensa ya Watu na Makazi”, ameeleza Rais Samia.
Hata hivyo, Rais Samia ameahidi kufanyia kazi maombi mbalimbali yaliyotolewa na Chama cha Mawakili Tanzania (TLS) ikiwa pamoja na kupata eneo mjini Dodoma. “TLS mmeseme eneo lenu limechukuliwa na SGR, hili suala la maendeleo letu sote. Sisi tutawapa eneo kule Dodoma bila fidia yoyote kama eneo lenu la awali limechukuliwa na TRC wanaosimamia ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR)”, amesema.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...