Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Mhe. Patrobas Katambi (MB), amesema Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ni miongoni mwa
Taasisi za Serikali ambazo ni mfano wa kuigwa barani Afrika.
Ameyasema hayo wakati
wa hafla ya kukabidhi kompyuta za mezani kwa Tume ya Utumishi wa Umma (PO-PSC)
kwa ajili ya kuboresha utekelezaji wa majukumu yao iliyofanyika katika Ofisi za Mfuko huo zilizopo
Jijini Dodoma.
“Mfuko huu umekuwa ukitekeleza majukumu yake kisasa
zaidi na umewekeza sana kwenye matumizi ya Teknolojia (TEHAMA) kuanzia usajili,
kupokea michango hadi kuchakata madai vyote kwa njia ya mtandao,” amesema Mhe. Katambi.
Ameongeza kuwa WCF imefanikiwa kulipa mabilioni ya fidia
kwa kipindi kifupi sana tangu kuanzishwa kwake 2015.
“Serikali ya
Awamu ya Sita iliona umuhimu wa kuboresha mazingira ya uwekezaji ndio maana
iliridhia punguzo la michango ya wafanyakazi kwa waajiri wa Sekta Binafsi
kutoka asilimia moja (1%) hadi sifuri nukta sita (0.6%) pamoja na punguzo la
tozo kutoka asilimia kumi (10%) hadi asilimia (2%) kwa lengo la kuweka
mazingira rafiki zaidi ya uwekezaji hapa nchini, na hii ndio dira ya Mhe. Rais
wetu mama Samia Suluhu Hassan.” Alisisitiza
Mhe. Katambi amesema
WCF imejijengea utamaduni mzuri wa kusaidia bila
kubagua ambapo wamekuwa wakiwakumbuka wadau mbalimbali.
Amesema, kwa upande wa Tume ya Utumishi wa Umma, anatambua
wanawajibu mkubwa sana katika kuhakikisha wananchi wanapokea huduma
zilizokusudiwa kwa kusimamia vyema nidhamu ya watumishi wa umma. Amesisitiza ili
Tume iweze kutekeleza majukumu yeke kwa ufanisi zaidi, matumizi ya TEHAMA
kwenye ulimwengu wa sasa ni muhimu sana.
“Wajibu wenu ni kuhakikisha mnafanya kazi kwa
kuzingatia sheria, simamieni nidhamu ya Utumishi wa Umma na endeleeni kuangalia
maeneo mengine yanayoweza kuboresha utendaji kazi wenu. TEHAMA inapunguza
urasimu hakikisheni mnatumia kompyuta hizi katika kuongeza tija kwenye shughuli
zenu za kila siku hususan wakati huu ambao Serikali ya Awamu ya Sita ina
dhamira ya dhati ya kumaliza kero ya urasimu katika utoaji wa huduma za
Serikali kwa wananchi wake”, amesema Mhe. Katambi.
Mhe. Katambi pia amewapongeza WCF kwa kuandaa
machapisho yenye miongozo mbalimbali kuhusu fidia kwa wafanyakazi kwa nukta nundu
ambayo yalikabidhiwa kwa Jumuiya ya Watu Wasioona (TAB) wakati wa kilele cha
Maadhimisho ya Maandishi ya Nukta Nundu(Braille). Vilevile amewapongeza kwa
misaada ya fimbo nyeupe kwa jamii hiyo yenye mahitaji maalum. Huu ni utamaduni
mzuri endeleeni kugusa makundi yote kwenye jamii yetu, amesisitiza Mhe. Katambi.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma amesema pamoja na punguzo hilo la michango ya
waajiri la kutoka asilimia moja (1%) hadi kufikia asilimia sifuri nukta sita
(0.6), malipo ya fidia kwa wafanyakazi hayataathirika.
Akizungumzia kuhusu
vifaa walivyotoa, Dkt. Mduma amesema walipokea maombi ya vifaa mbalimbali vya kiutendaji kutoka Tume ya Utumishi
wa Umma na kwa kutambua umuhimu wa mahitaji hayo WCF iliona ishiriki katika kusaidia
upatikanaji wa kompyuta za mezani kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji
pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.
Mama Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuleta
maendeleo kwa wananchi.
“Tunatambua umuhimu wa Tume hii katika kusimamia
uwajibikaji nchini hususan watumishi wa umma. Usimamizi wao madhubuti
utachangiwa sio tu na uweledi wa wafanyakazi wa Tume katika utekelezaji wa
majukumu yao bali pia uwepo wa vifaa vitakavyorahisisha utendaji kazi”,
alisisitiza Dkt. Mduma.
Naye Katibu wa
Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew Kirama ameishukuru WCF kwa msaada huo na
kuongeza kuwa umekuja wakati muafaka.
“Tunatambua kuwa
zipo Taasisi nyingi zinazokabiliwa na changamoto ya vitendea kazi lakini mmeipa
Tume kipaumbele tunawashukuru sana na kuahidi kuongeza bidii zaidi ambapo vifaa
hivi ni sehemu ya uboreshaji wa utendaji kazi wetu”, amesema Bw. Kirama.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...