Na Mwandishi wetu, Babati
Sintofahamu
imeibuka kwa baadhi ya wanachama wa CCM wa Wilaya ya Babati Mjini
Mkoani Manyara, wakilalamikia utaratibu wa ugawaji wa kadi za chama
hicho kwa manufaa ya watu wanaotaka madaraka kwenye uchaguzi mkuu wa CCM
unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Wanachama
hao ambao waligoma kutaja majina yao wakizungumza jana mjini Babati
wameomba viongozi wa CCM wa mkoa huo kuingilia kati na kuchukua hatua
ili ugawaji huo wa kadi usiofuata utaratibu ukomeshwe.
Mmoja
kati ya wanachama hao amedai kuwa watu hao wamepata kadi hizo na
wanatarajia kuzigawa kuanzia mwezi ujao wa Machi kwa watu wao ili waweze
kuwaingiza madarakani.
“Kadi
zinapaswa kutolewa kwenye na tawi kugongwa muhuri na kuingizwa kwenye
rejesta ya chama ila katibu tawi ndiyo anapaswa kuainisha mahitaji yake
ya kadi kwa katibu kata akiambatanisha orodha ya waombaji wa kadi na
siyo kama kama ilivyo sasa kwa kadi kupokelewa kutoka juu bila barua ya
maombi ya katibu wa wilaya,” amesema.
Mmoja
kati ya wanachama wa chama hicho kwenye kata ya Maisaka alisema
Mwenyekiti wa CCM wa kata moja alikuwa na kadi 300 anazogawa kwa watu
wake bila utaratibu.
“Huyu
Mwenyekiti alikuwa na kadi hizo tangu mwezi Desemba mwaka jana na
alikuwa anagawa kwenye mfumo usio rasmi kwa watu ambao hawajaomba
kupitia ofisi ya tawi lolote lile ila bado yupo nazo nyingi akisubiri
mwezi Machi,” amesema.
Mwanachama
mwingine amesema miongoni mwa wanaogawa kadi hizo za mchongo ni
kiongozi mmoja Mwenyekiti wa Serikali ya mtaaa uliopo kata ya Bagara
mwenye kadi 700.
Amesema
kadi ya CCM inapaswa kugongwa muhuri na katibu wa Tawi ila Mwenyekiti
huyo wa Serikali amekuwa anagawa kadi hizo za mchongo kwa wanachama
wapya bila kufuata utaratibu halali.
Mwenyekiti
mstaafu wa halmashauri ya mji wa Babati Mohamed Farah maarufu kama
(Mwanamaombi) amesema hata yeye alisikia taarifa za kuwepo kadi
zinazogawanywa kwa watu bila utaratibu.
Farah
amesema endapo utaratibu huo utatumika utakiharibu chama chao, kwanza
unachangia kuwafanya wanachama kutokuwa na mazoea ya ulipaji wa ada na
kukaa kusubiri uchaguzi na utaratibu huu pia ndiyo chanzo cha kupata
viongozi wabovu wasio na sifa ndani na nje ya chama.
“Pengine
ungezungumza na katibu wa CCM wa wilaya ya Babati mjini ambaye ndiye
mtendaji mkuu wa chama kwenye eneo hili, anaweza kukueleza zaidi juu ya
hilo,” amesema Farah.
Katibu
wa CCM wa wilaya ya Babati mjini Daniel Muhina amekiri kuwa na kadi
mpya ambazo zipo ofisini kwake na amezipokea kwa utaratibu kutoka ofisi
ya CCM mkoa wa Manyara.
Amesema
kadi zote ambazo zipo kwenye matawi na zinagawiwa hivi sasa kwa
wanachama wapya ni halali na makatibu wa matawi waliozichukuwa walisaini
kabla ya kupatiwa.
“Hakuna
kadi ambazo zinagawiwa mitaani bila utaratibu ila ni uzushi tuu kwa
baadhi ya watu wenye lengo la siasa za kuchafuana ndiyo wanazungumza
hayo,” amesema Muhina.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...