




******
NA MWANDISHI WETU
Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe.Hashim Mgandilwa amelipongeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa jitihada inazozifanya za kuendesha mafunzo kwa lengo la kuelimisha wajasiriamali na umma kwa ujumla juu viwango na ubora wa bidhaa hususani bidhaa za chakula.
Ametoa pongezi hizo leo tarehe 29/03/2022 wakati akifungua mafunzo kuhusu udhibiti wa Sumukuvu kwa mazao ya mahindi, karanga, Viungo vya chakula pamoja na bidhaa zake kwa wajasiriamali kutoka katika Jiji la Tanga.
Amesema Umuhimu wa chakula unasababisha suala la usalama kupewa kipaumbele katika kulinda afya ya jamii na uchumi wa nchi na kuwa kigezo muhimu katika biashara ya kitaifa na kimataifa.
"Chakula kisicho salama husababisha madhara ya kiafya na hata vifo kwa walaji pamoja na kusababisha athari za kiuchumi. Hata hivyo, usalama wa chakula unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchafuzi wa sumukuvu ambayo husababisha madhara ya kiafya na hata kiuchumi". Amesema
Aidha amewasihi wasindikaji na wazalishaji wa mazao kuzingatia mikakati ya kukabiliana na changamoto ya sumukuvu ili vyakula vyetu viendelee kuwa salama kwa muda wote.
Kwa upande wake Meneja wa Mafunzo na Utafiti Mwl.Hamisi Mwanasala amesema mafunzo hayo ni mojawapo ya fursa muhimu ya kuelimisha jamii juu ya kukabiliana na sumukuvu ili kulinda afya za wananchi na kuwezesha biashara ya chakula.
"Ili kuimarisha usalama wa chakula dhidi ya sumukuvu, TBS inatekeleza mikakati mbalimbali, ikiwemo udhibiti wa sumukuvu kwenye chakula hususani mazao ya mahindi, karanga na viungo vya chakula ambayo ndiyo yenye uwezekano mkubwa wa kuchafuliwa na sumukuvu". Amesema Mwl.Mwanasala.
Amesema TBS inatoa elimu kwa wadau katika mnyororo wa thamani wa mazao ya chakula kwani jamii ikielimika itatoa mchango zaidi katika kukabiliana na sumukuvu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...