WAZIRI
wa Madini, Dkt. Doto Biteko ameagiza kuundwa kwa Kamati Maalum ya
Wataalamu ili kuchunguza uwepo wa milipuko inayolalamikiwa na wananchi
kuwa chanzo cha mitetemo wanayoipata katika eneo la Kijiji cha Ulowa
kilichopo Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga.
Dkt.Biteko
ametoa agizo hilo leo Aprili 30, 2022 katika Kijiji cha Ulowa
Halmashauri ya Ushetu Wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga na akitaka kazi
hiyo ifanyike ndani ya wiki mbili.
Dkt.
Biteko amesema, Wizara ya Madini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti
wa Madini Tanzania (GST) itapeleka timu ya wataalamu inayohusika na
mitetemo ya ardhi ambao watafanya kazi ya uchunguzi kwa muda wa wiki
mbili.
Amesisitiza kuwa,
tetemeko la ardhi haliwezi kuwa limesababishwa na shughuli za kibinadamu
kwa kuwa hakuna ulipuzi wa miamba mikubwa unaofanyika katika eneo hilo.
Amesema
GST itasimika kifaa maalum katika eneo la Ulowa kwa ajili ya kunakili
mawimbi ya mitetemo mbalimbali itakayotokea katika eneo hilo ili kupata
taarifa sahihi juu ya chanzo halisi cha mitetemo hiyo.
Naye,
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojojia na Utafiti wa Madini Tanzania,
Dkt. Musa Budeba amesema, GST itafanya utafiti wa ziada ili kubaini
chanzo cha mitetemo katika maeneo hayo na kusisitiza kuwa wataalamu
watafika katika maeneo ya mitetemo ili kuondoa hofu walizonazo wananchi
hao kuhusu matetemeko ya ardhi.
Kwa
upande wake, Mjiolojia Mwandamizi, John Kalimenze akisoma taarifa
kuhusu mitetemo ya ardhi inayosadikiwa kuwa tetemeko la ardhi amesema,
jumla ya wananchi takribani mia moja walipatiwa elimu na mafunzo kuhusu
tetemeko la ardhi, namna gani linatokea, jinsi ya kuchukua tahadhari
kabla halijatokea, wakati linapotokea na baada ya kutokea.
"Mafunzo
hayo yalisaidia sana kupunguza taharuki iliyokuwepo miongoni mwa wakazi
wa Ulowa namba 8 na maeneo ya jirani kama ambavyo waliwaeleza wataalamu
baada ya kupatiwa mafunzo," amesema Kalimenze.
Taarifa
za mitetemo kutoka Kituo cha GST cha kuratibu mitetemo ya ardhi
kilichopo mjini Geita zinaonesha kwamba, hakuna matetemeko ya ardhi
yaliyotokea katika eneo la Ulowa katika kipindi cha tarehe 19 hadi 21
Aprili, 2022 kama ilivyodaiwa na wananchi wa Ulowa.
Kikao
hicho, kimehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga, Mbunge
wa Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani, Diwani wa Kata ya Nyamilangano,
Robert Mihayo na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Madini na Tume
ya Madini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...