Adeladius Makwega-DODOMA
Leo hii nimeikumbuka haiba ya mama mmoja ambaye aliwahi kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne. Msomaji wangu usione gere, leo mwanakwetu na haiba ya mama waziri wa zamani?
Nasema Naaam HAIBA WAZIRI WA ZAMANI?
Tambua kuwa kila mmoja wetu anavyo vitu anavyovipenda. Waziri huyu alikuwa mama mmoja mrefu, mwembamba, maji ya kunde, akibadilisha nguo za rangi tafauti, hayo yote tisa kumi ni ule mtindo wa nywele zake.
Ehee alikuwa anavaa wigi? Alikuwa akiweka dawa nywele zake na kuchana mitindo mbalimbali kama vile Bob, Bati, Moja kwa moja, Mkeka na mingine mingi?
Huko kote mwanakwetu sipo.
Siye waswahili tuna mitindo mingi ya nywele, mathalani Mwali Anatoka Mkoleni, Mwali Anakwenda Mkoleni, Kilimanjaro, Kukata nywele, Mabutu na Upara.
Mabutu husukwa kulingana na upenzi wa msukwaji kama yanasukwa mawili au zaidi ya hapo. Mabutu hayo yanaweza kuwekewa nyuzi au bila nyuzi. Upara nao ni mtindo mwingine huo hupakwa mafuta mengi huku ukimiminiwa na ufuta hasahasa bibi harusi akiwa anaolewa au akiwa anatolewa nje baada ya kukaa ndani.
Je mwanakwetu nimeangukia wapi?
Wakati wote niliyojaliwa kumuona waziri huyu wa zamani, macho yangu yalialikiwa na tabasamu zito lililopambwa na nywele za mtindo wa twende kilioni, nywele zake zilikuwa mithili ya maua yaliyoota mlimani katika bustani nzuri ya mfalme.
Macho yangu yalipoutazama mtindo huo, yalinipa hamu ya kutamani sana kukishika kichwa hicho cha mheshimwa waziri wetu wa zamani, ningekuwa mtoto ningedanganya kwa kumsalimia kwa kumshika kichwa ili ile kiu yangu ikatike lakini sifa ya utoto sina. Mie ni mkubwa, kibali cha kufanya hivyo sina. Nina hakika mwenye kibali cha kufanya hivyo kwa mheshimiwa huyo yupo.
Swali lililobaki moyoni mwangu tangu wakati huo hadi sasa, je kama kuzishika bila kibali ni kosa kama sheria ya SOSPER inavyonadi, je kuusifia mtindo wa nywele hizo za mheshimiwa wetu ni kosa?
Binafsi naona sioni haja ya kufunga safari hadi parokiani kwangu kumuuliza Baba Padri/Baba Mchungaji juu ya hili la kusifia mtindo huu wa nywele wa mheshimiwa wetu wa zamani.
Yote hayo ni ya waziri wa zamani, Fenera Mukangara aliyechagua mtindo wa Twende Kilioni ambapo huko ndipo moyo wangu ulipo, kwa hesabu zangu Mheshimiwa Fenera Mukangara alikuwa akisuka nywele 16, yaani 16 kichwa, moja ,mbili tatu…hadi ya kumi na sita.
Twende Kilioni umemtambulisha mno mheshimiwa huyu lakini pia ametuwakilisha vizuri siye makabwela kwa kuusuka mtindo huo kila mara.
“Yule Waziri aliyekuwa akisuka twende Kilioni, amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi bwana!”
Hapo makabwela wanamkumbuka Fenera Mukangara huku wakiusifia mtindo wake wa nywele.
Nyumbani kwetu Mbagala Sabasaba Dar es Salaam kuna mama mmoja maarufu mno anaitwa Mama Mchafu, mama huyu na binti zake ni wasusi wazuri sana wa aina mbalimbali za nywele, nilipowauliza juu ya gharama za kusuka twende kilioni walicheka sana.
“Kaka unaulizia kusuka twende kilioni unataka kumleta shemeji yetu kusuka? Kaka acha ubahiri ” Niliambiwa
Nikajibu hapana, wakacheka sana wakasema kaka huo mtindo tunasuka bure, huo ni kama kachumbari katika pilau, lakini mitindo mingine ni pesa yako tu kati ya Tsh 5000-70,000/-
“Lakini kaka, mwanamke akisuka twende kilioni anajiamini sana, hakuna kusema nywele zimetimka wala zitaanguka chini, hapo unahitaji tu kuziosha vizuri, kuziweka mafuta ya maji na unazisuka vizuri mno.”
Aliniambia Mama Mchafu.
Binafsi ninaupenda sana usukaji wa mheshimiwa Fenera Mukangara wa Twende Kilioni, nawaomba wengine pendeni mitindo mingine. Huu ni wangu mie.
Sifahamu mheshimiwa Fenera Mukangara alipo kwa sasa, lakini popote alipo namualika mheshimiwa huyu kwa heshima na taadhima aje kusuka mtindo huu kwetu Mbagala Sabasaba nina hakika Mama Mchafu ataweza kutoa 32 kichwa ya twende kilioni yaani moja, mbili ,tatu …hadi ya thelathini na mbili.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...