Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema haikuwa rahisi kutengeneza Filamu ya ‘The Royal Tour’ ambayo kwa sasa inazinduliwa nchini, Filamu yenye lengo kubwa kutangaza Utalii wa Tanzania na kuvutia Wawekezaji nchini.
Akizungumza katika uzinduzi wa Filamu hiyo, jijini Arusha, Rais Samia amesema kama muhusika wa Filamu hiyo, haikuwa rahisi kutokana na matakwa ya Waongozaji, akiwemo Peter Greenberg na mwenzako John ambapo mara kadhaa walikuwa wakiamuru kurudia matukio l ili kupata picha nzuri.
“Waliniambia weka Urais wako ofisini, ukija huku wewe ni ‘Tour Guide’ ukija huku wewe ni ‘Actress’, Urais sisi hatuna habari nao, kwa hiyo nikafanya hivyo, walikuwa wananituma ‘action’ moja unaifanya mara kumi, wakati mwengine nakasirika lakini wanasema, No! No! Samia ‘You have to do it’, amesema Rais Samia.
Mhe. Samia amesema wametumia siku nane kutengeneza Filamu hiyo na kupatikana kwake ambayo itaitangaza nchi ulimwenguni na kupata matunda kama Taifa, amesema tumeanza uzinduzi mkoani Arusha kutokana na kuwa Kitovu cha Utalii na ambapo Sekta hiyo inafanya vizuri, baadae uzinduzi huo utafanyika Zanzibar na Dar es Salaam.
Mhe. Samia amesema Filamu ya ‘The Royal Tour’ kwa kiasi kikubwa itatumika kutangaza Utalii na vivutio vya Uwekezaji na kufanya biashara, ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kutazama Filamu hiyo ambayo itapatikana nchini baada ya uzinduzi.
“Watanzania wanapaswa kutazama Filamu hii, pengine kuna vitu vipo humo hatuvijui, moja na uhakika hamlijui! Mtakuta kuna Ghala kubwa la Meno ya Tembo na Faru, hizi Pembe tumezikamata zilikuwa zinavushwa kimagendo, kwa miaka mingi zimehifadhiwa lakini tukaona tuseme Watanzania waone jinsi wanavyoteketeza Wanyama”, amesema Rais Samia.
Pia, Mhe. Rais amesema lengo kuonyesha ulimwengu kuwa biashara hiyo ya Meno ya Wanyama kama Tembo na Faru haifai kutokana na kuteketeza idadi ya Wanyama hao ambao ni tunu kwa taifa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...