Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akizungumza wakati wa hafla ya mapokezi ya meli hiyo na kueleza kuwa maboresho na maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia yataleta matokeo chanya zaidi, leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA,) Eric Hamissi akizungumza wakati wa hafla ya mapokezi ya ndege hiyo na kueleza kuwa kupitia maboresho yaliyofanyika wataendelea kupakua shehena nyingi zaidi na kuongeza mapato.

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA,) imeendelea kuvunja rekodi ya kupokea meli kubwa ambapo leo Aprili 8, 2022 imepokea meli kubwa zaidi kuwahi kufika katika bandari ya Dar es Salaam  'MV FRONTIER ACE' yenye ukubwa wa GRT 52,276 na urefu wa mita 189.45 iliyobeba magari 4,041 huku ikielezwa kuwa mafanikio hayo yametokana na maboresho makubwa ya Bandari hiyo yalifanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea meli hiyo iliyotoka moja kwa moja Japan hadi Tanzania Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema maboresho hayo yameleta mafanikio tele ukilinganisha na miaka mitatu iliyopita.

"Awali tulikuwa tukipokea magari 500 hadi 700 na kupitia maboresho yaliyofanywa na Serikali katika gati ya magari leo tunashuhudia historia ya kupokea magari 4,041 kwa wakati mmoja." Amesema Waziri Mbarawa.

Amesema, Rais Samia amekuwa Balozi bora katika kuitangaza bandari hiyo hali iliyopekea bandari kufunguka zaidi na kueleza kuwa maelekezo aliyoyatoa Rais kuhusu magari kukaguliwa nje ya nchi yataleta fursa nyingi zaidi hasa katika upakuaji wa haraka wa mizigo pamoja na kupokea magari mengi zaidi.

Vilevile Waziri Mbarawa amekitaka kitengo cha masoko cha Mamlaka hiyo kutoka nje na kuzungumzia majukumu lukuki yanayofanywa ili kuwavutia wateja wengi zaidi.

"Kitengo cha masoko kitoke nje na kuzungumzia Mamlaka hii na majukumu yake na hilo ni pamoja na kuzingatia usalama wa bidhaa za wateja ili kuwavutia zaidi.....TPA Mnafanya kazi nzuri ila fanyeni kwa kujilinganisha kwa kujipanga  kushindana na wengi." Amesema.

Kuhusiana na changamoto ya vifaa Prof. Mbarawa ameiagiza Mamlaka hiyo kutumia vifaa vilivyopo vizuri na kuagiza makontena yote yanayokaa muda mrefu kupelekwa bandari kavu kwa kuwa bandari ni sehemu ya kupakua mizigo na sio kuhifadhi. 

Awali akieleza mafanikio ya Mamlaka hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan Mkurugenzi Mkuu wa TPA  Eric Hamissi amesema kuwa, kumekuwa na uboreshaji wa bandari ili kuhakikisha wateja kutoka ndani na nje ya nchi wanapata huduma bora zaidi.

"Meli hii tunayoipokea leo hii imebeba magar 4,041  huku yanayoenda nje ya nchi ni magari 2,936 na yanayobaki nchini ni magari 1,105...Na magari yanayosafirishwa kwenda nchi za nje yanaelekea katika nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Malawi, Msumbiji, Sudan, Uganda, Zambia na Zimbabwe." Amesema.

Amesema kupitia maboresho yanayofanyika wanatarajia kuhudumia shehena kubwa zaidi za mizigo mchanganyiko.

Kuhusiana na ongezeko la shehena katika bandari ya Dar es Salaam Hamissi amesema,Katika  kipindi cha Machi 2021 hadi Februari 2022 kiwango cha shehena kilichohudumiwa na Mamlaka hiyo ni Tani milioni  19.225 sawa na asilimia 3.8 ya lengo la kuhudumia tani milioni 18.522.

"Mamlaka hii imeendelea kuvunja rekodi za kuhudumia shehena kwa ufanisi na viwango vikubwa na kuongeza mapato ya Mamlaka ambapo kwa kipindi cha kuanzia Machi 2021 hadi Februari 2022 mapato yalifikia shilingi bilioni 1,018 sawa na asilimia 95.5 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 1,067.41 na kufanya ongezeko la mapato yaliyokusanywa  kufikia asilimia 18.8." Amesema.

Aidha amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Balozi bora katika kuitangaza bandari hiyo katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa na kuahidi kuendelea kuwahudumia wateja kisasa kupitia bandari zao.

 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TPA Balozi Ernest Mangu akizungumza katika hafla hiyo na kueleza kuwa maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia yatazingatiwa katika kukuza bandari na kutoa huduma bora kimataifa.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo akizungumza katika hafla hiyo na kuahidi ushirikiano katika usalama katika kuyafikia mafanikio .








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...