NA YEREMIAS NGERANGERA….NAMTUMBO
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Dkt Julius Kenneth Ningu amewataka wananchi kuwabaini wanaopotosha zoezi la Sensa katika maeneo yao ili waweze kuchukuliwa hatua .
Akizungumza na wajumbe wa kamati ya sensa ngazi ya wilaya Dkt Ningu aliwataka wajumbe wa kamati kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu wilayani humo kubaini wananchi wanaopotosha zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajia kufanyika mwezi agusti mwaka huu.
Dkt Ningu pamoja na kuwaagiza wajumbe wa kamati alidai ziara ya mikutano katika kata 21 za Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kuhamasisha zoezi la Sensa litaanza kwa Lengo la kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kusikiliza changamoto toka kwa wananchi zinazoweza kuathiri zoezi la sensa lisifanyike kwa ufasaha na kuzipatia ufumbuzi wake
Aidha mkuu wa wilaya ya Namtumbo aliwaambia wajumbe kuwa zipo taarifa za wilaya katika sensa ya mwaka 2012 kuwa kulikuwa na watu kazi yao kubwa ilikuwa kupotosha wananchi kuhusu Sensa ya watu na makazi na kwa sensa ya mwaka huu mkuu wa wilaya huyo alisisitiza kutowaruhusu watu kupotosha wananchi juu ya zoezi la sensa na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria dhidi yao.
Katibu wa mbunge Zuberi Lihuwi aliyemwakilisha Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vitta Rashid Kawawa katika kikao hicho alimthibitishia mkuu wa wilaya kuwa katika sensa ya mwaka 2012 changamoto ya kuwepo kwa vikundi vya watu kuhamasisha wananchi kutokuhesabiwa lilikuwa kubwa na kuathiri upatikanaji sahihi wa takwimu za watu wa wilaya ya Namtumbo.
Lihuwi alidai yeye haamini takwimu ya idadi ya watu iliyopatikana katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 ilikuwa na uhalisia katika wilaya ya Namtumbo kwani idadi kubwa ya wananchi hawakuhesabiwa kutokana na kikundi hicho kupotosha wananchi kuhusu zoezi la sensa.
Glory Lwomile Hakimu mfawidhi wa wilaya ya Namtumbo naye pia alimthibitishia mkuu wa wilaya kuwa kikundi cha watu kinachohamasisha wananchi wa Namtumbo kutohesabiwa kinatoka nje ya wilaya ya Namtumbo akitolea mfano wa sensa ya mwaka 2012 kuwa yeye alikuwa katika wakati mgumu baada ya mahakama kuwaweka mahabusu baadhi ya wananchi ambao sio wakadhi wa Namtumbo baada ya kubainika kuhusika na kuwahamasisha wananchi kutoshiriki zoezi la sensa alisema Hakimu huyo.
Mratibu wa Sensa wilaya ya Namtumbo Kuno Ntini aliwaambia wajumbe kuwa maandalizi ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 katika wilaya ya Namtumbo yanaenda vizuri ambapo mpaka sasa kazi zilizofanyika ni pamoja na uundaji wa kamati za sensa ngazi za wilaya,kata ,vijiji na vitongoji umekamilika,ubandikaji wa matangazo ya ajira ya muda ya sensa ya mwaka 2022 katika kata zote zoezi ambalo nalo lilienda vizuri na utoaji wa ufafanuzi juu ya changamoto za waombaji wa nafasi za ajira za muda ya sensa nalo lilienda vizuri.
Ntini alidai waombaji wa ajira ya Muda ya sensa katika mfumo wa maombi kadiri ya tume ya taifa ya takwimu (NBS)wilaya ya Namtumbo waombaji wamefikia 2,277 ikiwa walioomba ukarani 1,741,usimamizi wa mahudhui 481 na usimamizi wa Tehama 55 huku maombi yaliyotumwa NBS ni 2047 na maombi 230 yanasubiria ukamilishaji wa fomu namba 1 alisema Ntini. Sensa ya mwaka huu 2022 katika wilaya ya Namtumbo mkuu wa wilaya amedai hataruhusu kikundi cha watu kupotosha zoezi la sensa na watakaobainika kufanya hivyo watakamatwa na kufikishwa mahakamani kwa zoezi la kuhujumu zoezi la sensa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...