Na Said Mwishehe, Michuzi TV
SHIRIKA la Limitless Mind Organization limetangaza kuzindua program ya Visionary Ladies Panel pamoja na kufanya harambee kupitia mradi wa Mwanadada Smart Charity kwa lengo la kumkomboa binti aliye mtaani anayepitia changamoto kubwa za kiuchumi na kikatili.
Akizungumza leo Juni 25,2022 wakati wa uzinduzi wa program hizo , Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Limitless Mind Organization Lydia Leonard amefafanua kuhusu Visionary Ladies Panel itawalenga mabinti/ wanawake wajasiriamali na wafanyabiashara au wenye ndoto kubwa na kupitia panel hiyo watakuwa wakijadili masuala yanayomkumba mwanamke kiuchumi, kimahusiano /ndoa.
“Tumekutana hapa kwa mambo makubwa mawili, kwanza tunafanya uzinduzi wa program Visionary Ledies Panel ambayo tunalenga kuifanya kwa wanawake wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo katika Mkoa wa dar es salaam na itakuwa ikifanyika kwa mwezi mara moja katika kipindi cha mwaka mzima.
“Hiyo Panel tutakuwa tunakutana na mabinti, wanawake wajasiriamali na wafanyabiashara ambapo tutakuwa tukijadili kuhusu changamoto zinazomkumbuka mwanamke ambaye anafanyabiashara na yuko kwenye mahusiano yakiwemo ya ndoa,”amesema.
Aidha jambo la pili amesema ni kufanya harambee kwa ajili ya kufaniksiha mradi Mwanadada Smart Charity ambao unalenga kumkomboa binti ambaye yuko mtaani ,hana kazi na hajasoma kwa hiyo watatumia mradi huo kumpatia ujuzi na baada ya ujuzi watamuwezesha kupitia ule ujuzi kukidhi mahitaji yake.
Kuhusu ndoto waliyonayo Limitless Mind Organization amesema wanataka kumbadilisha mwanamke au binti ambaye yuko mtaani hajasoma na hana kazi kwani wanaamini kuna wengine hawajasoma si kwasababu wanapenda bali walikosa watu wa kuwawezesha kwenda shule na wako mtaani.
“Tunaweza kuona tatizo la ajira ni kubwa sana na imekuwa changamoto, hata sisi tuliosoma tuna vyeti lakini tumeviweka ndani na hivyo tunapitia changamoto hiyo. Kwa hiyo tukaona tukiwawezesha kwa kuwapa ujuzi ambao hauhitaji uwe na elimu ya vyuo au vyeti bali uwe na uwezo wa kufanya kitu inaweza kusaidia katika kumsaidia mwanamke au binti kukabiliana na changamoto za kimaisha”.
Aidha amesema lengo lao ni kuwafikia mabinti 50 walioko kwenye Mkoa wa Dar es Salaam katika kipindi cha mwaka mmoja na kwamba watafanya kile wanachoweza kwa kusaidiana na wadau wengine ambao watajitokeza na kushirikiana nao.
Kwa upande wake Ofisa Masoko wa Limitless Mind Evodia Wiston akielezea namna ya kuwapata mabinti hao ambao watapatiwa ujuzi , watatumia mbinu mbalimbali ikiwemo ya kukutana na viongozi wa Serikali za Mitaa, nyumba za ibada pamoja na vyombo vya habari.
“Watu wengi wenye uwezo wa chini au ambao hawajafanikiwa wanakwenda sana katika nyumba za ibada na kuomba msaada na viongozi wa nyumba hizo wanawafahamu, hivyo watatusaidia kuwapata watu hao lakini katika Serikali za mitaa nako wanazo taarifa za watu wenye uhitaji hasa mabinti,”amesema.
Ameongeza kuwa wao wanaamini kuna mabinti wengi ambao wako mtaani na hawajafanikiwa kupata elimu na kutofanikiwa huko sio kwasababu hawana uhitaji wa elimu.“Kuna mabinti wengi sana wanapenda kusoma lakini unakuta nguvu zao zinakatishwa kwasababu mbalimbali.
“Kama unavyojua siku hizi kuna mabinti wengi wanaingia kwenye mahusiano ambayo wakati mwingine yamekuwa yakisababisha changamoto na kujikuta wakikatisha ndoto zao.Pia tunafahamu kuna wazazi au walezi wengi hawana uwezo wa kupeleka watoto shuleni.Hivyo kupitia mradi huo mbali ya kuwapa ujuzi tutakuwa tukiotoa elimu ya namna sahihi ya kukabiliana na changamoto hizo ili watimize ndoto zao,”amesema.
Wakati huo huo Paulina Deusdedith akizungumza kwa niaba ya mabinti wengine ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza ni matumaini yao kupitia program hizo kuna mambo watajifunza na kuwa chachu kuwafanya kutimiza malengo yao pamoja na kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo wanawake na mabinti wamekuwa wakikumbana nazo.
Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Limitless Mind Organization Lydia Leonard(kushoto) akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 25,2022 mkoani Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa program hiyo sambamba na harambee ya kufanikisha mradiwa Mwanadada Smart.
Sehemu ya washiriki wakiwa katika tukio hilo lililofanyika leo mkoani Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali waliojikita katika kumsaidia mwanamke na mabinti wa kitanzania kutimiza ndoto zao.
Baadhi ya mabinti ambao wamechaguliwa kuwa sehemu ya washiriki wa program hizo wakiwa makini kufuatilia maelezo mbalimbali yaliyokuwa yakitolewa kuhusu program hizo sambamba na harambee ya kuchangia mradi wa Mwanadada Smart.
Sehemu ya washiriki wakiendelea kuandika baadhi ya maelezo muhimu yaliyokuwa yakitolewa wakati wa uzinduzi huo.
Sehemu ya washiriki wakiendelea kuandika baadhi ya maelezo muhimu yaliyokuwa yakitolewa wakati wa uzinduzi huo.
Baadhi ya washiriki wa uzinduzi huo wakijadiliana jambo .
Paulina Deusdedith akizungumza kwa niaba ya mabinti waliohudhuria uzinduzi wa program hizo ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza ni matumaini yao program watajifunza masuala mbalimbali yatakayowezesha kutimiza ndoto zao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...