AWAMU ya pili ya mchakato wa kuhamisha wakazi wa eneo la Ngorongoro kwa hiyari limewasili Kijiji Msomera wilayani Handeni ambapo jumla ya kaya 27 yenye watu 127 na mifugo 488 wamehamishwa, kaya 1 kati hizo imehamia Karatu

Akizungumza baada ya kuwasili kwa kaya hizo , Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Kijiji cha Msomera Martin Oleikayo Paraketi amesema juzi wamepokea wageni kaya 21 yenye watu 111 na Juni 23,2022 wamepokea kaya 27 zenye watu 127 pamoja na mifugo 488.

"Tumewapokea na tutaendelea kuwapokea wageni wanaotoka Ngorongoro, lakini pia na sisi kama wana Kijiji wa Msomera tunaona ni fursa, sababu tumeshaona hapa kuna huduma zote muhimu za kijamii. Kuna kituo cha afya kipya kinajengwa, Kuna shule ya Msingi ambayo tumeipa jina la Samia Suluhu Hassan kwani yeye ndio ametujengea,tuna sekondari mpya, miundombinu ya maji na huduma nyingine zote zipo,"amesema.

Akielezea zaidi amesema kwanza wanashukuru Mungu kwa mapenzi yake mema lakini anaipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na Wizara zote za Wizara ya Maliasili na Utalii inayongozwa na Balozi Pindi Chana na Wizara ya Mifugo kwa kusimamia vema mchakato huo hadi ulikofikia .

"Niwapongeze kwa kazi kubwa ambayo wameifanya au wanayoendelea kufanya kutokana na agizo la Rais kuondoa watu katika Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro kwa hiyari kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi, kwanza niwapongeze na kuwashukuru sana na sisi kama Wana Kijiji cha Msomera tunaunga mkono jitihada za Serikali.Mimi kama kiongozi niliyechaguliwa na kusimamia utaratibu wa Serikali au kanuni zote za Serikali niko pamoja nayo .

"Waziri Mkuu jana alikuwa Ngorongoro na Loliondo na baadae akaja Kijiji cha Msomera na ukimuangalia unaona ambavyo amechoka lakini kwa kutujali amekuja kwa ajili ya kuendelea kuwatumikia Watanzania ,Mungu amlinde na aendelee kumpa hekima na busara ili kusukuma gurudumu alilopewa kama Mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali,"amesema.

Aidha amesema "Tunatoa ombi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mama yetu sisi wakazi wa Kijiji cha Msomera na wanaotoka Ngorongoro, sisi ni watoto wake maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu Aprili 24 kwa kutamka kwamba watu wa Msomera waliopo na watakaokuja kutoka Ngorongoro watakuwa sawa

"Ninachoomba watu wazingatie maagizo, kwa sababu Waziri Mkuu alisema wote watapewa hati miliki kwa watu wote wa hapa,pia alisema hakuna mtu anayenyanyaswa ,hivyo tunachoomba maagizo ya Waziri Mkuu yazingatiwe .Ndicho Wananchi wanachoomba lakini wako tayari kwa mikono yote miwili kupokea wenzetu".

Kuhusu kiijiji iwapo kinajitosheleza kihuduma kutokana na watu walioingia, Mwenyekiti huyo wa Kijiji hicho amesema idadi ya wakazi awali ni 6500 lakini hivi sasa wanaelekea wakazi 7000,pia kuna mifugo.Tunachoomba kwa Serikali maeneo ya malisho ya mifugo yaongezwe ili kutosheleza mahitaji na mifugo inayoendelea kuongezeka.

Awali mmoja ya wakazi wa Ngorongoro ambaye amehamia kwenye Kijiji Cha Msomera akitokea Ngorongoro Masiaya Parikoi Saseka amesema yeye na familia yake pamoja na mifugo wamefika salama.

Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali na kuwapatia fursa ya kumiliki ardhi."Pia tunampongeza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alituahidi kupata eneo jipya na tumepata na hatimiliki na tumepata maeneo ambayo tunauhuru zaidi na tumepata maeneo ambayo hakuna baridi kama Ile baridi ya Ngorongoro ilivyokuwa .

"Tumepata maeneo ambayo tuko huru , kwani ukiamua kutoka Msomera kwenda Handeni unaweza kwenda muda wowote na kurudi wala wa kusema muda huu hauruhusiwi au kibali kiko wapi hakuna, yaani Sheria za wanyamapori hapa hazipo , tunashukuru Mwenyezi,na nampongeza Rais hasa hili la kusema ukweli kwaababu miaka mingi imepita watu wanataka ardhi ya Ngorongoro.

"Lakini ardhi ya Ngorongoro ishakuwa kwenye mikataba ya UNESCO na tumeshakuwa kwenye mikataba ya kimataifa ni ngumu kuwa na ardhi na sasa Serikali yetu imetupa nafasi ya kuwa na ardhi, tunaifurahia.Namwambia mfugaji mwenzangu huku ng'ombe wamenawiri na wafugaji waliopo hapa ni Wamasai wenzetu

"Tunaweza kuongea nao lugha moja na tunaweza tukasema wapi kwa malisho, wapi kwa kulima , wapi pa kuishi na tunaweza kujuliana hali ,kwa hiyo namshukuru sana Rais Samia na Watanzania wote.Namshukuru Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwasababu alisema tuwe na imani na uongozi wa Rais Samia na sasa tumepata imani na uongozi kwasababu tuko huru, "amesema

Ameongeza wamepata ardhi maeneo ya kuweka mifugo yao lakini na watoto wao watasoma kwa uhakika huku akieleza kwa takribani miaka yote ambayo nimeishi NGORONGORO yeye na baba yake na Babu yake hawajawahi kumiliki ardhi.

"Tulihamia Ngorongoro Creater tukitokea Serengeti na sasa tuko Handeni, nimefurahi sana maana ninauwezo wa kumuachia mtoto wangu ardhi kwa ajili ya shamba au makazi kwwsababu tuko huru lakini kule Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imewabana sana wafugaji kwani hawako huru.

"Hapa tumepata nyumba nzuri sana katika kuanzia maisha, nimepata nyumba ya vyumba vitatu lakini kesho na keshokutwa mtoto wangu akisoma anaweza kujunga nyumba ya vyumba 10 au hata Ghorofa kwasababu ardhi ipo.Muhimu sio nyumba ila ni kumiliki ardhi.kwa hiyo nashukuru Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na uongozi wake na wasiogope changamoto hizi maana zipo tu."

Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Handeni Abel Busalama amesema Serikali imefanya maandalizi yote muhimu kwa ajili ya wakazi wa Kijiji hicho."Tulichowaandalia ni nyumba za kuishi na kwa kila familia, kwa Wamasai wenye mke zaidi ya mmoja kila mke anakuwa na nyumba lakini nyumba hiyo iko kwenye eneo lenye ukubwa wa hekari tatu ambapo anaweza kuongeza nyumba zingine hata zile za kienyeji bado anaweza kujenga pale.

"Pia tumewaandalia hekari tano kwa kila familia kwa ajili ya kilimo wakati kule Ngorongoro hawakupewa nafasi hiyo lakini katika Kijiji Cha Msomera watakuwa na hatimiliki, tumewaandalia eneo lenye malisho,maji ya kutosha,kwa hiyo tunawakaribisha hapa maisha yatakuwa burudani.

"Tunapowapokea cha kwanza tunachowahakikisha ni usalama wao, hili eneo liko salama kabisa na huduma zote za kibinadamu walizokuwa wanaweza kuzipata wakiwa Ngorongoro na hapa zinapatikana lakini katika ubora zaidi.Wananchi hawa ambao wamekuja hapa hata wenyeji waliowakuta ni jamiii ya Wamasai hivyo hakuna tofauti na walivyokuwa Ngorongoro.
Miundombinu ya barabara ikiwemo madaraja ikiendelea kujengwa usiku na mchana kuhakikisha kijiji cha Msomera ,Handeni mkoani Tanga kinakuwa tayari na kukamilika kwa ajili ya kuwapokea Wananchi wanao endelea kuhama kwa hiyari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kupisha shughuli za Uhifadhi.PICHA ZOTE NA MICHUZI JR-MSOMERA


Maji tayari yamefika katika kijiji cha Msomera

Miundombinu ya usambazaji maji ikiwemo kuweka matenki ya kusambaza maji maeneo mbalimbali katika kijiji cha Msomera ukiendelea kujengwa



Uunganishaji wa miundombinu ya kupitisha maji ikiendelea kuwekwa sawa kuhakikisha upatikani wa maji unakuwa ni wa asilimia 100 ndani ya kijiji hicho

Kijiji cha Msomera pia tayari kimefikiwa na mawasiliano,kama uonavyo pichani mmoja wa Wakala wa kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel akimsajilia laini ya simu mmoja wakazi wa Msomera tayari kwa kuwasiliana na ndugu jamaa na marafiki popote pale

Baadhi ya nyumba zinazoendelea kujengwa ndani ya kijiji cha Msomera,ambapo JKT wanatarajia kujenga nyumba 500 zitakazotumika kuishi Wananchi wanaohama kwa hiyari kutoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Kijiji cha Msomera Martin Oleikayo Paraketi alipokuwa akizungumza mambo mbalimbali na Waandishi wa Habari kuhusu ujio wa Wageni wake ambao ni Wananchi wanaohama kwa hiyari kutoka Ngorongoro,ambapo amesema tayari awamu ya kwanza wamepokea wageni kaya 21 yenye watu 111 na awamu ya pili Juni 23,2022 wamepokea kaya 27 zenye watu 127 pamoja na mifugo 488.
PICHA ZOTE NA MICHUZI JR-MSOMERA

Wakaazi waliohamia kijiji cha Msomera wakiendelea na shughuli zao za kila siku

Eneo la Muda kwa ajili ya kunyweshea mifugo,wakati maeneo ya kudumu yakiendelea kujengwa ndani ya Msomera.

Wakazi waliohamia kijiji cha Msomera kutoka Ngorongoro wakiendelea kujiandikisha tayari kwa taratibu za kukabidhiwa hati za umiliki wa maeneo yao ikiwemo nyumba na shamba



Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Mhe.Abel Busalama akisaidiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama akiongoza kuwapokea Wananchi wakaazi waliohama kwa hiyari kutoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuelekea kijiji cha Msomera Handeni mkoani Tanga,ikiwa ni awamu ya pili ambapo kaya 27 zenye watu 127 pamoja na mifugo 488 ziliwasili

Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Mhe.Abel Busalama akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni,mbele ya Wananchi wakaazi waliohama kwa hiyari kutoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuelekea kijiji cha Msomera Handeni mkoani Tanga kupisha uhifadhi.
PICHA ZOTE NA MICHUZI JR-MSOMERA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...