Na Said Mwishehe, Michuzi TV
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma imesema baada ya wakulima wa wilaya hiyo kupata mafunzo yanayohusu kilimo cha kisasa na chenye tija yaliyokuwa yanatolewa na WFP yamesaidia kuongezeka kwa mapato ya halmashauri hiyo.
WFP ambao ni Shirika la Mpango wa Chakula Duniani wamekuwa wakitoa mafunzo yanayohusu kilimo kuanzia hatua ya uandaji shamba, upandaji,uvunaji na uhifadhi sambamba na kutoa vifaa na ukarabati wa maghala ya kuhifadhi mazao ya wakulima.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Kakonko , viongozi wa vyama vya ushirika pamoja na wakulima walioko kwenye mradi huo unaofahamika zaidi kwa jina la Kigoma Pamoja wamesema kwa sasa kilimo kimeanza kulipa na watu wote wananuifaka nacho.
Akizungumza kuhusu WFP, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Mallasa amesema moja na eneo ambalo wamesaidiwa ni uwezeshaji kwa wakulima wa mazao yakiwemo Maharage na Mahindi.
“WFP wamekuwa ni wadau katika kusaidia na kuanzisha vyama vya ushirika hasa AMCOS, lakini wamekuwa na michango mikubwa kwa maana ya kutoa mafunzo kwa wakulima.Mara kadhaa wamesaidia vifaa kwenye maghala kupitia hizi AMCOS.
Kwa upande wake Ofisa Kilimo,Umwagiliaji na Ushirika Wilaya ya Kakanko Khalfan Muhidin amesema wamekuwa wakishirikiana na wadau wa maendeleo walioko kwenye mradi wa KGP na kwa upande wa kilimo wamekuwa na WFP na FAO.
“WFP tumekuwa tunafanya nao kazi vizuri, kwa kushirikiana nao tumetoa elimu kwa wakulima inayohusu uhifadhi bora wa mazao kwa kutumia mbinu na teknolojia ya kisasa kuzuia upotevu wa mazao ikiwemo kutumia mifuko ya kikinga njaa.
“WFP wametusaidia hata kutuunganisha na masoko na wenyewe pia wamekuwa wakinunua mazao pale kila wanapohitaji.Katika kuendeleza hii AMCOS ya Muungano wameweza kununua tani 373 za maharage,”.
Amesema mafanikio ya uwepo wa WFP na mradi wao wa kuendeleza kilimo mbali ya kuwa na manufaa kwa wakulima, pia umewezesha kuongeza kwa mapato ya halmshauri yanayotokana na ushuru wa mazao.
“Kabla ya mradi mapato yaliyokuwa yanapatikana kupitia mazao yalikuwa chini kwa mwaka ilikuwa haizidi sh.milioni 5, baada ya mradi na soko kueleweka tumekusanya ushuru wa Sh.milioni 21.8, kwa mwaka.
“Haya ni mafanikio makubwa kwetu lakini wakulima nao wameuza kilo moja ya maharage kwa Sh.1950 na walionunua ni hao hao WFP.Fedha hiyo ya ushuru ambayo tumekusanya ni katika AMCOS moja tu lakini tayari kuna AMCOS nyingine tumeanzisha,’amesema Muhidin.
Mwenyekiti wa Muungano Kiziguzigu AMCOS Jackson Christopher Bujege amesema kupitia mradi wa Kigoma Pamoja wamesaidia mambo mbalimbali yanayohusu kilimo.“Mradi huu umesaidia kwa kiasi kikubwa kutuunganisha wakulima ukilinganisha na huko nyuma.
“WFP wametuletea vifaa kwa ajili ya shughuli za kilimo, lakini wamekuwa wakinunua maharege yetu , katika msimu wa kwanza tumewauzia tani 100 na msimu wa pili tani 268 za maharage na msimu huu tunatarajia kuuza tani 400.Tumewahi kuwauzia WFP maharage yenye thamani ya Sh.milioni 717 .Katika ushirika wetu tuko wanachama 308,”amesema.
Aidha amesema iwapo WFP watajitoa kwenye mradi huo, wakulima wanaweza kujiendeleza kwani wamepatiwa mafunzo yanayohusu kilimo , biashara na kutafuta masoko, hivyo hata wakiondoka wanaweza kujiendeleza.
Wakati huo huo mmoja wa wakulima ambao ni miongoni mwa wanufaika wa mafunzo ya mradi huo Frola Barnabas wa Kijiji cha Gwarama wilayani Kakonko amesema kabla ya mafunzo alilima heka tatu lakini akapata mahindi gunia sita, baada ya mafunzo amelima heka moja na amevuna gunia 22.
“Huko nyuma tulikuwa tunalima kilimo cha mazoea, lakini msimu huu nimelima kwa kufuata maelekezo ya watalaamu wa kilimo, nimelima heka moja lakini nimevuna gunia 22 za mahindi.
Amesema mafunzo waliyopewa yalihusisha hatua mbalimbali kuanzia upandaji, uangalizi wa shamba, uvunaji pamoja na kuhifadhi.“Pale niliona kuna wadudu shambani niliwaita wataalamu wa kilimo wanishauri.Ukweli mafunzo ya WFP yametusaidia sana wakulima wa Kakonko.”
Jengo la ghala la kuhifadhi mazao ya chakula ambalo limekarabatiwa na Shirika la Mpango wa Chakula ( WFP) kama kupitia Mradi wa UN Kigoma Pamoja . Ghala hilo linatumiwa na wakulima kuhifadhi mazao yao wakati wanasubiri wanunuziOfisa Kilimo,Umwagiliaji na Ushirika katika Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma Khalfan Muhidin akizungumza na wandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika mradi wa kuwaendeleza wakulima unaofadhiliwa na WFP ambao ni sehemu ya wadau walioko kwenye mradi wa UN Kigoma Pamoja.
Ofisa Kilimo, Ushirika na Umwagiliaji wilayani Kakonko Khalfan Muhidin ( kulia) akiwa makini kumsikiliza mmoja wa wadau wa kilimo baada ya kufika kwenye eneo la ghala la kuhifadhi mazao ya wakulima.Baadhi ya akina Mama walioko kwenye AMCOS ya Muungano Kiziguzigu wilayani Kakonko wakiendelea na shughuli ya kusambaza maharage ambayo wameyaanika kabla ya kuyahifadhi ghalani
Maharage yakiwa yameanikwa kwenye maturubai ambayo ni sehemu ya msaada iliyotolewa na WFP katika kuwasaidia wakulima.
Baadhi ya wakulima wakiweka maharage kwenye kiroba kabla ya kwenda kuhifadhiwa ghalani
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...