RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Mwinyi, amesema kwamba Vyuo Vikuu vya nchi za Afrika vinawajibika kuongeza mashirikiano katika kufuatilia na kudhibiti viwango na ubora wa elimu itolewayo ili ilingane na mahitaji ya sasa kimaendeleo.

Mhe. Dk. Mwinyi ameyasema hayo huko hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege mjini Zanzibar, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, katika ufunguzi wa Kongamano kuhusu viwango vya ubora na ithabati ya elimu ya juu inayotolewa kwenye Vyuo vikuu vya Afrika.

Amesema kwamba ni muhimu kwa Vyuo Vikuu kufanya jitihada hizo za kuwaka itibati na viwango bora vya elimu kwa pamoja ili kuepusha nchi za Afrika kuathiriwa na viwango duni vya elimu na hivyo kuendelea kuachwa nyuma na kushindwa kusonga mbele kimaendeleo.

Aidha amefahamisha kwamba elimu ya juu ni nguzo muhimu katika jitihada za pamoja za kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kwamba mipango maalumu inapaswa kufanywa ili kuwekeza nan a hatimaye kupatikana elimu bora kwenye Vyuo Vikuu vya Afrika.

Amesema kwamba jitihada zinazofanywa na Shirikisho la Kusimamia, ubora na ithibati ya elimu ya Vyuo Vikuu Afrika itawezesha nchi hizo kuzalisha wataalamu bora wa fani tofauti wakaochangia kuharakisha maendeleo ya nchi zao.


Amesema kwamba jitihada za maendeleo zinazofanywa na nchi mbali mbali Afrika, lazima ziwe sambamba na uzalishaji wa wataalamu bora watakaotumika kwenye viwandani na taasisi nyengine za Serikali ili kuongeza kasi ya kukuza maendeleo ya Afrika.

Amezitaka nchi zote Barani Afrika kupitia shirikisho hilo kuhakikisha kwamba, kwa pamoja wanatimiza wajibu wao wa kuvisaidia Vyuo Vikuu kuzalisha wataalamu wanaokidhi vigezo na viwango vya kimataifa kwa fani mbali mbali kwa kuwa wanahitajika sana kimaendeleo.

Amesema sio vizuri kwa Vyuo Vikuu kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi pekee, lakini rasilimali na nyenzo nyengine za kufundishia zikabaki vile vile ama kutokidhi kabisa mahitaji ya kufundishia na hivyo kushindwa kufikia lengo la kuzalisha wataalamu bora wanaohitajika kwa vigezo vya kimataifa.

Amefahamisha kwamba wakati nchi za Afrika zinajitahidi kukabiliana na mabadiliko na changamoto za kiuchumi na kimaendeleo kwenye sekta mbali mbali duniani, elimu yenye kiwango bora inabaki kuwa ni mahitaji muhimu ili kuweza kufikia malengo mbali mbali yanayowekwa.

Aidha amesema kwa kuzingatia kwamba hivi sasa dunia imekabiliwa na changamoto kubwa ya kuwepo ushindani kimaendeleo kupitia ubunifu wa wataalamu ni vyema kufahamu na kutafuta jitiha za pamoja kukuza ubora na viwango vya wataalaamu wanaozalishwa kwenye vyuo vikuu mbali mbali.

Kongamano hilo la siku nne, limewakutanisha wataalamu wa fani mbali mbali wanaosimamia viwango, ubora na ithibati ya elimu ya Vyuo Vikuu kutoka zaidi ya nchi 12 za Afrika limeandaliwa na shirikisho linalosimamia , Ithibati, ubora na Viwango vya Elimu ya Juu Afrika.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano la Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Afrika la Ufuatiliaji wa ithibani na Viwango vya Elimu ya Vyuo Vikuu vya Afrika huko hoteli ya Golden Tulip Kiembe Samaki. Mhe. Othman alimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi leo tarehe 25.7.2022. Picha na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Kitengo cha Habari.
Washiriki mbali mbali kutoka nchi tofauti Barani Afrika waliohudhuria kongamano la siku nne kuhusu ufuatiliaji wa Ithibati na Viwango vya Elimu ya Juu kutoka katika Vyuo vikuu mbali mbali barani Afrika. Kongamano hilo linaendelea katika Hoteli ya Golden Tulip Kiembesaki mjini Zanzibar na Limefunguliwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman. Picha na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Kitengo cha Habari.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...