WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali
waweke msisitizo katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi na
kuhamasisha zaidi upatikanaji wa masoko wa bidhaa za ndani na uwekezaji.
Amesema kuwa maboresho ya sera na mfumo wa uwekezaji uliofanywa
na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania umesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji
nchini.
Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumatatu, Septemba 19,
2022) alipokutana na mabalozi hao ofisini kwake Bungeni jijini Dodoma.
Mabalozi aliokutana nao ni Balozi Caroline Chipeta (Uholanzi), Balozi
Simon Sirro (Zimbabwe) na Balozi Luteni Jenerali Mathew Mkingule
(Zambia),
Amesema Tanzania inahitaji wawekezaji makini
watakowekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, madini na
maliasili. “Tunataka uwekezaji wenye tija ili kuimarisha uchumi wetu,
pia tunataka wawekezaji watakaozalisha bidhaa hapa nchini kwa kutumia
malighafi zetu.”
“Nchi yetu ni moja kati ya mataifa ambayo
jiografia yake imekaa kimkakati, tuna masoko kutoka jumuiya mbalimbali
ikiwemo SADC na EAC, hata mazingira yetu ya uwekezaji ni mazuri, tunazo
ndege, bandari na sasa tunaendelea kufanya maboresho makubwa kwenye
sekta ya nishati.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka mabalozi
hao kuandaa makongamano na vikao vya pamoja vya kibiashara kati ya
wafanyabiashara wa nchi wanazoziwakilisha na sekta binafsi wa nchini
Tanzania.
“Nendeni Mkatafute masoko ya bidhaa zetu za ndani,
shirikini kwenye maonesho yanayoandaliwa ili mtangaze bidhaa zetu,
tunataka wakulima wetu wanufaike kwa kupata masoko kutoka kwenye nchi
mnazokwenda.”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza mabalozi
hao wahakikishe wanalinda taswira ya Tanzania katika nchi uwakilishi
sambamba na kujielekeza katika kuvutia watalii na kuwasaidia
wafanyabiashara wa Kitanzania kufanya biashara nje.
Pia, Waziri
Mkuu amewataka mabalozi hao wakajifunze teknolojia mpya na kuona namna
inavyoweza kuisaidia Tanzania. “Suala hili linaenda sambamba na kutafuta
fursa za masomo kwa vijana wetu katika nchi mnazokwenda.”
Waziri
Mkuu amesema mabalozi hao wanatakiwa kuitangaza lugha ya Kiswahili.
“Naamini mtatumia ushawishi wenu kukitangaza Kiswahili, angalieni namna
ya kuanzisha madarasa ya lugha ya Kiswahili.”
Akizungumza kwa
niaba ya mabalozi wenzake, Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Balozi
Simon Sirro amesema kuwa kutokana na imani kuwa walioneshwa na Rais
Samia watakwenda kufanya kazi na kuhakikisha nchi inanufaika na
uwakilishi wao.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na mabalozi
wa Tanzania walioapishwa hivi karibuni, baada ya kuzungumza nao ofisini
kwake bungeni jijini Dodoma, Septemba 19, 2022. Kutoka kushoto ni Balozi
Simon Siro (Zimbabwe), Balozi Caroline Chipeta (Uholanzi) na Balozi
Luteni Generali Mathew Mkingule (Zambia). (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...