Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WALIMU na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Paul Makonda pamoja na baadhi ya viongozi wa Mitaa na Kata wilayani Kigamboni Mkoa wa Dar es Salaam wamepata mafunzo kuhusu kulinda usalama wa taarifa binafsi wanapotumia Intanert.
Mafunzo hayo yametolewa na watalaamu wa Internet Society Tanzania Chapter(ISOC-Tz) wakiongozwa na Rais wao Nazar Kilama pamoja na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usalama Mtandao Mhandisi Stephen Wangwe aliyezungumzia Muswada wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi ambao umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni ili ujadiliwe na kisha ipatikane Sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi.
Akizungumzia mafunzo hayo Rais wa Internet Society Tanzania Nazar Kilama amesema washiriki zaidi ya 60 wakiwamo walimu, wanafunzi pamoja na viongozi wa mitaa na kata katika Wilaya ya Kigamboni wameshiriki na miongoni mwa mambo waliyojifunza ni namna ya kutumia kulinda taarifa binafsi unapotumia mtandao.
“Tulikuwa na mawasilisho mawili na moja lilihusu Muswada wa Usalama wa taarifa binafsi na tunaishukuru Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushiriki na sisi na kufanya wasilisho hili ambalo limedadavua kilichomo kwenye muswaada wa usalama wa taarifa binafsi kwani limekuwa jambo jema kwetu.
“Pia washiriki wamejifunza masuala ya usalama wa taarifa zao wanaposhiriki kwenye dunia hii ya kidigitali na tumeona pia wengi wao wamepata taarifa mpya kuhusu shughuli zinazohusiana na ulinzi na usalama wa taarifa binafsi mtandao.
“Ukijaribu kuangalia wengi ambao leo wameshiriki mafunzo haya walikuwa hawajui suala hili la muswada ambao umeshapelekwa bungeni na kusomwa mara ya kwanza, kwa hiyo tunafurahi kuona wameshiriki na kupata taarifa kuhusu huo muswada,”amesema Nazar.
Aidha amesema mafunzo hayo yamekuja wakati sahihi kwani Oktoba huwa ni mwezi wa Usalama Mtandaoni , hivyo wamefundisha kuhusu utunzaji taarifa kutoka mtu mmoja kwenda mwingine kidigitali.
“Internet Society Tanzania Chapter(ISOC-Tz)tutaendelea kuwashirikisha wananchi hasa wa ngazi za mitaa , kata , watendaji , shuleni na vijana walioko vyuoni na mtaani ili wajifunze kwani kujifunza ni nusu ya kuhakikisha usalama wa taarifa zao wanapotumia mitandao ya kijamii hasa Internet,”amesema.
Awali Mkuu wa Shule ya Sekondari Makonda Fulgesi Daudi amesema wamefurahi kuona walimu na wanafunzi wa shule hiyo wakipata mafunzo ya kufahamu namna ya kulinda usalama wa taarifa zao kwenye mtandaoni.
Amesema mafunzo hayo yamekuwa jumuishi na kitendo cha kuwafundisha walimu, wanafunzi pamoja na viongozi wa Serikali za mitaa ni jambo muhimu kwani nyuma yao kuna kundi kubwa.“Ubunifu huu tunaomba uendelee kwani unawafikia watu wengi kwa wakati mmoja, kupitia mafunzo haya pia tumejifunza kuhusu Muswawa wa Ulinzi wa taarifa binafsi.
“Ndani ya Muswada huo tumeona kuna mambo ya kujifunza, kuna kipengele kinachoelezea Serikali itakuwa na uwezo wa kuchukua taarifa za mtu binafsi pale wanapoona kuna ulazima wa kufanya hivyo kwa maslahi mapana ya Taifa,”amesema.
Ameongeza maana yake ni lazima wananchi wake makini na matumizi ya mitandao kwani siku hizi kumekuwa na ushabiki mwingi mitandaoni , hivyo bila kuchukua tahadhari wataingia matatizoni.Rais wa Internet Society Tanzania Nazar Kilama(waliokaa kulia) na Mkuu wa Shule ya Sekondari Paul Makonda, Fulgesi Daudi(aliyekaa kushoto) pamoja na walimu wengine, viongozi wa Mtaa na Kata wilayani Kigamboni na baadhi ya wanafunzi wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa mafunzo yaliyohusu utoaji elimu kuhusu njia sahihi za kulinda taarifa binafsi kwenye mitandao ya kijamii.
Rais wa Internet Society Tanzania Nazar Kilama akielezea umuhimu wa utunzaji taarifa pindi unapotumia mtandao wa kijamii kwa walimu, wanafunzi pamoja na viongozi wa mitaa na kata katika Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam.
Baadhi ya wanafunzi, walimu na viongozi wa mitaa na kata wakifuatilia mafunzo ya utunzaji taarifa binafsi mtandaoni.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Paul Makonda iliyopo Kigamboni mkoani Dar es Salaam Fulgesi Daudi akifafanua jambo wakati wa mafunzo hayo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Paul Makonda iliyopo Kigamboni Fulgesi Daudi(kushoto) akijadiliana jambo na mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo.(PICHA ZOTE NA SAID MWISHEHE) Mmoja ya viongozi wa Serikali za Mtaa wa Kigamboni akifafanua jambo wakati wa mafunzo hayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...