Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

Wekundu wa Msimbazi, Simba SC wamepata sare nyingine ya nne katika mfululizo wa michezo ya Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (NBC Premier League) baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mbeya City FC kwenye dimba la Sokoine jijini Mbeya.

Katika mchezo huo uliokuwa wa kasi muda wote wa dakika 90, Simba SC walianza kupata bao la kuongoza kupitia kwa Kiungo Mkabaji, Mzamiru Yassin dakika ya 15 baada ya kupokea ‘Pasi’ safi ya Mshambuliaji John Raphael Bocco.

Mchezo huo ulienda mapumziko kwa Simba SC kuongoza bao 1-0 kwenye dimba hilo la Sokoine, kipindi cha pili, Wana Koma Kumwanya walirudi kwa kasi na kuishika Simba SC, ambapo dakika ya 78, walisawazisha bao hilo kupitia kwa Mshambuliaji Tariq Seif Kiakala.

Simba SC wamepata sare hiyo ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City baada ya ile dhidi ya Singida Big Stars (1-1) kwenye uwanja wa CCM Liti, mkoani Singida, dhidi ya KMC FC (2-2) kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na sare nyingine dhidi ya Yanga SC (1-1) kwenye uwanja huo wa Benjamin Mkapa.

Simba SC wamepoteza mchezo mmoja dhidi ya Azam FC kwenye michezo yake 13 ya Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Azam FC walipata ushindi wa bao 1-0 kwenye uwanja Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, bao lililofungwa na Mshambuliaji Prince Dube.

Kwenye msimamo wa Ligi hiyo ya NBC, Simba SC wapo nafasi ya tatu wakiwa na alama 28 na michezo 13, Azam FC nafasi ya pili wenye alama 29 kwenye michezo 13, nafasi ya kwanza ni Yanga SC wenye alama 29 na michezo yake 11.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...