Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametoa rai kwa wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa miradi ya kimkakati katika jiji la Dodoma kuzingatia ubora na viwango katika kukamilisha miradi kwa wakati.
Mhe. Senyamule ameyasema hayo
leo Februari 15, 2023 wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi
wa miradi hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Msalato,
barabara ya mzunguko LOT 1 inayotoka Nala-Veyula-Mtumba-Ihumwa yenye urefu wa
kilometa 52.3 na LOT 2 yenye urefu wa Kilometa 60 inayotoka Dry pot Ihumwa, Ngo’ngo’na,
Matumbulu, Bihawana – Nala.
“Mradi huu ni wa aina yake barani Afrika tunampongeza sana Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za kukamilisha ujenzi wa kilometa 112.3 km za barabara za mzunguko ndani ya Mkoa wa Dodoma” Amefafanua Mhe. Senyamule.
“Sisi tunataka miradi yetu ikamilike
ndani ya muda, sote tunafahamu miradi hii muhimu inatakiwa kukamilika 2024 au mapema
2025 kama mkataba unavyoonyesha. Dhamira ya serikali ni kusogeza huduma kwa
wananchi na kuhikisha utekelezaji wa miradi hii unanufaisha wananchi ikiwa ni
pamoja na kuzingatia utoaji wa huduma kwa jamii (CSR) kwa kuzingatia Sheria, Taratibu
na miongozo iliyopo. Hatutamani sana tunaanza vizuri tunafika mahali tunaanza
kutoa sababu nyingi, changamoto zitatueni lakini zisipelekee kuongeza muda wa
mradi kukamilika’’ Alisisitiza Mhe Senyamule.
Akiwa katika eneo la ujenzi
wa uwanja wa ndege wa Msalato unaojengwa na Mkandarasi kutoka China Mhe Senyamule
amemtaka Mkandarasi huyo
kuongeza kasi ya ujenzi wa jengo la abira ili liweze kukamilika kwa wakati na kwenda
sambamba na ujenzi wa njia za kuruka na kutua ndege.
“Hii miradi inabidi iende sambamba, hatuwezi kukamilisha mradi mmoja
nakuanza kuutumia maana yote inategemeana, hakuna mkwamo wowote fedha za ujenzi
zipo, sisi tunahakikisha kazi inaendana na kasi, lazima wakandarasi wajue
matamanio ya Serikali, fanyeni kazi usiku na mchana” Amesisitiza Mhe.
Senyamule.
Mradi wa Ujenzi wa uwanja wa ndege wa
Msalato Lot 1 sehemu ya kwanza utagharimu
kiasi cha shilingi Bilioni 165 na Lot 1 sehemu ya 2 utagharimu kiasi cha
Shilingi Bilioni 199
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe.
Jabir Shekimweri ametoa rai kwa Mkandarasi huyo kuhakikisha anazingatia Mpango
wa Usimamizi wa Mazingira ili miundombinu inayojengwa hususan madaraja yaweze kupitisha
maji kikamilifu bila kuathiri wananchi na mazingira kwa upande wa pili.
Katika ziara ya siku moja ya kutembelea miradi
ya kimkakati ndani ya Mkoa wa Dodoma, Mhe. Mkuu wa Mkoa alimbatana na Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akikagua
maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato ambao ujenzi
wake umefikia asilimia 11.7 na utakapokamilika utaruhusu ndege 13 kutua kwa
wakati mmoja na utahudumia abiria Milioni 1.5 kwa kutumia mageti 8. Mhe.
Senyamule amemtaka Mkandarasi wa ujenzi kufanya kazi usiku na mchana ili
kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
Mhe. Rosemary Senyamule akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara za mzunguko katika Jiji la Dodoma Lot 1 kutoka
Nala-Veyula-Mtumba-Ihumwa yenye urefu wa kilometa 52.3 ambao ujenzi wake
umefikia asilimia 21.3 na unatarajia kukamilika Desemba 2024. Mradi huo unagharimu
kiasi cha Shilingi Bilioni 100.8. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir
Shekimweri
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...