Na Mwandishi wetu, Mirerani
DIWANI wa Viti Maalum Tarafa ya Moipo, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Paulina Makaseni ameipongeza kampuni ya Franone Mining & Gem Ltd inayochimba madini ya Tanzanite kwenye kitalu C na D, kwa kutoa kipaumbele kwa wanawake wanaochekecha kwa kuwapa mchanga.
Diwani huyo Paulina amesema wamiliki wa migodi, wachimbaji na wadau wa madini ya Tanzanite wanapaswa kuiga mfano wa kampuni ya Franone inavyowajali wanawake.
“Tunawashukuru viongozi wa kampuni ya Franone hususani Mkurugenzi wake Onesmo Mbise kwa kuwapa mchanga wanawake wachekechaji ili wajitafutie riziki zao,” amesema Diwani Paulina.
Hata hivyo, ametoa wito kwa wanawake wachekechaji kupendana na kuwa na umoja katika shughuli zao ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na waepuke migogoro na migongano.
Mwenyekiti wa jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania wa CCM (UWT) Kata ya Endiamtu, Claudia Dengesi amesema hatua ya kampuni ya Franone kuwapa mchanga wanawake hao inapaswa kupongezwa.
“Wanawake hivi sasa ndiyo wanalea familia zao hivyo tumpongeze Mkurugenzi wa Franone, Onesmo Mbise kwa kuwasaidia kina mama hao wachekechaji,” amesema.
Mwenyekiti wa jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania wa CCM (UWT) Kata ya Mirerani, Johari Mwaselela amewaomba wamiliki wa migodi ya Tanzanite wawe wanaotoa mchanga wenye mabaki mengi ya madini.
Mwaselela amesema wamiliki hao wakiwapa wanawake hao udongo uliotoka kwenye buti hawatakuwa wanafanya jambo sahihi hivyo waige mfano wa mkurugenzi wa Franone.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...