MBUNGE wa Vitimaalum Dodoma (CCM), Fatma Toufiq, ameahidi kushughulikia changamoto ambazo zinaikabili shule ya msingi maalum ya Buigiri iliyopo Chamwino mkoani Dodoma ikiwemo ujenzi wa ukuta na matibabu.Toufiq aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati SAMAF wakikabidhi msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo madaftari, taulo za kike, mafuta maalum kwa watoto wenye ualbino, fimbo za wasioona, soski, penseli na kalama kwa watoto walemavu na wenye mahitaji maalum katika shule hiyo.

Alisema changamoto alizojulishwa shuleni hapo zilizo nje ya uwezo wake atakwenda kuziwasilisha katika mamlaka husika ili zifanyiwe kazi.

Aidha, ameupongeza Umoja wa Wanahabari Wanawake Tanzania (UWWT) chini ya Taasisi ya Sauti ya Matumaini (SAMAF), kwa utayari wao na kuwa mstari wa mbele katika suala la kuisaidia jamii hasa kundi la watoto walemavu na wasiojiweza.

Toufiq alisema kujitokeza kwa wanahabari hao kutoa msaada huo, kunaonesha utayari wao katika kusaidia jamii, hivyo amewataka waendelea kutumia kalamu zao kuhabarisha umma juu ya umuhimu wa kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum.

Alisema licha ya jitihada mbalimbali zinazofanya na serikali ni muhimu kwa wadau wengine kuendelea kujitokeza kuwasaidia watoto hao wenye ulemavu ili waweze kupata elimu na malezi bora yatakayowawezesha kutimiza ndoto zao na hatimaye kutoa mchango wao katika maendeleo ya nchi.


"Nawapongeza wanahabari hawa kwa kumtumia kalamu zao kuelimisha jamii lakini pia kuwa sehemu ya kusaidia jamii hasa kwa kundi hili la watoto walemavu na wasiojiweza, hawa ni watoto wetu na wana haki sawa kama walivyo wengine hivyo tunaowajibu wa kuendelea kuwasaidia ili waweze kutimiza ndoto zao,"alisema Toufiq na kuongeza kuwa;

"Nawashukuru SAMAF kwa upendo wenu mlionao mnafanya kazi kubwa sana ya kurejesha tabasamu na matumaini kwa jamii, sisi Serikali tutaendelea kuzifanyia kazi zile changamoto mbalimbali ambazo zinazikabili kundi hilo,".

Naye Mwenyekiti wa SAMAF, Mary Geofrey alisema lengo la kutoa misaada hiyo ni kurudisha tabasamu kwa wanafunzi wanaoishi mazingira magumu na watoto wenye ulemavu ili nao kujiona ni sehemu ya jamii inayothaminiwa na kupewa kipaumbele kama watoto wengine.

"Tunaamini msaada huu utakuwa chachu ya wanafunzi hawa kuongeza juhudi za masomo ili kufikia ndoto na malengo waliyojiwekea bila kujali changamoto zao. Umoja huu ambao tumekuwa tukitumia kalamu kama kiunganishi kati ya serikali na jamii na wadau wengine, tumeamua sasa kujitoa kwa vitendo kuifikia jamii ya makundi maalum kwa nia ya kuunga mkono juhudi za serikali za kuwaletea Watanzania wote maendeleo bila kubagua makundi yenye mahitaji," alisema Mary.

Mary aliiomba serikali kuendelee kutoa mahitaji muhimu ya chakula, vifaa vya kujifunzia kwa kundi hilo ili kuendelea kuwapunguzia changamoto zinazowafanya washindwe kuendelea na masomo.

Aidha, Mary alilishukuru Taasisi ya Disability Hope (FHD) kwa kushirikiana nao katika kutoa misaada hiyo na kufanikisha hafla hiyo.

Mtendaji Mkuu wa SAMAF, Penina Malundo, alisema umoja huo utaendelea kusaidia kundi la watoto wenye ulemavu, wasiojiweza na wanaoishi katika mazingira magumu na kuwaomba wadau kusaidia wenye uhitaji.

"Tumefanya jambo hili kuunga mkono jitihada za Rais Samia katika kuhakikisha wanafunzi wote wanakuwa na mazingira bora wawepo shuleni hususani katika shule zenye elimu Jumuishi. Asante Mbunge Toufiq na uongozi wa Wilaya ya Chamwino pamoja na Shule ya Buigiri kwa kukubali kupokea msaada huu," alisema Penina.









Mwenyeikiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii na Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Dodoma, Fatma Toufiq, akimuongoza mwanafunzi wa Shule ya Msingi Maalum ya Buigiri, mara baada ya kukabidhi msaada wa fimbo za wasiyoona pamoja na vifaa vingine.( Na Mpiga picha wetu)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...