* Wanawake wahimizwa kutumia fursa za ubunifu na kutumia teknolojia kwa matokeo chanya

TANZANIA itaendelea kushirikiana na mashirika ya kimataifa ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa (UN,) Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women)UN Global Compact na International Finance Corporation katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ikiwemo kukomesha umaskini, usawa wa jinsia, ulinzi na usalama pamoja na utunzaji wa mazingira kupitia mpango mkakati wa mwaka 2015.

Akizungumza katika hafla ya sita ya kuchochea ushiriki wa wanawake katika kukuza uchumi na maendeleo endelevu 'Ring the Bell For Gender Equality' sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania Latifa Khamisi amesema nafasi ya mwanamke ni muhimu katika jamii na Taifa kwa ujumla hususani katika ukuaji wa uchumi na kueleza kuwa ili kufikia usawa wa kijinsia ni jukumu la kila mmoja kufanyia kazi changamoto ili kufikia malengo ikiwemo kuziba pengo la kidigitali kwa kutoa fursa kwa wanawake na mabinti kupata maarifa na kuweza kunufaika na fursa za ubunifu na teknolojia.

"Tanzania tupo katika nafasi nzuri ya utekelezaji wa usawa wa jinsia kwa vitendo katika nyanja zote na dhamira ya Serikali ni kuleta matokeo chanya....Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mfano wa kutekeleza hili kwa vitendo ndani na nje ya Serikali, wadau na jamii kwa ujumla tuunge jitihada hizi kwa kujenga uelewa na fursa kwa mafanikio zaidi." Ameeleza.

Kuhusiana na kauli mbiu ya maadhimisho hayo iliyolenga ubunifu na teknolojia kwa usawa wa kijinsia amesema imelenga kuangaalia namna ubunifu na teknolojia vilivyo na nafasi kubwa katika kufikia usawa wa jinsia na kufikia malengo mbalimbali ya kijamii na uchumi ikiwemo uboreshaji wa huduma za afya, elimu kwa kuwahimiza wanawake na mabinti kujikita katika masomo na fursa za ubunifu na teknolojia pamoja na wanawake kuripoti visa na matukio ya unyanyasaji wa kijinsia kupitia 'App' bunifu mahususi kwa wanawake na mabinti kuripoti visa na matukio ya unyanyasaji.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE,) Mary Mniwasa amesema, kila mwaka wanaungana na masoko ya Hisa takribani 60 duniani katika tukio hilo la 'Ring the Bell For Gender Equality' katika sekta ya fedha ambayo uwakilishi wa wanawake bado upo chini ambapo katika nafasi za juu uwakilishi wa wanawake ni asilimia 21 pekee na kwa DSE ni asilimia 14.

Kwa upande wake mtaalam wa program ya uwezeshaji wanawake kiuchumi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN- Women,) Lilian Mwamdamga amesema, katika maadhimisho hayo kwa mwaka huu mada kuu imeelekezwa katika kushirikisha na kihimiza nafasi ya mwanamke katika masuala ya teknolojia, digitali na ubunifu.

"Tumetoka na mengi katika hafla hii, tumeona ujuzi na uwezo walionao wanawake katika masuala ya teknolojia, uongozi na ubunifu pamoja na hamasa wanayoitoa kwa wanawake katika jamii." Amesema.

Ameeleza, nafasi ya sekta binafsi katika kusukuma gurudumu la maendeleo pamoja na uwekezaji wanawake ni mkubwa

"Tumeangazia nafasi za sekta binafsi na kutoa wito kwao kuendelea kuwapa nafasi wanawake katika nafasi mbalimbali ikiwemo uongozi, masuala ya teknolojia pamoja na kubuni na kuzingatia uhitaji wa wanawake na wasichana katika utekelezaji wa teknolojia na bidhaa zake, usalama, uwezo, ushiriki na ubunifu kwa ujumla." Amesema.

Kuhusiana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayowalenga wanawake na wasichana nchini inayofadhiliwa UN- Women Tanzania Bi. Lilian amesema, wanashirikiana na sekta binafsi, Serikali kupitia Wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Jinsia na Habari katika kuhakikisha fursa ya kiuchumi zinapita kwa wanawake wengi zaidi Tanzania bara na visiwani Zanzibar.

Awali Mkurugenzi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN,) nchini Zlatan Milisic alieleza kuwa mabadiliko ya mtazamo yanahitajika ili kuziba pengo la usawa wa jinsia kidigitali kwa kuboresha usalama pamoja na upatikanaji wa zana za kidigitali sambamba na kuhakikisha ushiriki kamili wa wanawake na mabinti kwa kuzingatia haki za binadamu, uvumbuzi, ushirikishwaji na ubunifu.

Grace Munisi, mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Jukwaa la Kizazi chenye Usawa aliyeteuliwa na Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan, ameeleza kuwa, ajenda ya usawa wa jinsia inahakikisha kuwa matumizi ya teknolojia na Ubunifu vinawekwa katika nyanja zote kwa kushirikiana na wadau pamoja na sekta binafsi ambao wametoa mchango mkubwa wa kujenga uelewa kuhusu matumizi chanya ya teknolojia pamoja na kuwawezesha na kuboresha haki za wanawake kiuchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa UN Global Compact, Bi. Marsha Macatta-Yambi amehimiza makampuni nchini kutia saini Kanuni za Uwezeshaji kwa Wanawake, Mkataba wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa na Mpango wa UN Women ili kusaidia kampuni kwa kuhakikisha kuwa biashara zao zinatekelezwa kwa kuzingatia usawa wa kijinsia. Na kueleza kuwa zaidi ya kampuni 2,000 duniani kote zimetia saini makubaliano hayo na Benki ya Stanbic Tanzania imekuwa mmoja wa watia saini wapya zaidi katika hafla hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Stanbic Tanzania Kevin Wingfield amesema wapo nchini kwa miaka 27 na wataendelea kuwezesha zaidi hususani biashara kupitia huduma za kifedha hususani kwa wanawake na kueleza kuwa utiaji saini makubaliano hayo ni heshima na wanaamini utaboresha zaidi utamaduni na juhudi zao za kuimarisha usawa wa kijinsia.

Leah Mwandamseke muongozaji wa filamu kupitia kampuni ya Lamata Village Entertainment kwa kuwahimiza wanawake na mabinti kukomesha uoga na kutumia teknolojia kwa matokeo chanya.

"Katika tasnia ya filamu nchini wanaume walianza kuigiza na kuwa waongozaji filamu lakini si wanawake...nilipambana na kujifunza zaidi hadi kufikia hapa na kuajiri vijana 100 kupitia filamu." Amesema.

Amewataka wadau wa kada mbalimbali kuhimiza na kuelimisha mabinti kutumia fursa za teknolojia ili kuleta matokeo chanya na yenye tija kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Hafla hiyo imeandaliwa na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE,) kwa kushirikiana na UN -Women, IFC, UN Global Compact na kudhaminiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL kupitia T-PESA na benki ya Stanbic Tanzania.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE,) Latifa Khamisi akizungumza wakati wa hafla hiyo na kueleza kuwa Tanzania inatekeleza usawa wa kijinsia kwa vitendo na kuwataka wadau hao kuunga mkono jitihada za Serikali katika kujenga uelewa zaidi na fursa za ubunifu na teknolojia kwa wanawake na mabinti, Leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic Tanzania Kevin Winfield akifuatilia hafla hiyo, Winfield amesema wataendelea kushirikiana na kuwezesha wanawake kupitia biashara na huduma za kifedha, leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN,) nchini Zlatan Milisic akizungumza wakati wa hafla ya na kueleza kuwa mabadiliko ya mtazamo yanahitajika ili kuziba pengo la usawa wa kijinsia kidigitali, leo jijini Dar es Salaam.

Mjumbe wa kamati ya kitaifa ya ushauri kuhusiana na kizazi chenye usawa Grace Munisi akizungumza wakati wa hafla hiyo na kuwataka wadau kuwawezesha wanawake katika matumizi chanya ya teknolojia.







Matukio mbalimbali wakati wa hafla hiyo iliyofanyika leo katika ukumbi wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE.) Jijini Dar es Salaam.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...